MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema Agosti 11, 2021 itatoa uamuzi kama Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) Dickson Maimu na wenzake wanne wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wana kesi ya kujibu au la.

Hatua hiyo imefikwa kufuatia upande wa mashtaka katika kesi hiyo uliokuwa ukiongozwa na  wakili wa serikali Mwandamizi Ladslaus Komanya, kufunga ushahidi baada ya jumla ya mashahidi 26 kutoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa na kuwasilisha vielelezo 45.

Uamuzi huo utatolewa mahakamani hapo na  Hakimu Mkazi Mwandamizi Rashid Chaungu anayesikiliza kesi hiyo

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Sheria wa mamlaka hiyo, Sabina Raymond, Meneja wa Biashara, Xavery Kayombo, Aveln Momburi na George Ntalima.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka mbalimbali ikiwemo kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 1.175.

Kabla ya kufunga ushahidi, shahidi wa mwisho, Emmanuel Koroso,  Ofisa wa Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), amedai  Mahakamani hapo kuwa Mkurugenzi wa Sheria wa Mamlaka hiyo, Sabina Raymond alishuhudia utiwaji saini mkataba ulioiingizia serikali hasara ya Dola za Marekani 551,500.

Amedai wakati akifanya Mahojiano na Sabina alimweleza kuwa yeye ndiye alikuwa msimamizi wa masuala yote yanayohusu Sheria NIDA ikiwemo kusimamia na kushuhudia utiwaji saini wa mikataba mbalimbali.

Ameeleza kuwa, Mkataba wa Dola 551,500 ulikuwa kati ya NIDA na Kampuni ya Ms Law Partner in association of School of Law Tanzania of University of Dar es Salaam kwa ajili ya Mapito ya sheria katika utekelezaji wa mradi huo na kulipwa kiasi hicho cha fedha na NIDA.

Amedai fedha hizo hazikupaswa kulipwa na NIDA  bali  Kampuni ya Gotham International Ltd ambayo iliingia mkataba wa Dola milioni 9 na NIDA kwa ajili ya kazi ya vitambulisho.

Kazi hizo ni pamoja na kutoa ushauri elekezi katika utekelezaji wa mradi wa NIDA.

Alidai pia mshitakiwa huyo alimueleza kwamba katika mkataba huo, Gotham ilikubaliana na NIDA kuwa inaweza kufanya kazi hiyo yenyewe ama kutafuta mtu  au Kampuni kwa malipo hayo.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...