Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesimamisha shughuli zote za Mradi wa uvunaji na uzalishaji wa Chumvi katika eneo la Buyuni Kitopeni, Wilayani Pangani mkoani Tanga.

NEMC imechukua hatua hiyo ya kusimamisha shughuli hizo baada ya kubaini kuwepo athari za mazingira katika eneo la Wanyama kwenye Hifadhi ya Taifa ya Saadan (SANAPA) pamoja na makazi ya Watu wanaoishi karibu na eneo hilo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika eneo hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka amesema licha ya Mmiliki wa mradi huo kupata Leseni ya Wachimbaji wadogo, wamechukua hatua hiyo baada ya Mmiliki huyo kushindwa kubainisha athari za mazingira katika eneo husika ambapo pia ameshindwa kutafakari kwa kina kwenye tathmini ya mazingira hayo.

Dkt. Gwamaka amesema kulingana na taarifa za Hifadhi ya Taifa ya Saadani, eneo hilo la Mradi huo, limehusishwa kupita kwa Wanyama wengi wakiwemo Tembo ambao wamekuwa wakipita mara kwa mara kwa ajili ya kutafuta malisho na unywaji wa Maji.

“Tumesimamisha uzalishaji wa Chumvi, hadi Mmiliki aje kuthibitisha athari za mazingira, au atuambie amepata wapi ridhaa ya kuharibu mazingira. Sisi kwenye Takwimu zetu hatuajaona Mradi wowote wa jina ambalo unahusisha maeneo haya”, amesema Dkt. Gwamaka.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephraim Mwangomo amethibitisha eneo hilo ni makazi pendwa ya Wanyama wakiwemo Tembo ambao mara nyingi wamekuwa wakipita na kukaa mara kwa mara kwenye eneo hilo sambamba na Wanyama wengine kama Simba.

Mhifadhi Mwangomo ameeleza kuwa aliwahi kumshauri Mmiliki wa eneo hilo kujenga Hoteli maalum kwa ajili ya Watalii wanaotoka kwenye Mataifa mbalimbali na Watalii wa ndani ya nchi kwa faida yake baada ya kupata eneo hilo karibu na Hifadhi ya Taifa ya Saadani, pia kuendana na Mazingira ya eneo husika.

“Hapa kwenye Hifadhi ya Saadani tunapokea Watalii 4000 kwa mwaka, Watalii kutoka nje ya nchi, wenzetu kule Zanzibar wanapokea Watalii kutoka nje ya nchi, Laki Tatu (300,000) kwa mwaka. Lakini Watalii wakitaka kuja hapa Saadani tunaweza kupata Watalii Elfu hamsini (50,000) na zaidi lakini hakuna sehemu za kuwalaza, hakuna Hoteli”, amesema Mhifadhi Mwangomo.

Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Buyuni, Diwani Akida amesema kuwa Mradi huo ulianza mwaka 2015 baada ya kupewa na Kijiji hicho Hekari 50 pekee, amesema baadaye alipatiwa Hekari nyingine na Wamiliki wengine ambapo sasa anamiliki zaidi ya Hekari 100.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka (wa mbele) akiangalia vyungu vya kuzalishia Chumvi eneo la Buyuni Wilayani Pangani Tanga, wa nyuma ni Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephraim Mwangomo.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephraim Mwangomo (kushoto) akimueleza jambo Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka (wa kulia) baada ya kuwasili kwenye eno hilo la Hifadhi ya Taifa ya Saadani ambapo kumekuwa na athari za mazingira kutokan na shughuli za uzalishaji Chumvi.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...