Na Zainab Nyamka, Michuzi TV
JESHI la Polisi Tanzania limemtaka Mwamuzi wa Kimataifa Inspekta Frank Komba kuendeleza ushirikiano mzuri na mataifa mengine atakapokuwa katika Fainali ya michuano ya mabingwa Afrika (AFCON) nchini Cameroon.
Komba amechaguliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuwa moja ya waamuzi watakaochezesha michuano y AFCON itakayofanyika Januari 2022 nchini Cameroon.
Akizungumza na Michuzi Blog, Msemaji wa Jeshi la Polisi SACP David Misime amesema kuchaguliwa kwa Kijana wao Inspekta Komba ni hatua moja muhimu na kubwa ambayo imelitangaza Jeshi la Polisi ndani na nje ya Tanzania.
“Tunampongeza Komba Kwani ameweza kulitangaza Jeshi la Polisi na ni hatua muhimu ndani na nje ya Tanzania na hii inaonesha uweledi awapo kwenye majukumu yake,”
Amesema, kuchaguliwa kwa Komba kunaonesha Tanzania kupitia Jeshi la Polisi lina waamuzi wenye uweledi, mafunzo na wanaaminika pindi wanapokuwa katika majukumu yao.
Misime amesema, “ukiachilia kusema michezo ni kujenga afya ila sisi kama Jeshi tunatumia michezo kama kuongeza ushirikiano na watu wengine na kupata taarifa mbalimbali hususani za kiuhalifu,”
Aidha, amesema mbali na kuwa moja ya waamuzi watakaochezesha michuano hiyo mikubwa Komba anaenda kuiwakilisha nchi na hilo litaenda kuongeza wigo mpana, mahusiano mazuri na ushirikiano kwa nchi zingine ambazo tumekuwa tunashirikiana nazo katika masuala mbalimbali ya kiusalama.
Mwamuzi Frank Komba ni mtumishi wa Jeshi la Polisi Tanzania na amekuwa moja ya Waamuzi wasaidizi wenye Beji ya FIFA waliochaguliwa na CAF kwenda kuchezesha michuano ya AFCON nchini Cameroon.
Komba ameweza kuwa moja ya waamuzi bora katika kipindi cha misimu miwili mfululizo na kupelekea kupata mechi nyingi za Kimataifa katika ngazi ya Klabu kutokana uwezo wake wa kusimamia Kanuni 17 za mpira wa miguu.
Mbali na kuwa mwamuzi wa Kimataifa Mwenye beji ya FIFA, ni Inspekta wa Jeshi la Polis na pia ni Mwanasheria kitaaluma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...