Adeladius Makwega,Dodoma.

Utani katika kabila ya Wazaramo umegawanyika katika makundi makubwa mawili nayo ni utani baina ya wazaramo na makabila mengine na utani baina ya ukoo na ukoo. Kwa sasa unapomuuliza mzaramo wa leo juu ya asili ya yeye kutaniana na kabila lingine inawezekana ikawa vigumu yeye kukupa majibu sahihi juu ya asili ya utani huo.

Unaweza ukajibiwa kuwa:

“Aka nie siumanyile utani wizase, wose tuvika vivo.”

Akimaanisha kuwa hafahamua utani uliazanje wote tumekuta tu hivyo.

Lakini je utani baina ya Wazaramo na makabila mengine ulitokanaje? Inaaminika kuwa Wazaramo na baadhi ya watu waliokuwa wakiishi kandokando za Bahari ya Hindi walikuwa ni mabingwa wa kutengeneza chumvi kutokana na maji ya bahari hivyo kazi hiyo iliwasukuma mara walipomaliza kutengeneza waliibeba chumvi hiyo na kwenda kuiza huko bara.

Biashara hiyo iliendelea kwa muda mrefu sana na hata mara baada ya ujio wa Waarabu uliwakuta watu wa Pwani wakifanya biashara na watu wa maeneo hadi ya Unyamwezini maeneo yote ya Tabora na jirani zake.

Biashara hiyo ya chumvi iliwavutia watu kutoka Tabora nao kwenda hadi Pwani kufuata chumvi. Ujio wa Waarabu uliwabeba watu wa Tabora kama watumwa au wapagazi kwa kubeba pembe za ndovu hadi pwani. Huku ikiaminika kuwa hawa watu wa Pwani ambao walikuwa wakifanya biashara na watu wa Tabora walikuwa wajuzi wa lugha ya Kiswahili hivyo waliwasindikiza Waarabu katika safari hizo za kufuata watumwa na bidhaa zingine.

Kwa kuwa Wazaramo walienda na Waarabu kufuata watumwa na pembe za ndovu na watumwa hao walikuwa Wanyamwezi. Wazaramo wakawaita Wanyamwezi watumwa wao. Kwa hiyo kwa kuwa ilitumika dhihaka kwa Wanyamwezi kuwa watumwa hapo hapo utani ukaibuka baina ya Wazaramo na Wanyamwezi.

Baadhi ya Wanyamwezi walikwenda Uzaramoni na kwa kuwa walikuwa wageni walifanya vibarua katika mashamba ya Wazaramo ili waweze kuishi na ilikuwa ngumu tena wao kurudi Tabora. Inaaminika kuwa idadi ya Wanyamwezi kutoka Tabora ilikuwa kubwa katika maeneo ya Wazaramo, hilo likaleta ugomvi baina ya Wazaramo na Wanyamwezi lakini Wazaramo hawakuwa na silaha za kupambana na Wanyamwezi ambao walikuwa mabingwa wa vita, kwa kuwa Wanyamwezi walikuwa ni kabila la kivita na Wazaramo walikuwa wachache mno kwa hiyo Wanyamwezi walitumia hekima hapo ndipo utani wa Mzaramo na Mnyamwezi ukadumu hadi sasa.

Ndiyo kusema Wazaramo wanawaita Wanyamwezi ”Mwe mwatuma zetu.” Hawa watumwa zetu na Wanyamwezi wanaita Wazaramo kuwa ni wavivu, hawana nguvu, watu wafupi, wasemaji tu na hawawezi kulima. Wanyamwezi wanaenda mbali na kusema kuwa hawezi kupigana na mtu ambaye hata chakula cha kula hana.

Utani huo unakwenda mbali kwa Wazaramo kuwatania Wanyamwezi kuwa ni WANYA+MWEZI hashakumu si matusi-wanakunya mwezi. Falsafa kando ya hilo ni kuwa kwa kuwa Wanyamwezi wanatoka magharibi ya pwani na huko ndipo mwezi unapotokea na ndiyo maana wakaitwa Wanyamwezi.

Kutokana na hilo hata wasukuma waliingia katika mkumbo huo huo kwa kuwa Wazaramo walishindwa kuwatafautisha Wanyamwezi na Wasukuma kimaumbile na wanavyoongea. Kwa hiyo kiasili hakuna utani baina ya Wazaramo na Wasukuma bali Wasukuma waliingia kimakosa kwa kuwa watani wa Wazaramo.

Swali ni je huo utani unafanyikaje? Mara zote utani huo upo katika mazungumzo kwa mfano. Mzaramo humwambia Mnyamwezi ”Kwa mtumwa wangu gwe hata ukaigoda kefle.” Hata ufanyeji wewe ni mtumwa wangu tu, huna lolote.”Tena kwa muhonjo.” Tena haujatairiwa.”, ” Utali Kongo mgoi” akimaanisha mrefu kama chatu.

“Izo unilimile mgunda wangu nikugwelele hela” Njoo ulime shamba langu nikupatie pesa. “Wakulonjele kuchezela mizoka tu konga kuna moyo.” Ujuzi ulionao ni wa kuchezea nyoka tu kama mwendawazimu. Kwa kuwa Wasukuma waliingizwa utani kimakosa na wao wanayapata matusi ya Wazaramo.” Genda kacheze na ng’ombe huko.” Nenda kacheze na ng’ombe.

Wanyamwezi na wasukuma hujini mapigo kwa wazaramo kuwa watu wavivu hawewezi hata kupambana na ndama wa ng’ombe, hawawezi hata kulima shamba dogo la mihogo kazi yao kubwa ni kunywa madafu na ndiyo maana wanakuwa ni mabusha.

Japokuwa hayo husemwa kwa mzaramo, mara zote Mzaramo huwa harudishi majibu hukaa kimya tu na utawasikia Wanyamwezi na Wasukuma wanasema Kazaramo hako. Utani huo uenda hadi katika kumpokonya Mzaramo vitu vyake mathalani Mnyawezi anaweza akafika katika shamba la Mzaramo akachimba muhogo na kuondoka nao. Hapo Mzaramo akitambua kuwa mtani wake kafanya hivo huwa hana cha kufanya.

Pia unatazamwa utani baina ya Wazaramo na Wadigo ikiaminika kuwa wadigo walikuwa ni mabingwa wa kuroga kwa hiyo kutokana na ufundi huo Wazaramo hawakuwa na budi kujenga mazoea na wadigo kwa ustadi wao wa elimu hiyo ya ushirikina.

“Hawi lakini gwe kuzidi, koguluka konga ndege ulaya, kwa galu.” Nyinyi ni wachawi zaidi, yaani mnaweza kuruka kama ndege ulaya. Utani wa Wazaramo na Wadogo hauwi mkubwa kama ule wa Wasukuma na wanyamwezi kwa sababu ya kuogopa kurogana.

Kwa desturi Wazaramo lugha yao inavyoongea huwa inachekesha kwa hiyo hilo limefanya hata Wazaramo kuwa na utani na kila mtu wanayekutana naye kwa hiyo Mzaramo anapokutana na mtu yoyote anayemfahamu huwa wanapenda kufanya utani hata kama hayupo katika makundi hayo niliyoyataja.

“A wee, nakuona unanoganoga tu siku hizi” nakuona siku hizi unafuraha sana. “Na mtungi mwingi na mabibi kwa wingi vile vile.” Akimaanisha kuwa unakunywa pombe nyingi na wanawake wengi. Lugha hiyo ni maarufu mno katika maeneo ya Dar es Salaam na viunga vyake.


makwadeladius@gmail.com

0717649257




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...