Na Humphrey Shao, Michuzi Tv
SHIRIKA la nyumba la Taifa limekuja na mpango kabambe Kwa wateja wake ambao wanalimbikiza kodi Kwa kufunga vitasa vya kidigitali ambavyo vitakuwa vinajifunga venyewe (Automatic) hivyo mpangaji kushindwa kuingia ndani wala kutoka nje.
Akizungumza hayo leo jijini Dar es Salaam,Meneja Habari na Mahusiano wa NHC,Muungano Saguya wakati akiongea na waandishi wa habari kwa shughuli mbalimbali walizozitekeleza tangu walipoanza mwaka 2021 na mipango waliyona kwa mwaka ujao 2022.
Alisema katika kutekeleza mpango huo,shirika hilo litafata sheria zote ya mpangaji kama kawaida hivyo kama mpangaji akiwa hajalipa kodi kwa muda unaotakiwa atapatiwa notisi.
“Notisi hiyo ambayo itakuwa ni ya siku 30 baada ya hapo atapewa notisi na dalali wa mahakama ya siku 14 kisha kumalizika kwa utaratibu huo utaratibu wa kumfungia utakuwa umekamilika,”alisema na kuongeza
“Hii itazuia kidogo kwenye suala la ulimbikizaji wa madeni,hii inakuwa kama wanavyofanya watu wa kwenye umeme na maji,”alisema
Aidha alisema ifikapo mwezi Januari mwakani ,shirika lao litaanza mpango kabambe la kukusanya madeni yake yote kwa wapangaji walihama na madeni pamoja na waliolimbikiza kodi.
Alisema maelekezo haya yametolewa na Serikali,Bodi pamoja na Menejimenti ya shirika hilo kuhakikisha kodi hizo zinakusanywa kwa watu hao ambao sio waaminifu.
“Kodi hizi zikikusanywa zote zinauwezo wa kujenga nyumba nyingine 450 na kusaidia watanzania wengine kupata makazi,hatutakuwa na msalie mtume kwa mtu ambaye hawezi kulipa kodi,”alisema na kuongeza
“Hivi sasa tunachambua madeni haya ni nani ni nani,…na anadaiwa kiasi gani,tujue kama wapo hai au wapo sehemu gani tutashirikiana na Mamlaka zingine Nida na Brella kuhakikisha tunataarifa zao zote muhimu hasa kwa watu ambao wametelekeza nyumba na kuacha madeni makubwa,”alisema
Hata hivyo Saguya alisema kwa mwaka 2022 shirika lao linatarajia kutekeleza ujenzi wa majengo ya biashara ya Kashozi mkoani Bukoba,Mtanda mkoani Lindi,Kahama mkoani Shinyanga pamoja na Masasi mkoani Mtwara.
“Shirika pia linatarajia kujenga nyumba za makazi Isomvu Sumbawanga na maghala ya mazao sehemu mbalimbali ya nchini huku kuendelea na mradi wa uuzaji wa viwanda kwaajili ya ujenzi wa nyumba za makazi na majengo ya biashara,”alisisitiza Saguya
Alisema katika mwaka huo 2022,NHC inatarajia kuanzisha viwanda vyake vya matofali,kokotona bati kwaajili ya kupunguza gharama za ujenzi na kupata vifaa bora vya utekelezaji wa miradi yao.
Meneja Habari na Mahusiano wa shirika la nyumba la Taifa Muungano Saguya akizungumza na waandishi wa Habari.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...