Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC)limeingia makubaliano ya kiutendaji na Shirika la Posta nchini (TPC) ili kupanua wigo wa kiuendaji, kuongeza ufanisi wa huduma zake sambamba na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibima hasa maeneo ya vijijini.
Uamuzi huo ulioungwa mkono na serikali kupitia Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Juma Malik Akili umetajwa kuwa utasaidia kuongeza mapato kwa mashirika hayo yote mawili huku wito kwa mashirika na taasisi mbalimbali za serikali zilizopo Tanzania bara na Zanzibar kuanzisha mahusiano ya kiutendaji ili kuongeza wigo wa utoaji huduma zao kwa pande zote mbili za nchi.
Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano hayo ya ushirikiano wa fursa za matumizi ya pamoja ya huduma na bidhaa za mashirika hayo mawili iliyofanyika mapema hii leo Zanzibar, Dk Akili alisema kupitia makubaliano ya namna hiyo wadau wanakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupunguza gharama za uendeshaji, kutanua wigo huduma na hivyo kuongeza kipato.
“Baada ya makubaliano haya tafsiri yake ni kwamba Shirika la Bima Zanzibar tayari linaweza kutoa huduma zake nchi nzima kupitia ofisi za Shirika Posta lenye ofisi zake maeneo yote bara na visiwani. Huu ni mkakati mzuri kibiashara naomba sana mashirika mengine yaige mfano huu,’’ alisisitiza.
Zaidi Dk. Akili alitoa wito kwa mashirika hayo mawili kuhakikisha yanakuwa na utaratibu wa kujifanyia tathmini kila mwaka ili kujua ufanisi wa muungano huo huku akisisitiza kuwa serikali itakuwa bega kwa bega na mashirika hayo kuhakikisha ushirikiano huo hauvunjiki na zaidi unakuwa chachu ya kuvutia mashirika mengine kuwa na mahusiano kama hayo ya kibiashara.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Ndg.Amour Hamil Bakari,.alimuhakikishia Dk Akili kuwa serikali tayari imejipanga kuhakikisha kwamba inalinda kwa nguvu zote uhusiano huo huku ikiendelea kuhamasisha taasisi na mashirika mengine kuiga mfano huo.
Awali wakizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa ZIC, Bw Arafat Haji na Kaimu Posta Master Mkuu Bw Macrice Mbodo waliyataja maeneo makuu matatu yanayohusishwa katika ushirikiano huo kuwa ni pamoja na Shirika la Posta kuwa wakala wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), Shirika la Bima Zanzibar kutumia huduma za Shirika la posta hususani katika utumaji wa Nyaraka, Vipeto, Barua na Vifurushi pamoja na kutazama na kutumia fursa zilizopo baina ya pande hizo mbili ikiwemo huduma ya rasilimali za majengo na ardhi.
“Kupitia ushirikiano huu, zipo huduma za Shirika la Bima La Zanzibar zitakazotumiwa na Shirika la Posta ikiwemo Huduma ya Bima kwa mali za Shirika la Posta zikiwemo vyombo vya moto na majengo. Tafsiri ya hiki tulichokifanya hapa ni kwamba kwamba popote lilipo Shirika la Posta ifahamike pia kuwa hapo pia sisi Shirika la Bima Zanzibar tupo.’’ Alisema Bw Arafat .
Aliongeza kuwa kuwa uamuzi huo utapunguza gharama za uendeshaji, kuongeza kipato sambamba na kuongeza huduma kwa wateja ambao hapo awali walikuwa hawafikiwi na Shirika hilo.
Kwa upande wake Bw Mbodo alisisitiza kuwa ushirikiano huo utakuwa na tija zaidi kwa pande zote hususani kipindi ambacho Shirika la Posta lenye matawi yake zaidi 350 nchi nzima pia limewekeza zaidi katika huduma za kidigitali.
“Tunaamini pia kupitia duka letu la mtandaoni (Online Shop) tunaweza kuuza na kutangaza huduma za ZIC kila pande ya nchi na kote ulimwenguni.Tunaamini ushirikiano huu utaendelea kuvutia wadau wengine ili waje kushirikiana na sisi sababu Shirika la Posta tupo kwa ajili ya kumuhudumia kila mtu.’’ Alisema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ZIC, Balozi Juma Abdallah Ali alisema mbali na faida za kiufanisi na kiuchumi, ushirikiano huo utaisaidia kuborisha uhusiano uliopo baina ya pande mbili za Tanzania bara na Zanzibar kwa kuwa huduma wananchi wa pande zote mbili wamefikiwa na huduma za mashirika hayo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC)Bw Arafat Haji (kushoto) na Kaimu Posta Master Mkuu wa Shirika la Posta nchini (TPC) Bw Macrice Mbodo (Kulia) wakisaini hati ya makubaliano ya kiutendaji baina ya mashirika hayo mawili wakati wa hafla fupi iliyofanyika Zanzibar leo.Wanaoshuhudia ni pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Juma Malik Akili (Kushoto waliosimama nyuma) Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Ndg.Amour Hamil Bakari (Kulia waliosimama nyuma) na Mwenyekiti wa Bodi ya ZIC, Balozi Juma Abdallah Ali (Katikati)
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC)Bw Arafat Haji (katikati) na Kaimu Posta Master Mkuu wa Shirika la Posta nchini (TPC) Bw Macrice Mbodo (Kulia) wakiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) hati ya makubaliano ya kiutendaji baina ya mashirika hayo mawili baada ya kusaini wakati wa hafla fupi iliyofanyika Zanzibar leo. Wanaoshuhudia ni pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Juma Malik Akili (Kushoto waliosimama nyuma) Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Ndg.Amour Hamil Bakari (Kulia waliosimama nyuma) na Mwenyekiti wa Bodi ya ZIC, Balozi Juma Abdallah Ali (Katikati). Kushoto ni Katibu Shirika la ZIC Bi Safia Hija Abrass.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Juma Malik Akili akizungumza kwenye hafla hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Ndg.Amour Hamil Bakari akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC)Bw Arafat Haji akizungumza kwenye hafla hiyo.
Kaimu Posta Master Mkuu wa Shirika la Posta nchini (TPC) Bw Macrice Mbodo akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC)Bw Arafat Haji (kushoto) akikabidhi zawadi ya mlango wa Zanzibar kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Juma Malik Akili wakati wa hafla hiyo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Juma Malik Akili (kushoto) akimkabidhi zawadi Kaimu Posta Master Mkuu wa Shirika la Posta nchini (TPC) Bw Macrice Mbodo wakati wa hafla hiyo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Juma Malik Akili (Katikati), Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Ndg.Amour Hamil Bakari (wa pili kushoto walioketi) wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na wafanyakazi wa Shirika la Bima Zanzibar na Shirika la Posta.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...