Na Joseph Lyimo

VIONGOZI wa Serikali na vyama vya kisiasa nchini wameaswa kupata chanjo ya Uviko-19 hadharani, ili kuhamasisha jamii ishiriki shughuli hiyo kuliko kuchanja wenyewe bila kuonekana.

Ofisa elimu ya msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Silvanus Tairo amesema endapo viongozi wa Serikali na vyama vya kisiasa wakipatiwa chanjo hadharani jamii nayo itashiriki kwa kiasi kikubwa.

Tairo amesema jamii inapata mwamko mkubwa pindi wakiwaona viongozi wao wanashiriki kupatiwa chanjo hivyo wataweza kujitokeza kwa wingi na wao kujumuika kwenye zoezi la chanjo ya Uviko-19.

Amesema kutokana na baadhi ya watu ambao siyo wataalamu wa afya kuzusha taarifa potofu kwenye mitandao ya kijamii juu ya chanjo inayotolewa kuna wengine wameingia hofu hivyo kushindwa kushiriki.

“Mwananchi wa kawaida pindi akimuona kiongozi wake wa serikali au chama cha kisiasa anachanjwa hadharani, naye anatamani kuchanjwa kwani anaona mfano kwa kiongozi,” amesema Tairo.

Amesema faida ya viongozi kuchanja hadharani ni kubwa kuliko kuchanja kwenye chumba peke yao bila kuonekana hivyo anatoa wito kwa viongozi watimize hilo ili kuchochea hamasa.

“Tumeona mara kadhaa kwa viongozi wanapochanjwa hadharani jamii hufuata nyayo zao na kuwa na amani mioyoni mwao kwa kuona kumbe taarifa potofu za mitandaoni hazina mashiko,” amesema Tairo.

Mkazi wa kata ya Terrat, Isaya Lemomo amewapongeza baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo na kata hiyo ambao wameshiriki kuchanja hadharani na kuwapa hamasa.

Amesema baadhi ya viongozi waliochanja hadharani ni diwani wa kata hiyo Jackson Ole Materi, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Baraka Kanunga Laizer na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo Awadh Omari.

“Tumehamasika kuchanja na sisi kupitia viongozi hao akiwemo pia Mwenyekiti mstaafu wa CCM wa Mkoa wa Manyara, Lucas Ole Mukusi, ambaye alichanja hadharani,” amesema Lemomo.

Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Abdi Seif amesema vingozi wanapochanja hadharani wao huamasika kushiriki kwani hudharau dhana potofu ya watu wasiokuwa na utaalamu wa afya wanaopotosha chanjo hiyo.

“Viongozi wetu tunawaamini mno ndiyo sababu tunapowaona wanachanjwa hadharani nasi tunapata imani kubwa ya kutumia chanjo hii ya Uviko-19,” amesema Seif.

Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Dkt Aristidy Raphael amesema wilaya hiyo ilipatiwa dozi 1,000 za chanjo ya Uviko-19 na kuongezewa nyingine 2,000 zikawa 3,000 na watu wengi wameshiriki kuchanja.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...