Na Muhidin Amri,Mbinga
WANUFAIKA wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika kata ya Amani Makolo
Halmashauri ya wilaya Mbinga,wametakiwa kutumia kiasi cha fedha
wanazopata kuwekeza katika elimu ya watoto wao kwa kuwapeleka shule,
badala ya kuzitumia katika anasa.
Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali
Wilbert Ibuge,wakati akizungumza na wanufaika wa mpango huo wa kata ya
Amani Makolo Halmashauri ya wilayani Mbinga akiwa katika ziara ya siku
moja kutembelea kaya maskini zinazopokea ruzuku ya fedha kutoka mfuko wa
maendeleo ya jamii(Tasaf).
Alisema, madhumuni ya mpango kunusuru kaya maskini ni kuziwezesha jamii
hasa kaya hizo kuongeza kipato,fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji ya
msingi ikiwamo chakula,malazi,afya, elimu na kuziwezesha kuwekeza
kwenye rasilimali watu kwa kuwapa ruzuku yenye masharti kwa watoto
kuhudhuria shule na kliniki.
Ibuge amewataka walengwa hao, kutumia fedha hizo kama ilivyo mpango wa
Serikali ambao unalenga kuhakikisha kila mtoto hapa nchini anayetoka
katika familia maskini anapata elimu,matibabu kwa wazazi na walezi
kujiunga na mfuko wa afya ya jamii na wanufaika kujikimu kimaisha.
Alisema, ni muhimu kutambua uzito wa kile wanachopokea na Serikali
ambayo ina nia njema na wananchi kwa kutafuta na kutoa fedha ili ziweze
kubadili maisha ya baadhi ya watu wenye kipato duni ili kuwajengea
uwezo kiuchumi na kushiriki kazi mbalimbali za maendeleo katika jamii.
Alisema, unufaikaje huo ni lulu na hauwezi kuendelea milele, hivyo
amewakumbusha wanufaika wa mpango huo kukumbuka kujiwekea akiba na
kuanzisha miradi ya kiuchumi ili waweze kujitegemea siku za baadaye
badala ya kuendelea kuitegemea Serikali.
Aidha Jenerali Ibuge,amewataka wananchi wa wilaya ya Mbinga kutunza
mazingira na kulinda vyanzo vya maji wakati huu ambao wanaendelea na
shughuli zao za kilimo na kuwaagiza viongozi wa vijiji,kata na wilaya
kusimamia sheria za mazingira zilizopo.
Amewapongeza baadhi ya wananchi waliojiunga na mfuko wa afya ya
jamii,hata hivyo amewataka viongozi wa wilaya hiyo kuendelea kuhamasisha
watu wengine kujiunga na mfuko huo ili waweze kupata matibabu kwa
urahisi pindi wanapougua.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo alisema,
wilaya hiyo yenye Halmashauri mbili imepokea jumla ya
Sh.3,122,582,400.00 kwa ajili ya malipo ya walengwa 12,067 wa mpango wa
kunusuru kaya maskini katika vijiji 195.
Alisema,Halmashauri ya wilaya imepokea Sh.2,243,912,400.00 kwa ajili ya
malipo ya kaya 8,669 na Halmashauri ya Mji Mbinga imepokea
Sh.878,670,000.00 kwa ajili ya kaya 3,398.
Mamgosongo alimueleza Mkuu wa mkoa kuwa, mwaka wa fedha 2020/2021 malipo
yamefanyika katika awamu sita na kaya 8669 zimenufika kwa vipindi vya
miezi miwili katika kila dirisha la malipo kwa kupokea ruzuku ya msingi
na ruzuku ya masharti na Sh.2,243,912,400.00 zimelipwa kwa kaya
maskini.
Alisema,kupitia mpango huo kumekuwa na mafanikio makubwa ambapo fedha
zinazohawilishwa kwa kaya za walengwa vijijini zimeweza kutoa msukumo
katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kutokana na ongezeko la mzunguko
wa fedha.
Mangosongo alitaja mafanikio mengine ni baadhi ya kaya kutumia sehemu ya
fedha wanazopata kujiunga na mfuko wa afya ya jamii iliyoboreshwa
ambapo jumla ya kaya za walengwa 4,918 kati ya kaya 8,669 sawa na
asilimia 77 zimejiunga na mfuko huo.
Alisema, kupitia mpango huo kasi ya watoto walio chini ya umri wa miaka
mitano kupelekwa kliniki ni kubwa na mahudhurio ya wanafunzi wa shule
za msingi na sekondari yameongezeka kufuatia kuboreka kwa maisha ya
watoto wanaotoka katika kaya maskini.
Baadhi ya walengwa wa mpango wa kunusuru kaya masikini kata ya Amani Makolo Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma wakimsikiliza Mkuu wa mkoa huo Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge(hayupo pichani) wakati wa ziara ya Mkuu wa mkoa kutembelea kaya maskini zinazopata ruzuku kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii nchini Tasaf katika Halmashauri ya wilaya Mbinga.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...