Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika Kata Nne za Tanzania bara utakaofanyika tarehe 9 Oktoba mwaka 2021.
Akitangaza uchaguzi huo Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Wilson Mahera Charles amesema Tume imepokea barua kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa akiitaarifu juu ya kuwepo kwa nafasi wazi za Madiwani kwenye kata nne (4) za Tanzania Bara.
Alisema nafasi hizo zilitokana na kufariki kwa Madiwani wa
Kata 3 na mmoja kujiuzulu, hivyo kwa kuzingatia masharti ya Kifungu cha
13 (2) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, Tume
imeandaa Uchaguzi Mdogo ili kujaza nafasi za Udiwani kwenye Kata nne (4)
za Tanzania Bara.
Amezitaja kata hizo kuwa ni Kata ya Buyuni
iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam mkoa wa Dar es Salaam, Kata
ya Dongo Halmshauri ya Wilaya ya Kiteto Mkoa wa Manyara, Kata ya Lighwa
iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida na Kata ya
Ndembezi Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Mkoa wa Shinyanga.
Dkt. Mahera alifafanua kuwa Uchaguzi huo Mdogo wa Udiwani katika Kata nne (4) utafanyika sambamba na Uchaguzi Mdogo wa Ubunge wa Majimbo mawili (2) ya Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba – Zanzibar na Ushetu, Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Mkoa wa Shinyanga Tanzania Bara pamoja na Kata sita (6) za Tanzania Bara.
“Kata hizo ni Lyowa –
Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Mkoani Rukwa, Kileo - Halmashauri ya
Wilaya ya Mwanga, Mkoani Kilimanjaro, Vumilia - Halmashauri ya Wilaya ya
Urambo, Mkoani Tabora, Neruma - Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Mkoani
Mara”alisema Dkt. Mahera na kuongeza kuwa:
Kata ya Luduga -
Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoani Njombe, na Kagera-Nkanda -
Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Mkoani Kigoma.
Dkt. Mahera alisema ratiba ya Uchaguzi Mdogo wa Kata nne (4) Tanzania Bara itaenda sambamba na Ratiba ya Uchaguzi Mdogo wa wa Majimbo mawili (2) ya Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba – Zanzibar na Ushetu, Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Mkoa wa Shinyanga Tanzania Bara na Kata sita (6) za Tanzania Bara.
Alisema wagombea watahukua fomu za uteuzi kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 19 Septemba, 2021, Uteuzi wa wagombea utafanyikatarehe 19 Septemba, 2021, Kampeni za Uchaguzi zitaanza tarehe 20 Septemba hadi tarehe 08 Oktoba 2021 na Siku ya kupiga kura ni 09 Oktoba 2021.
Dkt. Mahera amevikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo yatayotolewa na Tume katika kipindi cha uchaguzi huo mdogo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...