Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande katikati akikagua jana sehemu ya machinjio ya nyama ya Shule ya Tanga katika Manispaa ya Songea alipofanya ziara ya kukagua machinjio hayo, wa kwanza kushoto Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema na kulia Mkuu wa idara ya Mifugo katika manispaa hiyo Rozina Chuwa.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande akiangalia mfereji unaotumika kusafirisha maji  machafu katika machinjio ya Shule ya Tanga katika Manispaa ya Songea akiwa katika ziara ya siku tatu mkoani Ruvuma,kulia kwake ni Mkuu wa idara ya mifuko Rozina Chuwa.
Naibu Waziri  Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande katikati akimsikiliza  mmoja wa vibarua anayefanya kazi katika machinjio ya nyama Shule ya Tanga katika Manispaa ya Songea ambaye hajalipwa stahiki zake za mishahara tangu machinjio hayo yalipoanza kufanya kazi Mwezi Mei hali iliyomfanya kuishi kwa shida kubwa ikiwemo kufukuzwa kwenye nyumba anayoishi kwa kushindwa kulipa kodi,wa pili kulia Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema na kulia Mkuu wa idara ya mifugo manispaa ya Songea Rozina Chuwa.
Picha na Muhidin Amri


Na Mwandishi Wetu, Songea
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na mazingira Hamad Chande, ametoa  siku tatu kuanzia jana(leo) kwa uongozi wa Manispaa ya Songea,kulipa madeni ya vibarua wanaofanya kazi katika machinjio ya kisasa ya Shule ya Tanga.

Naibu Waziri Chande, ametoa agizo hilo jana wakati alipotembelea machinjio hayo akiwa katika ziara yake ya siku tatu katika mkoa wa Ruvuma  kujionea utekelezaji wa utunzaji wa mazingira na uhifadhi  wa vyanzo vya maji katika mkoa wa Ruvuma.

Akiwa katika machinjio hayo Naibu Waziri alipata malalamiko  kutoka kwa baadhi ya  vibarua  wakilalamika kutolipwa stahiki zao tangu machinjio hayo yaliyopoanza kufanya kazi Mwezi Mei Mwaka huu.

Amesema, Serikali ya awamu ya sita haitaki kuona wala kusikia wananchi wake wanapata shida kutokana na  uzembe wa baadhi ya watumishi wake ambao wanashindwa kwa makusudi kutatua  kero za wananchi katika maeneo yao.

“kwa kuwa mkurugenzi  hapa hayupo basi nakuagiza mwakilishi wake hadi kufika tarehe 15 keshokutwa akikisheni mnalipa  madeni yote  mnayodaiwa,pia mkuu wa wilaya nakuomba fuatilia malipo ya hawa vijana,siyo ustaarabu hata kidogo  mtu  unampa kazi lakini wakati wa malipo unamzungusha hili siperndi lijitokeze tena. ”Amesema.

Aidha,ameagiza  kufanyiwa marekebisho kadhaa katika machinjio hayo ikiwemo mfumo wa maji taka na kuwapa vifaa vya  usalama  vijana wanaofanya kazi  katika machinjio baada ya kushuhudia wakifanya kazi mbalimbali kama kuondoa damu sakafuni  na kusafisha sehemu ya  kinyesi cha wanyama wanaochinjwa bila ya kuvaa vifaa kinga.

Hata hivyo,ameipongeza Manispaa hiyo kwa uamuzi wa kujenga machinjio hayo na kusisitiza yatumike kwa ajili ya wananchi kupata nyama safi.

Mwenyekiti wa umoja wachinja nyama katika machinjio hayo Ased Ali amesema, changamoto katika machinjio hayo ni uhaba wa vifaa vya kufanyia kazi kama vile visu,kofia ngumu,buti  na wafanyakazi wachache, hivyo ameiomba Manispaa kuwapatia vifaa na kuongeza idadi ya watumishi ili waweze kutekeleza majukumu yao.

Mmoja wa vibarua katika machinjio hayo Josephat Mwambiga, amelalamikia kutolipwa  stahiki zake tangu machinjio yalipofunguliwa

jambo linalowafanya waishi maisha magumu  ikiwemo kutakiwa kuhama kwenye nyumba walizopanga kutokana na kushindwa kulipa kodi.

Kwa upande wake Kaimu Mhandisi wa ujenzi wa Manispaa hiyo Caroline Bernald amesema, mradi wa machinjio ulianza kutekelezwa kwa awamu mbili,awamu ya kwanza ulianza mwezi Julai 2017 na kukamilika Machi 2019 na awamu  ya pili ulianza  Januari 2020 na kukamilika Mwezi Desemba 2020 kwa gharama ya sh.5,748,799,559.00.

Amesema, awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa machinjio imefanywa na Mkandarasi Girraf Investment Ltd kwa gharama ya sh.2,725,624,900.00 na kusimamiwa na Mhandisi  Mshauri S&F Consultancy kwa gharama ya sh.232,260,000.00 na hivyo kufanya gharama  ya mradi kwa kipindi hicho kuwa sh.2,957,884,900.00.

Amesema, awamu ya pili ya ujenzi umetekelezwa na Wakandarasi wawili ambao ni STUMAIK Engeneering Co Ltd ambaye alianza kazi mwezi Januari 2020 na kukamilisha  Mwezi Desemba kwa gharama ya sh.950,593,823.00 na mpaka mradi kukamilika  imetumika sh.717,312,580.00.

Kwa mujibu wa Mhandisi Caroline, katika kipindi hicho msimamizi wa mradi ni Mhandisi mshauri Bureau For Industry Cooperatin(BICO) kwa gharama ya sh.225,856,250.00 na ameshalipwa  sh.218,370,000.00.

Ametaja kazi zilizofanyika ni kuingiza umeme na kufunga Transfoma,kuchimba kisima kirefu cha maji mita 100,kuchimba mabwawa ya maji machafu,shimo la kutupa nyama isiofaa kwa matumizi ya binadamu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...