Bidhaa za nyama, gesi ya kupikia, mkaa na viazi mviringo zimetajwa kuongeza mfumuko wa bei kutoka asilimia 3.8 Agosti hadi asilimia 4.0 kwa Septemba mwaka huu.
Taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) jijini Dodoma, imetaja bidhaa nyingine zilizoongeza mfumuko wa bei ni ngano na maziwa ya unga.
Akisoma taarifa hiyo kwa waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ruth Minja alisema sababu za kuongeza mfumuko ni kutokana na kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma.
Minja alisema mabadiliko hayo ni kwa mwaka ulioishia Septemba ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia Agosti 2021.
Amesema badiliko hilo la asilimia 0.2 limechangiwa na kasi ya mabadiliko ya bidhaa za vyakula kama unga wa ngano kwa asilimia 6.8, nyama ya ng’ombe kwa asilimia 3.4, maziwa ya unga kwa asilimia 9.2, mayai kwa asilimia 5.0 na viazi mviringo kwa asilimia 4.7 na kufanya kuongezeka kwa asilimia 4.0 kutoka asilimia 3.6 mwezi Agosti.
Amesema pia bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko ni gesi ya kupikia kwa asilimia 2.7, mkaa kwa asilimia 3.5, na huduma ya malazi katika nyumba za kulala wageni kwa asilimia 5.7na kufanya bidhaa hizo kuongezeka hadi asilimia 4.1 kutoka asilimia 4.0 mwezi Agosti.
Pia, amesema mfumuko wa bei katika nchi za Kenya na Uganda umeongezeka ambapo kwa mwaka ulioishia Septemba nchini Kenya umekuwa kwa asilimia 6.91 huku Agosti ukiwa ni asilimia 6.57
“Vilevile nchini Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2021 umeongezeka hadi asilimia 2.2 kutoka asilimia 1.9 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti,” amesema Minja.
Kwa upande wake Stanslaus Mrema ambaye ni Mchumi Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alisema kupitia taarifa hizo zinasaidia Serikali kuhakikisha halivuki lengo la kufikia asilimia 5 ya mfumuko wa bei kitaifa ambayo imejiwekea.
“Kwa upande wa Benki Kuu mfumuko wa bei ni moja ya kiashiria kikubwa sana katika utekelezaji wa majukumu yetu, kwamba Sera ya fedha inalenga viwango tunavyovikadiria vya mfumuko wa bei na ukuaji wa uchumi,” amesema.
Hata hivyo, amesema Serikali inajitahidi kuchukua hatua kwa kuangalia sehemu ambazo wanaweza kurekebisha akitolea mfano sakata la kupanda kwa bei ya mafuta lililotokea miezi kadhaa iliyopita na kuongeza tija kwenye uzalishaji ili kuinua masoko ambayo yameanguka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha Uviko-19.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...