Na Joseph Lyimo


HALI ya sintofahamu na mtafaruku umezuka kwenye shule ya msingi Endiamtu Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara na wanafunzi kukimbia shuleni hapo, mara baada ya gari la kubeba wagonjwa kufika wakihofia kupata chanjo ya UVIKO-19.

Wazazi na walezi zaidi ya 30 wenye watoto kwenye shule hiyo walifika mara moja shuleni hapo baada ya kusikia kuwa chanjo ya UVIKO-19 inatolewa kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Hata hivyo, akizungumza na wazazi hao waliofika shuleni hapo mwalimu mkuu wa shule hiyo, Evetha Kyara amesema habari hizo siyo za kweli.

Mwalimu Kyara amesema madaktari wa kituo cha afya Mirerani walifika kutoa elimu ya kujikinga na corona na homa ya ini na siyo kutoa chanjo ya corona kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Amesema madaktari hao walifika shuleni hapo kutoa elimu ya corona na kwa walimu wa shule hiyo kwani kila mwaka huwa wanatoa elimu ya afya na walitoa siku hiyo kisha wakaondoka.

“Wanafunzi walipoliona gari na madaktari wamevaa mavazi meupe ndipo baadhi yao wakaingiwa na hofu na kukimbia kwenda majumbani mwao wakidhani wanapata chanjo ya UVIKO-19,” amesema Mwalimu Kyara.

Amesema wanafunzi wa darasa la awali, la kwanza na la pili ndiyo waliopatwa na hofu zaidi na kukimbia huku wakipiga kelele na kusababisha mtafaruku shuleni hapo.

Amewahakikishia wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule hiyo yenye wanafunzi 894 kuwa chanjo ya UVIKO-19 haitolewi shuleni hapo ila inatolewa kwenye kituo cha afya Mirerani.

"Wataalamu wa afya wanaelezea kuwa chanjo ya UVIKO-19 haitolewi kwa watu walio chini ya miaka 18 hivyo watoto hawawezi kuchanjwa ni watu wazima pekee," amesema.

Mmoja kati ya wazazi wa shule hiyo Baltazari Massawe amesema alipata taarifa kuwa shuleni hapo kuna mtafaruku kutokana na chanjo hiyo, hivyo akafika mara moja shuleni hapo.

“Nina mwanafunzi wa darasa la tano anaitwa Nancy Massawe hivyo nikafika mara moja shuleni lakini kumbe ni habari potofu zilikuwa zinasambazwa na hakukuwa na chanjo ya UVIKO-19 ikitolewa,” amesema Massawe.

Mmoja kati ya wanafunzi wa shule hiyo, Nancy Massawe ambaye anasoma darasa la tano amesema walihofia baada ya kuona gari hilo limefika shuleni wakadhani limefika kutoa chanjo hiyo.

"Baadhi ya wanafunzi walikuwa wanasemaje wazazi wao waliwaambia wakiona gari la kituo cha afya wakimbie na ndiyo walivyofanya watoto wakakimbia," amesema.

Mkazi wa kata ya Endiamtu, Ally Mohamed amesema bado elimu ya kutosha haijatolewa kwa wazazi kwani haiwezekani chanjo ya UVIKO-19 itolewe kwenye shule ya msingi.

"Serikali imetangaza kuwa chanjo inatolewa kwenye hospitali, kituo cha afya na zahanati kwa watu wazima na siyo kwenye shule ya msingi au sekondari," amesema.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...