Na: Albert G. Msando

Mosi, ni kweli kwamba nimekopeshwa na Benki ya Equity jumla ya sh Milioni Mia Moja na Sita (Tsh 106,000,000). Fedha hizo nimeamua kutumia kuwasaidia wamachinga takribani 788 kujenga mabanda ya biashara.

Ieleweke kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro haijakopa, sijakopa kwa niaba yake na sijaidai fedha hizo mpaka sasa.

Kilichofanyika ni uamuzi wangu binafsi kama kiongozi kutafuta njia ambayo,

1. Tunatatua suala la wamachinga ambalo nimelikuta baada ya kuteuliwa.

2. Kuongeza mapato ya Halmashauri.

3. Kuonyesha kwamba tukiamua kupanga vizuri maeneo yetu tunaweza kupata sehemu rafiki kwa machinga kufanya biashara.

4. Tukiwa na vipaumbele sahihi kuhusu matumizi yetu ya fedha tutatatua kero za msingi za wananchi kwa haraka zaidi.

Kitendo cha kukopa kwa ajili ya wamachinga sio kiki wala sijakiuka utaratibu wa kiserikali kuhusu matumizi ya fedha. Nimeanza na wamachinga Manispaa ya Morogoro tangu siku ya kwanza nimeingia ofisini.

Pili, kwa sasa tumeweza kujenga sehemu 788 kwa fedha hizo na tunaendelea na awamu ya pili ya sehemu 351 za wamachinga ambazo wataingia kwa hiari yao wenyewe. Jumla Soko Kuu Kingalu litakuwa na wamachinga takribani Mia Tisa.

Kwa nini nimefanya hivyo? Baada ya kuapishwa tayari Halmashauri ilishapitisha bajeti yake ya 2021/2022 na haijawahi kutenga fedha kwa ajili ya wamachinga kuhama barabarani. Hakukuwa na mpango huo kwenye bajeti.

Njia rahisi ingekuwa kuwatoa kwa nguvu na kuwalazimisha kwenda sehemu ambazo ziko wazi bila miundombinu. Sehemu hizo wangeenda sio kwa sababu wanataka au zinafaa ila kwa sababu ni rahisi (cheap) kwa upande wa Halmashauri.

Au, ingebidi kusubiri vikao vya kupitia upya Bajeti ya 2021/2022 na Bajeti ya 2022/2023 kupata fedha kwa ajili ya kuwapanga wamachinga. Tatizo lingebaki kwa muda wote huo huku wao wakiongezeka kila kukicha na hakuna mapato tunapata kama Halmashauri.

Tatu, wamachinga hali zao ni duni kujenga wenyewe vibanda vizuri au kukopa fedha benki. Tuliwaza kufanya hivyo na Equity Bank wako tayari kutoa fedha hizo. Lakini tukawaza pamoja na wamachinga kwamba wakikopa wao wataanza biashara na deni la tsh 230,000.

Hii ingeweza kuwapa changamoto wakishindwa kurejesha mmoja mmoja. Mbeleni wangenyang’anywa vibanda hivyo au mitaji isingekua. Nikaamua kukopa mimi kwa kutumia mshahara wangu.

Sasa hivi Equity Bank wako tayari kuwakopesha fedha hizo kama mitaji badala ya gharama za ujenzi kwa sababu wana sehemu rasmi ya biashara.

Nne, tunaweza kufanya nini?

1. Baada ya mabanda kukamilika endapo kwa pamoja sasa kama wamachinga tukiamua kila mmachinga akilipa sh 1,000 tu kwa siku kama ushuru ni sh 23,640,000 kwa mwezi (tukimfanyia 500 itakuwa tsh 11,820,000 kwa mwezi). (Huu ni mfano SIO bei au maelekezo kuhusu bei).

Gharama za ujenzi zinaweza kurudi ndani ya miezi 5.5 au miezi 9!!. Na tatizo likawa limeisha ndani ya siku 60 tu.

AU

2. Halmashauri ikawakopesha wamachinga hao hao kwani ni wajasiriamali walio kwenye sekta isiyo rasmi kupitia fedha za vikundi (wanawake, vijana na walemavu). Fedha hizi zikarudishwa kama rejesho na kutumika kwa makundi mengine!!

Kiasi cha sh 1,000 au 500 kwa mazingira ya soko na biashara itakavyofanyika kinalipika kwa mmachinga.

Tano, kama viongozi ni lazima TUJITOE. Tuwaguse wananchi kupitia utatuzi wa kero za kwa njia yoyote halali. Hayati Nyerere, Nkurumah, Karume nk walijitoa katika maisha yao kuwanyanyua wananchi wao. Sisi tunafanya nini ndio swali la kila mmoja wetu.

Binafsi, sina uhuru ninaoupigania kutoka kwa mkoloni, sina ukombozi ninaotafuta kwa ajili ya wananchi, sina fedha za kujenga SGR nk kwa hiyo nimetumia nyenzo (mkopo) niliyonayo kutokana na nafasi yangu kujitoa kwa kadri ninavyoweza.

Nimeona wengi wanahoji inawezekana vipi kwani nitakuwa sina hela nimebakiwa nayo. Jibu ni kwamba kabla ya kuteuliwa nilikuwa na kipato ambacho hakijabadilika sana baada ya uteuzi. Naweza kuishi nacho.

Sasa hivi nimepewa na Serikali dereva, nyumba, mafuta na posho (ya hapa na pale) ili niwatumikie wananchi. Na heshima pia. Vinatosha ukiwa na nia ya dhati kuwatumikia wananchi.

Albert G. Msando,
Mkuu wa Wilaya Morogoro.
18/09/2021.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...