Na Said Mwishehe, Michuzi TV.
TAASISI ya Teknolojia Dar es Salaam(DIT) pamoja na Shirika la Posta Tanzania (TPC) wamesaini mkataba wa ushirikiano katika maeneo matano yakiwemo ya kutumia utalaam na watalaam kuboresha mifumo ya TEHAMA ya shirika hilo.
Mkataba huo wa ushirikiano umesainiwa katika ofisi za DIT jijini Dar es Salaam ambapo kwa upande wa DIT wamewakilishwa na Mkuu wa taasisi hiyo Profesa Preksedis Marco Ndomba wakati Shirika la Posta Tanzana wamewakilishwa na Kaimu Postamasta Mkuu Macrice Mbado.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mkuu wa taasisi ya DIT Profesa Ndomba amesema makubaliano ya ushirikiano ambayo wameingia yataakisi uwezo mkubwa uliopo miongoni mwa watalaam walionao katika taasisi hizo na kudhihirisha namna wanavyoweza kusaidia nchi yao kutoa suluhisho kwa changamoto zinazoikabili jamii ya Watanzania na kuweka alama kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu mchango wa uhandisi,sayansi na teknolojia katika kuedeleza uchumi nchini.
Amefafanua mkataba huo wa ushirikiano ambao wameusaini kati yao na Shirika la Posta Tanzania utahusu DIT kutoa utalaam na watalaam kuboresha mifumo ya TEHAMA ya shirika hilo,kutumia ofisi za shirika la posta zilizopo mikoa yote nchini kuhamasisha uhawilishaji wa maarifa kwa wabunifu wadogo mikoani.
Maeneo mengine ni kutuma ofisi za Shirika la Posta Tanzania zilizopo mikoa yote nchini pamoja na mtandao wa mawasiliano kuwezesha ukuaji wa ujuzi wa kidigitali katika maeneo ya vijijini.Pia kutengeneza nafasi za mafunzo viwandani kwa taasisi hizo mbili kwa kupitia mafunzo ya wanafunzi viwandani na kuimarisha ushirikiano kwa kubadilishana watumishi wenye mafunzo viwandani.
"Postamasta Mkuu nikuhakikishie kuwa uwezo na weledi wa watalaam wa DIT hauna shaka na tegemea kupata kilicho bora kabisa katika ushirikiano huu ,kikubwa tu ni kwamba sisi kama taasisi tunapenda na kuenzi sana makubaliano ambayo yatakuwa hai na endelevu.
"Ili kufikia lengo kusudiwa na hili litawezeshwa na timu ya pamoja ya watalaam kutoka katika taasisi hizi ambayo tayari imekwishaundwa kuratibu na kusimamia utekelezaji wa yale yote tuliyokubaliana,"amesema Profesa Ndomba.
Aidha amewashukuru wadau mbalimbali wakiwemo watumishi wa DIT hasa watalaam wote kutoka kituo chao mahiri cha TEHAMA (ITCoEICT) kwa kusimamia na kufanikisha siku ya leo , naomba ushirikiano huu udumishwe na hasa katika kutoa mafunzo zaidi ya kitalaam kwa taasisi za serikali na binafsi na jamii kwa ujumla.
Amesisitiza kama ilivyo desturi ya DIT , wategemee kushuhudia vitendo zaidi ya nadharia , hilo linachangiwa sana na dhana ya teaching factory inavyotimizwa katika mafunzo yao na shughuli zote wanazozitekeleza."Kwa mundelezo huo tunaamini tutafikia lengo la makubaliano haya katika maeneo yote ya mikataba."
Profesa Ndomba amesema DIT imejipanga kutoa ushauri wa kitalaam inayokidhi mahitaji ya Shirika la Posta Tanzania ili kutatua changamoto za kiufundi zinazokabili shirika hilo hasa katika mifumo ya TEHAMA.
"Itoshe kusema ushirikiano huu unakwenda kufanya mabadiliko makubwa na yenye tija katika sekta ya TEHAMA ambayo pia yatasaidia kupunguza gharama kubwa za utendaji na kuongeza ufanisi serikalini,"amesisitiza.
Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Profesa Preksedis Ndomba (kushoto) na Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Mbado(kulia) wakiwa wameshika mikataba ya ushirikiano baada ya kuisaini.
Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Profesa Preksedis Ndomba (kushoto) na Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Mbado(kulia) wakisaini mkataba wa ushirikiano katika maeneo matano, lengo kuboresha utoaji huduma na kutatua changamoto zinaikabili jamii ya Watanzania.
Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Profesa Preksedis Ndomba (kushoto) akizungumzia faida ambazo zitapatikana baada ya kusaini mkataba wa ushirikiano kat yao na Shirika la Posta Tanzania.Kulia ni Kaimu Postamasta Mkuu Macrice Mbado.
Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania(TPC) Macrice Mbado akifafanua jambo kuhusu mkataba wa ushirikiano ambao wameusaini kati yao na DIT.
Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Profesa Preksedis Ndomba (kushoto) na Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Mbado(kulia)wakibadilishana mikataba ya ushirikiano baada ya kuisaini.
Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Mbado(kulia) akikabidhiwa kalenda ya DIT na Diary kutoka kwa Mkuu wa taasisi hiyo Profesa Preksedis Ndomba (kushoto).
Mwanasheria wa DIT(kushoto) na Mwanasheria wa TPC (kulia) wakishuhudia utiajia saini wa mkataba wa ushirikiano.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...