Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
Katika maadhimisho ya Kitaifa ya mtoto wa kike duniani, Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA) wametoa elimu Kuhusiana na masuala ya VVU na UKIMWI pamoja na ugawaji wa Taulo za kike(Pads) kwa wanafunzi zaidi ya 500 wa Shule ya Sekondari Zimbwini iliyopo wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.
Akizungumza katika siku hiyo, Diwani Viti Maalum, Wilaya ya Kibiti, Bi. Zaharia Ally Mninguya ametoa wito kwa jamii kutoa kipaumbele kwa Watoto bila kujali jinsia sambamba na jamii kuchukua jukumu la kuwalinda Watoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao kama ilivyo binadamu yeyote.
“Waendesha Bodaboda na jamii kwa ujumla msiwalaghai Watoto wa shule ili waweze kutimiza ndoto zao na kutengeneza nguvu kazi katika Taifa letu”, ameeleza Bi. Zaharia.
Meneja wa NACOPHA, Kanda ya Dar es salaam, Victoria Humburya amesema NACOPHA kwa kuwezeshwa na Shirika la UNAIDS wameweza kutoa Boksi 20 za Pedi kwa wanafunzi wa kike wa Shule hiyo zaidi ya 500 ili kuwawezesha Watoto wa Kike kutimiza ndoto zao, kuwawezesha kuhudhuria katika masomo.
Huburya amesema, “Watoto wengi wa Kike wanashindwa kufika mashuleni na kubudhuria masomo yao kutokana na kutokuwa na uwezo wa kununua taulo kwa ajili kujisitiri katika kipindi cha hedhi, Taulo hizi zitawasaidia kujistiri katika kipindi hicho mkiwa kama Watoto wa kike”.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Zimbwini, Estomic Kimwemwe amewashukuru NACOPHA kwa msaada huo waliotoa kwa kuwagusa Watoto wengi wa Kike, amesema Watoto wengi wanatumia vitambaa kipindi cha hedhi hali inayo hatarisha usalama wa Afya zao.
Pia Kimwemwe ameyaoma Mashirika mengine kujitokeza kutoa misaada ili kuwasaidia Watoto hao kukabiliana na changamoto hiyo wanapokutana nayo.
Naye, Afisa Maendeleo wa Wilaya ya Kibiti, Anthony Nyange amesema Halmashauri hiyo imejipanga katika kuhakikisha mtoto wa kike anaishi katika kupata haki zake za msingi kama binadamu mwingine, ambapo alizungumzia kauli mbiu ya mwaka huu ambayo inasema KIZAZI CHA KIDIGITALI, KIZAZI CHETU ambapo aliwaasa wasichana kutumia mitandao ya kijamii kwa ustawi wao ili kutengeneza kizazi salama na kujenga Taifa imara.
Maadhimisho hayo yameenda sambamba na kutoa elimu ya jinsi ya kukabiliana na suala zima la mimba za utotoni ili kuwasaidia Watoto hao kufikia ndoto zao. Pia maadhimisho hayo
yalihudhuriwa na Mashirika na Asasi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali katika kuhaikisha nafasi ya mtoto wa kike katika jamii inaheshimiwa kama ilivyo kwa binadamu yoyote.
Meneja wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA) Kanda ya Dar es Salaam, Victoria Huburya (wa pili kutoka kulia) akikabidhi Box 20 za Taulo za Kike (Pads) kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari, Kibiti, Estomic Kimwemwe (kwa kwanza kutoka kushoto) kwa niaba ya Wanafunzi wa Kike 500. Wa kwanza kutoka kulia ni Afisa Maendeleo wa Wilaya ya Kibito, Anthony Nyange wakati wa zoezi hili lililofanyika mwanzoni mwa wiki hii katika Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani kwa kuwezeshwa na Shirika la UNAIDS.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...