Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi akizungumza kwenye uzinduzi wa kikundi cha pili kupata mafunzo ya watendaji wakuu (CEO Apprenticeship Programme - CAP). Mafunzo haya yameandaliwa na jukwaa la watendaji wakuu wa Tanzania CEO Roundtable (CEOrt) na Chuo Kikuu cha Strathmore (SBS), kwa lengo la kujenga uzoefu wa kuongoza mashirika, kuandaa viongozi bora wa siku zijazo, na kujadili changamoto mbalimbali zinazokabili Taifa.

Serikali imesema iwapo kutakuwa na maafisa watendaji wakuu wa taasisi mbalimbali nchini ambao ni wazawa nchi itanufaika kiuchumi na kuongeza fursa za ajira kwa watu.

Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Utumishi Deogratius Ndejembi wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mafunzo ya uongozi wa miezi 12 mahsusi kwa Watanzania wenye ujuzi na uzoefu ndani ya sekta za umma na binafsi ili kuwaandaa kuwa watendaji wakuu wa siku zijazo.


Alisema mafunzo kama haya ya kikundi cha pili ya CEO Apprenticeship Programme (CAP) yanawajenga watanzania kuwa viongozi wa siku zijazo pamoja na kuwa na weledi ambao utakuza biashara na taasisi zao.

 Bodi ya Wakurugenzi Watendaji wa Tanzania CEO Roundtable (CEOrt) kwa kushirikiana na Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Strathmore (SBS) inazindua rasmi mafunzo ya kikundi cha pili cha CEO Apprenticeship Programme (CAP) leo. 

CAP ni Mpango wa mafunzo ya uongozi wa miezi 12 iliyoundwa mahsusi kwa Watanzania wenye ujuzi na uzoefu ndani ya sekta za umma na sekta binafsi, ili kupitia mafunzo haya, ufundishaji na ushauri, kuwaandaa kuwa watendaji wakuu wa siku zijazo. Lengo kuu la mpango wa CAP ni kuwezesha kuwaandaa viongozi wenye uwezo wa juu na maono nchini Tanzania. 

Kupitia kikundi cha kwanza, mafunzo ya CEO Apprenticeship Programme yameonyesha mafanikio mengi. Hadi sasa, wahitimu watatu wa kikundi hicho wamepandishwa daraja na kushika nyadhifa za uongozi kwenye mashirika yao, na wengine wawili wamepanda vyeo pia. Vilevile, miradi kadhaa iliyotokana na mpango wa CAP na inayolenga maswala ya kijamii na kiuchumi inaendelea kustawi, ikiwemo jukwaa la Fanisi Program linalosaidia kukuza maendeleo binafsi na ya kikazi, na Ajira Kiwandani, tovuti inayounganisha waajiri na Watanzania wenye ujuzi wa sekta ya viwanda. 

Katika hafla ya uzinduzi asubuhi ya leo, CEOrt wanafurahi kuwakaribisha wageni wakiwemo Bi. Ruth Zaipuna, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Dkt. George Njenga, Mkuu wa Chuo cha SBS pamoja na mhitimu wa kikundi cha kwanza cha CAP, Bw. Unguu Sulay, Mkurugenzi Mtendaji wa Coca-Cola Kwanza. Wageni hawa watazungumza na kutoa maoni yao juu ya uongozi kwa ujumla na matokeo ya mafunzo ya CAP mpaka sasa. 

Mara tu baada ya uzinduzi, ratiba ya mafunzo kwa kikundi cha pili cha CAP inaanza rasmi. Kwa muda wa miezi 12, washiriki wa CAP watapata fursa ya kuzungumza na washauri, kujenga uzoefu wa kuongoza mashirika, na kujadili suluhisho za changamoto mbalimbali zinazokaibili taifa. 

CEOrt inachukua nafasi hii kushukuru viongozi wa Serikali, Sekta Binafsi na Washirika wa Maendeleo ambao wameunga mkono mpango huu muhimu wa kuboresha nguvukazi ya taifa tangu kuanzishwa. Vilevile, shukrani za dhati ziwaendee wadhamini wa Kikundi cha Pili cha CAP kwa kutambua umuhimu wa kujenga Watanzania watakaokuwa viongozi bora na kuwasaidia walengwa kushiriki kwenye mafunzo haya - Songas Limited, National Bank of Commerce (NBC), Kenya Commercial Bank (KCB), Kioo Limited, Primefuels Tanzania, Multichoice Tanzania, Reni International, CRDB Bank, Chemi Cotex, Stanbic Bank, NMB Bank, Spedag Interfreight, Empower Limited, na Management & Development Health. Uzinduzi huu ni hatua nyingine muhimu katika kukuza talanta za Tanzania.Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...