Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Bw. Hery Mkunda akieleza jambo wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi PURA.
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Bw. Hery Mkunda na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Sara Rwezaula wameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa kushirikisha watumishi wa Taasisi hiyo katika kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu. Viongozi hao wametoa pongezi hizo katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi PURA kilichofanyika tarehe 15 na 16 Oktoba, 2021 mkoani Morogoro kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/21 na utekelezaji wa majukumu kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/22.
Akitoa maoni katika kikao hicho, Bw. Hery ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi PURA ameeleza kuwa kushirikisha watumishi wa Taasisi katika kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ni jambo la msingi sana na litasaida kuongeza ufanisi katika utendaji kazi. “Niipongeze PURA kwa kuandaa kikao hiki muhimu na nimatumaini yangu kuwa watumishi watajadili kwa kina na kufanya tathmini ya mwenendo wa utendaji kazi wa Taasisi, kufahamu maeneo ambayo Taasisi imefanya vizuri, maeneo yanayohitaji kutiliwa mkazo na kutoa ushauri wa nini kifanyike kuongeza ufanisi zaidi”, alieleza Bw. Hery.
Kwa upande wake Bi. Sara alieleza kuwa PURA imefanya jambo la kupigiwa mfano kwa kuwa sio Taasisi nyingi zenye utaratibu wa kuhusisha watumishi kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu waliyojipangia katika mwaka wa fedha husika. Aidha, Bi. Sara ameipongeza PURA kwa kutoa fursa kwa watumishi kupitia wawakilishi wao ambao ni wajumbe wa Baraza kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu waliyojipangia
Baraza la Wafanyakazi PURA linaundwa na wajumbe 34 waliopatikana kwa mujibu wa miongozo ya uundaji wa mabaraza ya wafanyakazi. Kati ya wajumbe hao, wapo wajumbe wanaoingia kwa nyadhifa zao (Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi, Wakuu wa Idara na Vitengo, na Wajumbe wa Halmashauri ya Tawi la TUGHE); wajumbe wa kuchaguliwa kutoka Idara/Kitengo vya Taasisi; Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...