Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw Anthony Mtaka ametoa wito kwa benki ya Exim Tanzania kuangalia namna ya kuwawezesha wakandarasi wa ndani ya nchi ili waweze kutekeleza miradi mikubwa ndani na nje ya nchi.

Bw Mtaka alitoa wito huo mwishoni mwa wiki aliposhiriki kwenye hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Benki ya Exim kwa ajili ya wateja wake wa jijini Dodoma, ambapo alitolea mfano wa Benki ya Exim China ambayo imekuwa ikiwawezesha wakandarasi kutoka nchini humo kutekeleza miradi mikubwa nje ya nchi ikiwemo Tanzania.

“Nimefurahishwa na ufunguzi wa tawi jipya la Benki ya Exim hapa jijini Dodoma, hivyo basi pamoja na kuongeza mtandao na huduma kwa wateja wenu, nashauri ni vema zaidi pia muangalie namna ya kuwasaidia wakandarasi wetu wa ndani ili waweze kutekeleza miradi mikubwa ndani na nje ya nchi ikiwemo kwenye mataifa ambayo tayari benki ya Exim ina matawi yake ikiwemo Comoro, Djibouti, Uganda na Ethiopia.’’ Alisema.

Alisema kwa kuwa makampuni makubwa yanayotekeleza miradi yake hapa nchini yamekuwa yakiwezeshwa kifedha na mabenki katika mataifa yao ipo haja pia kwa benki hapa nchini kuiga mfano huo.

Zaidi Bw Mtaka alitoa ushauri kwa benki hiyo kuangalia namna ya kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wanaohitimu vyuo hapa nchini kwa kufadhili miradi inayotokana na mawazo yao kwa kuanzisha mfuko maalumu unaofanana na ule wa uwajibikaji kwa jamii (CSR).

“Badala ya kuwa na mpango wa Uwajibikaji kwa jamii peke yake (CSR) benki ya Exim mnaweza kuwa na mpango wa Uwekezaji kwa jamii (CSI), ambao pamoja na mambo mengine ulenge kusaidia wahitimu wa elimu ya juu wakiwa mmoja mmoja au vikundi ambapo mtawapatia mikopo ili waweze kutekeleza mawazo yao,’’ alisema.

Akuzungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa Bodi ya benki hiyo Bi Irene Mlola alisema benki hiyo imepokea mawazo ya Bwana Mtaka na kuahidi kuyafanyia kazi huku akisisitiza uwepo wa tawi la benki hiyo jijini Dodoma ni mwanzo wa kuwasaidia wakazi wa jiji hilo kukuza uchumi wao kwa kuwasogezea huduma za kifedha karibu zaidi katika kuhakikisha kwamba huduma hiyo inawafikia wananchi wote hususani waliopo pembezoni.

Alisema benki hiyo pia imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inashiriki kikamilifu kujenga uchumi wa nchi kwa kushirikiana na Serikali na zaidi sekta binafsi ili kufanikisha uchumi wa viwanda.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Huduma za Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya Exim, Bwana Andrew Lyimo pamoja na kuwashukuru wakazi wa jiji la Dodoma kwa kuipokea vema benki hiyo, aliahidi kuwa benki hiyo imejipanga kutoa huduma za kibenki zinazoendana na mahitaji yao sambamba na ubunifu unaotokana na uwekezaji kwenye huduma za kidigitali.

“Pamoja na uwekezaji kwenye huduma kidigitali, wakazi wa Dodoma wajipange kufurahia huduma zetu zinazoendana na mahitaji yao ikiwemo mikopo ya binafsi, ya kibiashara au hata ya umiliki wa nyumba  yenye riba nafuu kabisa. Tunawakaribisha sana Benki ya Exim,’’ alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw Anthony Mtaka akizungumza na viongozi na wateja wa benki ya Exim aliposhiriki kwenye hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wa jijini Dodoma mwishoni mwa wiki. Wanaomsikiliza ni pamoja na Mkuu wa Huduma ya Rejareja wa Benki ya Exim, Andrew Lyimo  (Katikati) na Mkurugenzi wa Bodi ya benki hiyo Bi Irene Mlola (wa pili Kulia).

Mkuu wa Huduma ya Rejareja wa Benki ya Exim, Andrew Lyimo akizungumza na wageni waalikwa wakiwemo viongozi wa serikali na wateja wa benki hiyo kwenye hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wa jijini Dodoma mwishoni mwa wiki. Wanaomsikiliza ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw Anthony Mtaka (Kulia).

Mkurugenzi wa Bodi ya benki ya Exim Bi Irene Mlola akizungumza kwenye hafla hiyo



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...