Dar es
Salaam Jumamosi 19 Juni 2021. Equity Bank
Tanzania imeendelea kuonyesha dhamira ya kuwanyanyua kiuchumi wafanyabiashara
wadogo maarufu kama Wamachinga kwa kuendesha
kongamano kwa viongozi wa Masoko na wafanya biashara
zaidi ya 250 jijini Dar es Salaam. Semina hiyo iliyofanyika
katika ukumbi wa Golden jubilee, imelenga kutoa mafunzo kwa viongozi hao juu ya mikopo, Bima, na uwekaji wa kumbukumbu za hesabu, ilikusanya wafanyabiashara na wajasiriamali kutoka nyanja tofauti, wakiwemo viongozi wa masoko ya Kariakoo, Feri, Gongo la Mboto, Manzese,
Tegeta, Sinza na mengineyo.
Mgeni Rasmi katika hafla hiyo, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam
Omar Kumbilamoto, alisema kuwa Serikali mkoani Dar es Salaam inapongeza Benki
ya Equity kwa kufanya makongamano ya kuwapa elimu wafanyabishara wadogo ili kuwapa
ufahamu wa masuala ya fedha na uwekezaji. “Naupongeza uongozi wa
Benki ya Equity, kwa ubunifu huu mliokuja nao wa kuanza kuwakopesha
wafanyabishara hawa wadogo kupitia mikopo yenu ya Fanikisha machinga
Loans. Jiji la Dar es
Salaam linaendelea na juhudi za kurasimisha wafanyabiashara wadogo ili kurasimisha biashara zao na hivyo kuwapa fursa ya kupata huduma
kama vile bima za afya
na huduma za mifuko ya jamii. Rai yangu kwenu ni kuhakikisha kuwa mikopo hii na fursa nyingine
za fedha mnazopewa, zitumike kwa miradi stahiki ili kufanikisha malengo. Tumieni
mikopo hii vizuri na pia mkumbuke kulipa kwa wakati ili wengine waweze kukopeshwa” alisema
Mstahiki Meya.
Akizungumza katika warsha hiyo, Mkurugenzi Mwendeshaaji wa Equity Bank Bi.Esther Kitoka alisema “Benki ya Equity inaendeshwa kwa
sera ya kuwawezesha wananchi kwa kuwapatia huduma bora na nafuu za kifedha ili
kuweza kuwakomboa kiuchumi. Moja ya kundi ambalo limekuwa likipewa kipaumbele
ni kundi la wafanyabiashara wadogo maarafu kama wamachinga. Pamoja na ukubwa wa kundi hili, na ukweli kuwa ndio linaloajiri vijana
wengi kuliko kundi lolote, bado limekuwa likibaguliwa na taasisi nyingi za
Fedha kwa kisingizio cha kukosa dhamana. Hivyo Benki
ya Equity imeingiza
sokoni bidhaa ya mikopo iitwayo Fanikisha Machinga loans ikiwa na dhumuni la kutoa mikopo
nafuu kwa wafanyabishara wadogo walio katika mijumuiko yao kama masoko na
maeneo mengine ya majumuiko.
Kwa kuanzia tulianza na wafanyabishara wa masoko ya Kariakoo, Gongo la Mboto na
soko la Samaki Feri. Mikopo hii ya Fanikisha, ina lenga kuwakomboa
wafanyabiashara hawa kwa kuwapa mikopo nafuu kuanzia shilingi laki moja mpaka
milioni moja hadi mbili, kwa kipindi cha miezi mitatu kwa riba nafuu kabisa.
Huduma hii pia huwapa wafanyabiashara hao wigo wa kufanya marejesho kwa kipindi
cha kati wiki moja hadi mbili ili kuwapa nafasi ya kufanya biashara kwa utulivu” alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...