Charles James, Michuzi TV

KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imetembelea eneo la Mtera Mkoani Dodoma na kuridhishwa na elimu inayotolewa kuhusu uvuvi haramu kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao kwenye bwawa la Mtera.

Akizungumza na wavuvi na wananchi wa eneo hilo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Christina Ishengoma amesema baada ya kamati hiyo kuzungumza na wananchi wa kijiji vya Msisiri kilichopo Wilayani Mpwapwa, Dodoma na kijiji cha Mnadani kilichopo upande wa Iringa wamebaini kuwepo kwa elimu ya uvuvi haramu kwa wananchi hao.

Dk Ishengoma amesema katika vijiji vyote walivyovitembelea wamebaini kuwepo kwa elimu hiyo kwa wananchi ambao pia wamekua wakishiriki katika kupambana na watu wanaofanya uvuvi haramu kwenye bwawa hilo.

" Niwaombe ndugu zetu mnaofanya shughuli zenu za uvuvi kisheria katika bwawa hili kuhakikisha mnakua walinzi katika kudhibiti uvuvi holela na haramu, kufanya hivyo siyo tu mnaisaidia serikali lakini pia mnajisaidia wenyewe kwani wanaovua kiholela wanawaharibia pia na nyie," Amesema Dk Ishengoma.

Dk Ishengoma pia amepokea changamoto ya wananchi wa kijiji cha Mnadani ambao wamelalamikia uwepo wa wingi wa Viboko kwenye bwawa hilo ambapo ameahidi kupeleka malalamiko yao kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Damas Ndumbaro.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi, Dk Rashid Tamatamah amesema Wizara imekua ikitoa elimu ya uvuvi kwa wananchi hao ambao sasa wameielewa elimu hiyo na wanashirikiana na Serikali katika kudhibiti uvuvi haramu na kuteketeza nyavu zisizofaa ambazo zimekua zikikamatwa.

Dk Tamatamah amewaahidi wananchi wa Miseseri kuwa Serikali itawaletea nyavu moja ya boti ifikapo Julai mwaka huu ambayo itawasaidia kwenye shughuli zao za uvuvi na kufanyia pia doria ya kudhibiti uvuvi haramu.

" Niwaahidi hapa mbele ya kamati yetu ya Bunge kuwa Wizara itatuma wataalamu wa utafiti kutoka TAFIRI kuja kuangalia na kutafiti kama upo uwezekano wa kuweka mbegu ya samaki ili kusaidia kuongeza wingi wa samaki kwenye bwawa hili.

Lakini pia Ndugu zangu wavuvi niwasihi na kuwakumbusha kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili viwasaidie katika kupata mikopo itakayokua msaada kwenu katika kujiimarisha kwenye shughuli zenu kwani mtapata fedha mtakazotumia kununua nyavu na zana nyingine za uvuvi," Amesema Dk Tamatamah.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christina Ishengoma akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mnadani Kata ya Izazi wilayani Iringa, Mkoani Iringa baada ya kamati hiyo kufanya ziara na kuzungumza na kuwasikiliza wananchi hao kuhusu maendeleo ya Bwawa la Mtera.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ambaye pia ni Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde akitoa mapendekezo yake kwa wananchi wa kijiji cha Msisiri kilichopo wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma mara baada kamati hiyo kutembelea kijiji hicho kuhusu Maendeleo ya Bwawa la Mtera.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akitoa ufafanuzi kwa wananchi wa kijiji cha Mnadani Kata ya Izazi wilayani Iringa Mkoani Iringa  wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji iliyosikiliza maoni na kero za wananchi kuhusu maendeleo ya Bwawa la Mtera.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Msisiri wakifatilia majibu na maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na viongozi wakati wa mkutano wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji walipofika kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho kilichopo Kata ya Chipogolo wilayani Mpwapwa  kuhusu za maendeleo ya Bwawa la Mtera.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...