Na Said Mwishehe, Michuzi TV

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu changamoto ya uhaba wa dawa,hivyo ametoa rai kwa Bohari ya Dawa( MSD) kuhakikisha inatatua changamoto hiyo ya ukosefu wa dawa haraka.

Ametoa kauli hiyo leo Januari 21,2022 wakati alipofanya ziara MSD kwa lengo la kukagua hali ya uwepo wa dawa sambamba na kukaa na menejimenti ya bohari hiyo na kisha kuweka mikakati itakayofanikisha kuondoa changamoto zilizopo ambazo zimekuwa zikiwababisha uhaba wa dawa katika zahanati na vituo vya afya

"Kumekuwa na malalamiko mengi ya wananchi kukosa dawa wakati Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa inatoa fedha za kutosha kwa ajili ya huduma katika sekta hiyo.Januari hadi Desemba 2021, MSD ilikuwa inatakiwa kusambaza dawa zenye thamani ya Sh.bilioni 519, lakini dawa ambazo zimetolewa ni za Sh. bilioni 160 sawa na asilia 31, wameshindwa kusambaza dawa kwa asilimia 70. Nakwenda kukaa na menejimenti ya MSD ili kujua tatizo ni nini," amesema.

Kwa mujibu wa Ummy, kwa kuwa makisio yapo, hakuna haja ya kununua dawa kwa zimamoto bali zinunuliwe za miezi sita.Aidha, amepongeza Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Meja Jenerali Gabriel Mhidze (Dkt.) kwa kuanzisha viwanda vya dawa vya Bohari Kuu, ili kutatua changamoto ya dawa nchini.

"Nataka niwapime MSD kwa kutekeleza wajibu wao. Niwaahidi wananchi nitalisimamia hili, mapema vipaumbele vyangu ni pamoja na kusimamia ubora wa huduma za afya ikiwemo muda anaofika mgonjwa kituoni na kuhudumiwa, upatikanaji wa vipimo, lazima tuwe na tofauti kati ya mtu kwenda hospitali na kwa mganga," amesema.

Ameongeza kwamba Serikali inataka kuona kunakuwepo na uhakika wa upatikanaji wa dawa, kudhibiti wizi na ubadhirifu huku akitumia nafasi hiyo kutoa onyo kwa watumishi waliopo kwenye sekta ya afya ambao wamekuwa wakishindwa kutimiza majukumu yao wawapo kazini.

"Yapo malalamiko kutoka sehemu mbalimbali kuhusu baadhi ya watumishi wa afya kushindwa kutekeleza majukumu yao ya msingi. Wapo wanaofika kazini na kuzunguka bila ya kuhudumia wananchi, kutoa lugha chafu, watu hawapati huduma kwa muda stahiki,"

"Niwaambie wale wanaofanya hivyo kwamba, serikali ni moja zinazobadilika ni zama tu kwa kupokezana kijiti, misingi na majukumu ya utumishi katika sekta ya afya bado iko vile vile, kila mmoja ahakikishe anatekeleza wajibu wake.Serikali inafuatilia kwa karibu mienendo ya watumishi wa afya na yeyote atakayepatikana akizembea na kuacha kuwahudumia wananchi wanaofika vituoni kupata huduma, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake,"amesema.

Kuhusu mabadiliko ya watendaji katika sekta ya afya, Waziri Ummy Mwalimu amesema kumeibuka tabia kwa baadhi yao kuwa na lugha chafu kwa wagonjwa, kufanya kazi kwa mazoea na kutokidhi miongozo ya utoaji huduma.

Amesema Serikali ni moja, uongozi ni kupokezana kijiti, hivyo wale watumishi wanaodhani wakifanya vitendo vya hovyo wako salama ni vema wakaacha mara moja na kwamba atafanya ziara maeneo yote yanayolalamikiwa ili achukue hatua.

Akizungumzia huduma ya afya ya mama na mtoto, Waziri Ummy amesema Rais Samia ameweka kipaumbele katika afya hususan eneo la huduma ya mama na mtoto, hivyo amewaagiza wahudumu wa sekta ya afya kuhakikisha wajawazito wanapata huduma stahiki.

"Nitaenda Mwananyamala na hospitali zote, pia nitahakikisha wananchi wanajengewa uwezo kufahamu haki zao za Msingi wanaofika vituoni. Niwape salamu hospitali yetu ya Taifa Muhimbili, wanaofanya vizuri katika huduma za kibingwa lakini malalamiko ni mengi. Jumatatu nitafanya ziara," amesema.

Kwa upande wake, Meja Jenerali Mhidze alisema kulikuwa na 'gape' (pengo) la miezi 18 ya kutonunua dawa kutokana na janga la corona huku uzalishaji kwa baadhi ya nchi ukiwa umepungua na nchi hizo wenyewe mahitaji yakiwa yameongezeka.

Pia, amesema usafirishaji wa dawa ni tatizo kutokana na vizuizi vya safari vilivyopo, lakini kwa sasa wameanza kupunguza mashartihivyo wanatarajia kupokea mzigo mkubwa wa dawa hivi karibu."Nikuhakikishie Waziri wetu wa Afya na Watanzania kwa ujumla changamoto ya kukosekana kwa baadhi ya dawa tunakwenda kuitatua, tumeshachukua hatua kadhaa."




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...