Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imejiwekea nafasi nzuri ya kufuzu Michuano ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, baada ya ushindi wa bao 3-2 dhidi ya wageni Madagascar katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa Dar es Salaam.
Taifa Stars ikiwa chini ya Nahodha wake, Mbwana Samatta ilipata ushindi huo kwa mabao ya Beki wake, Erasto Edward Nyoni dakika ya 2, Novatus Dismas dakika ya 26 na Feisal Salum dakika ya 52 ya mchezo huo.
Mabao ya Madagascar yamefungwa na Wachezaji, N. Rakotoharimalala dakika ya 36 na T. Fontaine dakika ya 45+2 ya mchezo huo.
Kwa matokeo hayo, Taifa Stars itakuwa nafasi ya kwanza katika Kundi J linaloundwa na timu za DR Congo, Benin na Madagascar ikiwa na alama 4 sambamba na Benin ikiwa tofauti ya magoli ya kufunga. Alama tatu hizo zitasaidia Tanzania kufuzu hatua nyingine ya 10 Bora (Play Off) ili kufuzu Michuano hiyo mikubwa duniani (FIFA World Cup 2022).
Taifa Stars itasubiri michezo mingine dhidi ya Benin (nyumbani na ugenini), DR Congo (nyumbani, Benjamin Mkapa) na mchezo dhidi ya Madagascar (ugenini) ili kupata uongozi wa Kundi hilo la J.
Makundi yote 10, kila Kundi likiwa na timu 4 litatoa timu moja pekee ambayo itaunda timu 10 pekee ambazo zitacheza kutafuta timu 5 zitakazofuzu kucheza Michuano ya Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...