Mwanaharakati wa jinsia na haki za binadamu kutoka TGNP, Gemma Akilimali akitoa mada wakati wa mafunzo maalum kwa wakuu wa idara wa jiji la Ilala juu ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia na kueleza kuwa kupitia vitengo vya idara hizo wasimamie bajeti kwa usawa katika makundi yote pamoja na kutoa elimu kwa vikundi mbalimbali hususani vya wanawake vinavyopambana na mfumo dume.


MTANDAO wa Kijinsia Tanzania (TGNP,) wiki hii ulikutana na kutoa mafunzo ya bajeti yenye mrengo wa kijinsia (GRB,) kwa wakuu wa idara katika jiji la Ilala mkoani Dar es Salaam ili kuwasaidia katika bajeti za ngazi ya Wilaya zinazotarajiwa kufanyika kuzingatia mlengo huo na hiyo ni pamoja na kufafanua umuhimu wa bajeti kwa jamii, changamoto na ufumbuzi wa masuala mbalimbali ya kijinsia hasa kwa kundi la wanawake, watoto na kundi la wenye ulemavu.

Akitoa mada katika mafunzo hayo Mwanaharakati wa jinsia na haki za binadamu kutoka TGNP, Gemma Akilimali alieleza changamoto za tofauti za kijinsia zinavyoathiri wanawake katika nyanja mbalimbali ikiwemo uchumi.

''Wanawake ndio walezi wakubwa wa familia, watafutaji katika kila aina ya mazingira na wapo kwenye hatari katika utafutaji wao ni jukumu letu kupaza sauti na Serikali ya awamu ya sita ni sikivu itasikia hili kwa kuwaweka salama akina mama na watoto pindi wanapokuwa katika shughuli za utafutaji.'' Amesema.

Alieleza kuwa bado kuna changamoto za kutoa maamuzi kuanzia ngazi ya familia ambapo baadhi ya tamaduni bado hawawatambui wanawake katika nafasi hiyo jambo ambalo limepitwa na wakati na kandamizi kwa jamii ya sasa kuendeleza kauli za mwanaume ni kichwa/kiongozi katika familia.

Mafunzo yakiendelea.

Mwanaharakati wa jinsia na haki za binadamu kutoka TGNP, Gemma Akilimali akitoa mada katika mafunzo hayo na kuwahimiza viongozi hao kuangalia makundi yote kwa usawa katika bajeti yenye mrengo wa kijinsia.


Katika mafunzo hayo hayo suala la bajeti lilitazamwa kwa jicho la inayotatua changamoto za ukosefu wa usawa na haki ya uchumi kwa kuhakikisha rasilimali zote zinawanufaisha wanawake na wanaume bila ubaguzi. Mfano, bajeti kwa ajili ya umilikishaji wa ardhi na rasilimali nyingine.

Suala la bajeti ni mtambuka na kwa mujibu wa dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2025 imebainisha wazi kuwa bajeti ni ya kuondoa utofauti/ubaguzi wa rangi na kijinsia katika kushiriki shughuli za kiuchumi pamoja na kujenga jamii ya Kitanzania yenye usawa na wanawake wenye uwezo katika masuala yote ya kiuchumi, kijamii na mahusiano ya kisiasa na kiutamaduni.

Baadhi ya washiriki wakichangia mada katika mafunzo hayo ya bajeti yenye mrengo wa kijinsia yaliyotolewa na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP.)


Mapendekezo yaliyotolewa ni pamoja na kasi ya usambazaji wa maji hususani vijijini na miundombinu iendane na uwekezaji katika kuhakikisha miundo mbinu yenyewe au miradi inafanya kazi kwasababu ni kiasi kikubwa cha fedha ambazo ni kodi za wananchi zinazotumika kujenga miundo mbinu.

Aidha wamependekeza katika bajeti kuwepo na ongezekezo la wanawake katika uongozi wa taasisi au mamlaka zinazokusanya mapato yatokanayo na maji hususani katika miradi iliyoko ngazi ya kata au vijiji, ambapo TGNP imeshuhudia ongezeko mara dufu ya mapato baada ya wanawake katika moja ya kata Morogoro kushika usukani katika mradi wa maji.

Mafunzo yakiendelea.

Vilevile katika kufanikisha bajeti yenye mrengo wa kijinsia wamependekeza kuwepo kwa mjadala wa pamoja katika sekta muhimu za Afya, Elimu, Maji, Kilimo, na kumaliza Ukatili wa kijinsia.

Mafunzo hayo yaliyotolewa na TGNP yalihusisha idara za utawala na utumishi katika sekta za elimu, uvuvi, elimu, takwimu, mipango miji, afya na mazingira.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...