Pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali katika kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji nchini,mbunge wa jimbo la Madaba mkoani Ruvuma Joseph Mhagama ameiomba serikali kutoa ufafanuzi ni lini wafugaji waliopo kwenye eneo la ekari 1800 zilizotolewa kwa wakulima wa kijiji cha Ngadinda halmashauri ya Madaba watahamishwa ili kuepusha migogoro inayowakabili wananchi wa kijiji hicho.
Akihoji swali la nyongeza kwa naibu waziri wa mifugo na uvuvi Abdallah Ulega bungeni wiki iliyopita Mhagama ameitaka serikali kutoa ufafanuzi ni lini itasaidia kuwaondosha wafugaji ili kuepusha migogoro inayoendelea katika kijiji hicho.
“Pamoja na majibu mazuri ya serikali,wafugaji ambao wameambiwa wahame kwenye eneo la hekta 1800 ambazo zilitolewa na serikali kwa wakulima hawajahama ni nini kauli ya serikali kuhusu kuwaondoa hawa wafugaji ambao wamekaa kwenye eneo ambalo lilitolewa kwa ajili ya kilimo ni lini wafugaji hawa wataondoka?”alihoji Mhagama
Aidha katika swali lake la pili mhagama amehoji ni lini serikali itachukua hatua za makusudi za kuwawezesha wafugaji nchini ili waweze kuwa na ufugaji wa kisasa ili kuondoa migogoro ya wafugaji na wakulima.
Akitoa majibu kwa maswali hayo ya nyongeza,Naibu waziri wa mifugo na uvuvi Abdallah Ulega amesema ni kweli serikali iligawa eneo hilo na kupiga marufuku kwa wafugaji kuwaingilia wakulima katika eneo hilo.
“Shamba la serikali la Ngadinda lililopo pale Songea lilikuwa na ekari 6000 na miaka michache nyuma tuliligawa,1800 tukawapa wanakijiji na 4000 tukabaki nazo serikali na kugawa vitalu.Kwa kuwa tayari 1800 tulishazigawa kwa wanakijiji kwa ajili ya shughuli zingine ikiwemo kilimo sasa ni marufuku kwa wale ambao hawakupewa eneo hilo kufanya shughuli zingine za kuwaingilia wale wanaokwenda kufanya shughuli za kilimo na hili naielekeza halmashauri kulisimamia”alisema Ulega
Ulega amesema mkakati katika kuwawezesha wafugaji,serikali inaendelea na mkakati wa kugawa vitalu na kuviboresha ili kuwapa fursa wafugaji nao kuwa na maeneo yao yasiyoingiliana na wakulima hatua itakayosaidia kupunguza changamoto hizo za migogoro.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...