Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kwa gharama ya shilingi takribani bilioni 165.

Ujenzi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa kampuni tatu kutoka China ambazo ni Sinohydro Coorporation limited, M/s Beijing Sino-Aero Construction Engineering Co. limited pamoja na M/s China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation Co. Ltd ambapo unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 36 kutoka sasa.

Akishuhudia utiaji saini huo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amewataka wakandarasi hao kutekeleza mradi huo kwa viwango vilivyokubaliwa kimkataba na kwa kuzingatia muda ili kuwezesha malengo ya Serikali ya kuifanya Dodoma kuwa Mji Mkuu wa Serikali kufikiwa.

“Serikali tumejipanga kuhakikisha malipo kwa mkandarasi yanalipwa kwa wakati, hivyo hakikisheni Mkandarasi anatekeleza majukumu yake yote kwa mujibu wa mkataba, hatutakubali visingizio vyovyote”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka, ameishukuru Serikali kwa kufikia hatua hiyo na kuahidi kutoa ushirikiano kwa wakandarasi pale unavyohitajika.

Aidha, amewataka wananchi wa Dodoma kutumia fursa ya ujenzi wa kiwanja cha ndege huo kupata ajira na kusisitiza kufanya kazi kwa uaminifu na bidii kwa watakaofanikiwa kupata ajira katika mradi huo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Malongo, amesema Wizara imejipanga kukamilisha taratibu za kiutendaji zilizobaki kwa wakati na kuwataka wote wanaohusika na mradi huo kuanza kazi mara moja.

“Mkataba umekamilika tunawataka wakandarasi na wasimamizi waende site mara moja, wizara tuko tayari kwa kazi,’ amesema Katibu Mkuu Mhandisi Malongo.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Babaraba Nchini (TANROADS) Mhandisi Rogatus Mativila, amesema ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Msalato utahusisha awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itakuwa ni ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege na ujenzi wa majengo ikiwemo jengo la abiria.

Kiwanja hicho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka pindi kitakapokamilika. 
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa (katikati) akishuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kati ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila (kushoto), na Muwakilishi wa Kampuni ya Sinohydro Coorporation ya China, Bw. Shi Yong (kulia), jijini Dodoma.


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila na Muwakilishi wa Kampuni ya Sinohydro Coorporation ya China, Bw. Shi Yong, wakionesha mkataba wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato Dodoma, mara baada ya kuusaini, jijini Dodoma.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Malongo, akisisitiza jambo kabla ya zoezi la utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato uliofanyika jijini Dodoma.


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara hiyo mara baada ya kushuhudia zoezi la utiaji saini wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, jijini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...