Na Mwandishi Wetu

OFISA Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Asasi zinazotoa Huduma ndogo za Kifedha (TAMFI), Winnie Terry amezitaka taasisi za fedha zinazohudumia wajasiriamali wadogo kuanzisha bidhaa mpya zitakazohusiana na nishati mbadala.

Kauli hiyo aliitoa mwishoni mwa wiki akizungumzia haja ya wajasiriamali wadogo kutumia nishati mbadala kupunguza changamoto ya nishati ambayo inawakumba hasa maeneo ya pembezoni.

Alisema wajasiriamali wa Tanzania wana nafasi kubwa ya kutumia nishati mbadala hasa nishati ya jua, lakini wanahitaji kuwekewa mazingira ya uwezeshaji wa nishati hiyo hasa watumiaji.

Alisema wajasirimali hao wanahitaji kupata uwezo huo kukabiliana na changamoto za nishati ya umeme hasa maeneo ambayo hayajafikiwa gridi ya taifa na yale ambayo upatikanaji wake wa umeme ni duni.

Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji huyo nishati mbadala huchangia kuhifadhi mazingira na pia silaha ya kukabili umaskini, ni bidhaa ambayo ina faida kubwa ikiwekezwa.

Alisema TAMFI inataka taasisi ndogo za fedha kuandaa bidhaa hizo katika mifumo yao ya uwezeshaji kifedha wajasiriamali wadogo ili waweze kukopa bidhaa za nishati mbadala kuharakisha maendeleo ya uchumi wa nchi na kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa katika ustawi wa jamii.

Katika semina kadhaa zilizoendeshwa na TAMFI ilibainika uwapo wa haja kubwa ya nishati mbadala hasa ya jua katika kufanikisha uzalishaji wa bidhaa zenye viwango katika mfumo wa mnyororo wa thamani, kutokana na kukosekana kwa umeme wa uhakika katika maeneo ya pembezoni.

Alisema pamoja na kuwapo kwa nishati mbadala kukosekana kwa uwezeshaji hasa kwa watumiaji wa mwisho kumefanya nishati hiyo kushindwa kutumika kikamilifu katika kuongeza tija miongoni mwa wajasirimali wadogo wakiwemo wasindikaji wa bidhaa mbalimbali.

Kutokana na haja hiyo TAMFI ikishirikiana na Mfuko wa Charles Stewart Mott na SELCO Foundation wanaendesha kampeni kubwa ya kuhakikisha kunakuwepo matumizi ya nishati mbadala yenye tija kwa taasisi za fedha na wadau kuhakikisha wanakuwa na bidhaa zinazohusika na nishati hiyo katika biashara zao.

Mratibu wa semina zinazohusu nishati na nishati mbadala wa taasisi hiyo, Michael Onesimo alisema nishati mbadala yenye tija hasa matumizi ya nishati ya jua huleta faida kubwa kama yakitumika katika masuala ya ukulima,ufugaji na uvuvi .

"Ni muhimu kufanya utafiti wa soko, kulielewa soko vizuri na kuchangia kuunda mazingira wezeshi kwa haya yote kutokea; wanahisa wakiongeza uwekezaji kutakuwa na matokeo chanya," alibainisha Onesmo ambaye pia ni mtaalamu wa huduma za maendeleo ya biashara na utafiti wa soko.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...