WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi,
Prof. Makame Mbarawa, amevunja Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa
Bandari Tanzania (TPA), na Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL),
kwa sababu ya uzembe na usimamizi mbovu wa miradi.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar
es Salaam, wakati akizungumza na waandishi
wa habari mara baada ya ufunguzi wa maboresho ya Gati namba 0 hadi 7 na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi
wa miundombinu ya Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Pili (km 20.3)
uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
"Leo tarehe 04/12/2021 kwa
Mamlaka niliyonayo nimetengua Bodi za Wakurugenzi wa TPA na MSCL kutokana na
kutokuwajibika ipasavyo katika kutoa ushauri na wakati wa ubadhirifu na
ukiukwaji wa vipengele katika mikataba ya miradi walikuwepo", amesema
Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesema kuwa
uamuzi huo umetokana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoridhishwa na utendaji
kazi wa Bandari ya Dar es Salaam hasa
katika usimamizi wa gati hizo zilizoboreshwa kutokuwa mzuri na kusababisha
kuwepo kwa marekebisho ya baadhi ya gati ili viendane na viwango vinavyostahili
kulingana na mkataba.
Prof. Mbarawa ameeleza pia
kumeripotiwa matukio ya wizi katika mifumo ya bandari ambapo mkandarasi
aliyefunga hiyo mifumo hakuitekeleza ipasavyo na kuacha mianya ya wizi
ukaendelea.
Kwa upande wa Kampuni za Huduma
za Meli Tanzania (MSCL), Prof. Mbarawa amebainisha kumekuwa na mapungufu kwa
mkandarasi aliyeshinda kazi za ujenzi wa meli nne zinazotarajiwa kujengwa
katika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Bahari ya Hindi.
"Baada ya utiaji saini
mikataba minne tarehe 15 Juni, 2021 Serikali ilitilia shaka uwezo wa mkandarasi
na kuamua kufanya ufuatiliaji wa uwezo wa mkandarasi huyo aliyeshinda zabuni na
kubaini kuwa hana uwezo wa kutengeneza meli na hakuwa na ofisi”, amefafanua
Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa ametoa rai
kwa watendaji wote waliopo chini ya Wizara yake kuwa waadilifu na kusimamia kwa
karibu miradi yote inayoendelea kutekelezwa.
"Naomba nichukue fursa hii
kuwataka watendaji wote kuwa waadilifu, wazalendo, tuumwe na nchi hii katika
miradi ya kiamaendeleo", amesisitiza Prof. Mbarawa.
Bodi ya Wakurugenzi ya TPA ilikuwa na jumla ya wakurugenzi saba (7) ikiongozwa na Mwenyekiti Prof. Ignas Rubalatuka na Bodi ya MSCL ina wakurugenzi watano (5) ikiongozwa na Mwenyekiti Prof. Zacharia Mganilwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...