Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MAKANDARASI nchini wameshauriwa kuweka bei halisi kwenye zabuni za ujenzi badala ya kuweka gharama ndogo kwa lengo la kupata miradi ya ujenzi lakini mwisho wake wanakimbia kazi hizo.
Hayo yamesemwa mjini Dodoma na Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Consolata Ngimbwa wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kuhusu usimamizi wa mikataba ya ujenzi .
Amesema baadhi ya makandarasi wamekuwa wakiweka bei ndogo kwa lengo la kupata miradi lakini mwisho wa siku kazi hizo zimekuwa zikiwatesa na wengi kushindwa kuzikamilisha na kukimbia.
“Tuwe makini tunapojaza zabuni tuweke bei halisi kwasababu unakuta mradi wa sh milioni 400 mtu anaweka milioni 200 sasa kweli huu mradi utaukamilisha kwa namna gani? Unachukua mradi ilimradi tu umepata mradi lakini unakukondesha na hata usingizi hupati sasa inakusaidia nini,” amesema.
Aidha amewataka makandarasi kuisaini na kama wakishindwa kuielewa wawatumie wataalamu badala ya kuingia kwenye mikataba hiyo kichwa kichwa na kuwasababishia hasara kubwa inayowaletea msongo wa mawazo.
Kwa upande wake, mwezeshaji wa semina hiyo, Mhandisi Emmanuel Kachuchuru, amesema makandarasi wengi nchini hawajiamini na wanashindwa kutetea haki zao zinapokiukwa na wateja wao sababu kubwa ikiwa ni kutokuwa na ufahamu wa haki hizo kwenye zabuni.
Amesema kukosa elimu kuhusu usimamizi wa miradi kumewafanya makandarasi wengi kuwa wanyonge na kuonewa na watoaji wa zabuni hivyo aliwataka kuchangamkia mafunzo kila yanapotokea ili waongeze ujuzi na uwezo wa kulinda haki zao.
“Wengine wanaogopa kudai haki zao kwa kuogopa kuwa siku nyingine hatapata kazi, kama ulipata kazi kwa uwezo wako huwezi kuogopa. Ila kama ulipewa kazi ya ujenzi kwa njia za rushwa huna nguvu ya kudai kwasababu aliyekupa atakushangaa umepata wapi nguvu hiyo.
Amesema mara nyingi watoaji wa zabuni wamekuwa wakiwanyanyasa makandarasi ambao hawajui haki zao wala namna ya kuzitetea kwenye mikataba ya ujenzi tofauti na wale wenye uelewa na usimamizi wa mikataba ya ujenzi.
Aidha, amesema watoaji wa zabuni wamekuwa wakiwaogopa makandarasi wa kigeni kwani wanajua fika kwamba wanajua haki zao na wanauwezo mkubwa wa kuzidai kila zinapokiukwa.
“Niambieni lini mmesikia mkandarasi wa kigeni analalamikalalamika kama sisi? Ni kwasababu wanazijua na wana uwezo mkubwa wa kudai haki zao na vile vile hata hawa watoaji wa zabuni wanajua kwamba hawa ukiwagusa tu utapata shida, sasa nanyinyi mfike huko msikubali kuonewa,” amesema
Aidha, amesema asilimia 65 ya bajeti ya nchi inakwenda kwenye miradi ya ujenzi hivyo makandrasi wanapaswa kujua wajibu wao na kuisimamia kwa mujibu wa makubaliano ya kwenye mikataba wanayoingia na wateja wao.
“Miradi hii ya ujenzi ni mingi na inawapa fursa nyinyi ya kukua hivyo timizeni wajibu wenu kila mnapopata kazi na hakikisheni kila mtu anajua wajibu wake wewe na mwajiri wako ili mwisho wa siku kila mtu apate anachostahili,” amesema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...