Huku ikiwa imebaki mwezi mmoja na siku chache kabla ya mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon, usajili unaendelea kushika kasi huku waandaaji waitoa wito kwa washiriki wajisajili mapema kuepusha usumbufu.

Taarifa iliyotolewa na waandaaji wa mbio hizo Jijini Dar es Salaam, ilisema punguzo la asilimia 20 lililokuwepo tangu Oktoba mwaka jana lilimalizika  Januari 7, 2022. Punguzo hili lilikuwa kwa ajili ya bei za kujisajili.  
 
Tayari bei za mbio tofauti zimepanda isipokuwa kwa km 5 huku wakitoa wito kwa washiriki wajisajili mapema kuepusha usumbufu dakika za mwisho kwani mbio hizo zinaadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.  

“Punguzo hili limekuwepo tangu Oktoba 17 mwaka jana wakati usajili ulifinguliwa rasmi na bei za usajili zimepanda sasa,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza kuwa usajili ni kwa njia ya mtandao www.kilimanjaromarathon.com au kwa njia ya Tigo Pesa kwa kubonyeza*149*20#.

Hapo awali, watanzania na wananchi wa Afrika Mashariki walikuwa wanalipa Tsh 25,000 kwa mbio za km 42 na 21 na za km 5 Tsh 5000 lakini sasa wameanza kulipa Tsh 30,000 kwa mbio za Km 42 na 21 na km 5 imebaki vile vile Tsh 5,000.

Kwa mujibu wa waandaaji hao, wakazi wa Tanzania na wa Afrika mashariki wenye vibali vya kazi au vibali vya ukaaji na wananchi wa SADC  walikuwa wanalipa $40 kwa mbio za km 42 na 21 lakini kuanzia Januari 8, 2022, walianza kulipa $50 lakini bei ya km 5 imebaki kuwa $5.


“Washiriki wa kimataifa walikuwa wanalipa $80 ila kuanzia Januari 8, 2022 walianza kulipa $90 kwa km 42 na 21 na km 5 imebaki kuwa $ 5,” walisema waandaaji hao.
Taarifa hiyo ilisema usajili utafungwa saa sita ya usiku Februari 7, 2022 au pale ambapo nafasi zitajaa hata kama ni kabla ya tarehe hiyo.

“Tunatoa wito kwa washiriki wote wazingatie tarehe hizi kuepuka usumbufu kwani huenda namba zote zikaisha kama miaka ya nyuma na huku ikizingatiwa kuwa mwaka huu tunaadhimisha miaka 20,” walisema waandaaji.

Waandaaji hao pia walisema kupitia taarifa hiyo kuwa maandalizi  yanaendelea vizuri ili kuhakikisha mbio hizi za 20 zinakuwa za aina yake na zinaacha kumbukumbu ya kipekee kwani mbio hizo, zilizoanza na washiriki wasiozidi 500 waliokimbia kwa kujifurahisha, sasa zinajivunia washiriki zaidi ya 12,000 kutoka mataifa zaidi ya 55 na watazamaji wanaokaribia idadi hiyo ya washiriki. 

Wakati wakiadhimisha miaka 20 ya mbio hizo waandaaji hao pia wametaja sababu 20 za washiriki kujiunga na mashindano hayo ambayo ni pamoja na medali za kiwango cha hali ya juu-kwa wote watakaomaliza mbio, tisheti za kiwango cha juu za kukimbilia-kwa washiriki wote waliojisajili, vituo vya maji vya kutosha na baadhi vya soda aina ya Coke, eneo la matibabu na magari ya huduma ya kwanza katika ruti nzima na eneo la kumalizia, usalama wa kutosha katika ruti nzima na kwenye vituo vya maji, magari kuongozwa na polisi wa traffic pamoja na baadhi ya barabara kufungwa kwa muda, burudani ya kutosha katika eneo la kumalizia mbio na eneo maalumu la kuuza bia na vinywaji vingine pamoja na vyakula vya aina tofauti.

Sababu nyingine ni shamrashamra za aina yake wikiendi ya mashindano, ruti imepimwa kitaalamu na kuhakikiwa na Shishikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF). Hii ina maana kuwa umbali unaokimbia ni halisi na pia inakufanya uweze kufuzu kushiriki katika mbio nyingine kubwa kama vile Comrades Marathon na pia kuwa sehemu ya Abbot WMW Wonder Age Group World Rankings.

Sababu nyingine ni muda uliokimbia ni halisi kwani vifaa vya kupima muda vimethibitishwa na IAAF, matokeo yote yanapatikana ndani ya saa 24, namba za kukimbilia zinatolewa Dar es Salaam, Arusha na Moshi kabla ya mashindano, usajili kwa njia ya mtandao na kwa njia ya Tigo Pesa kwa watanzania, maonesho ya kwanza ya aina yake ya watu (The People’s Expo) yatakayofanyika Moshi.  Ya kwanza kwa Kili Marathon.

“Kila mshiriki ataweza kupakua picha yake yenye ubora wa hali ya juu bila malipo yoyote,  Kipindi maalumu cha dakika 13 chenye matukio mbalimbali ya Kili Marathon katika chaneli ya Super Spot ya DSTV, nafasi katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo magazeti, redio, televisheni na mitandao ya kijamii, wadhamini wenye hadhi na wa uhakika na sababu ya 20 ni mbio za Kili marathon huvutia washiriki kutoka zaidi ya nchi 50 kuthibitisha kuwa ni tukio la kimataifa,” walisema waandaaji hao.

Mbio za mwaka huu zitafanyika Jumapili Februari 27, 2022 katika Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi (MoCU).

Wadhamini wa mbio za mwaka huu ni Kilimanjaro Premium Lager- 42km, Tigo- 21km, Grand Malt -5km wadhamini wa meza za maji ni Absa, Unilever, TPC Sugar, Simba Cement, Kilimanjaro Water na wasambazaji maalumu GardaWorld Security, Keys Hotel, Kibo Palace Hotel na CMC Automobiles.

Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon huandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa kitaifa na kampuni ya  Executive Solutions Limited.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...