Na. John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ameitaka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) na wadau mbalimbali wakiwemo wazalishaji wa muziki hapa nchini kutengeneza muziki wa kitanzania ambao utalitambulisha taifa la Tanzania duniani.
Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Februari 9, 2022 alipofanya ziara ya kikazi kwenye taasisi hiyo mjini Bagamoyo akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wake Dkt. Hassan Abbasi na Naibu Katibu Mkuu. Saidi Yakubu.
Amesema kutokana na ukongwe wa chuo hicho ni muhimu kikafanya kitu kikubwa ambacho kitasaidia kuutambulisha utamaduni wa Tanzania duniani na kutoa ajira kwa vijana wengi.
Aidha Mhe, Mchengerwa ameitaka Wizara yake kuanzisha kituo cha Televisheni na Redio kitakachokuwa na studio maalum ambayo itasaidia kuzalisha, kukuza na kunoa wasanii kutoka mitaani na vijijini nchi nzima, pia viongozi wa sanaa na wafanyakazi katika sekta ya utamaduni sambamba na kuzalisha kazi za sanaa pamoja na huduma za medianuai (multimedia).
Mkakati wa kusaka vibaji vya wasanii mtaa kwa mtaa nchi nzima ni jambo aliloliasisi Mhe. Mchengerwa mara baada ya kuteuliwa hivi karibuni kuiongoza Wizara hiyo ambapo sasa anataka kuanzishwa kwa kituo cha televisheni na redio ambacho kazi yake kitakuwa kikitangaza maudhui ya Utamaduni na Sanaa za kitanzania pia michezo mbalimbali ili kuuza utamaduni wa mtanzania kimataifa.
Aidha, Mhe. Mchengerwa ameelekeza TaSUBa kuanza mara moja maandalizi ya Tamasha la kimataifa la Sanaa na Utamaduni la mwaka huu ili liwe bora zaidi kuliko matamasha yote yaliyotangulia pia kutangaza utamaduni kama bidhaa ya utalii kimataifa.
“Naelekeza sasa tujipange kuanzia sasa kwa ajili kuandaa tamasha hili la kimataifa la utamaduni na sanaa na tushirikiane na wenzetu wa Wizara ya Mambo ya nje kulitangaza nje ya mipaka ya nchi yetu na tuwakaribishe wageni.” Amesisitiza Mhe. Waziri
Ameitaka Wizara yake ishirikiane na Wizara ya Utalii ili tuweze kuuza sanaa na Utamaduni nje ya Tanzania kupitia mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na matamasha ya utamaduni.
Akitolea mfano amesema TaSUBa inatakiwa kuwa wabunifu kwa kuandaa wa Tamasha la Utamaduni kama tamasha Masai nchini Uingereza na Marekani ili kuuza na kutangaza utamaduni duniani.
Amesema katika kipindi hiki atahakikisha masuala ya uzembe, rushwa, ubadhilifu hayana nafasi kwenye wizara yake ili kuleta mapinduzi ya haraka kwenye sekta anazozisimamia.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi ametumia tukio hilo kutangaza rasmi kuwa shughuli za TaSUBa zitakuwa zikisimamiwa kwa karibu zaidi ya Naibu wake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...