Adeladius Makwega,DODOMA
Wakaguru ni kabila linalofanya utani katika hatua mbalimbali kama yalivyo makabila mengine. Utani uliopo ni baina ya mtu na mtu, ukoo na ukoo na hata Wakaguru wa milimani na wale wa wabondeni yaani (Waitumba na Wamegi). Pia utani na makabila mengine kama nilivyokudokeza katika matini yangu ya kwanza
Utani katika kabila hili ni mkubwa mno, huku zikitajwa koo namna zinavyoweza kutaniana kama niliyokueleza kuwa ndugu hawa wapo katika makundi makubwa mawili.
Inaaminika kuwa wakati Wakaguru wanafika katika eneo hili walipo sasa Kilosa, Mpwapwa, Kongwa na hata baadhi ya maeneo ya Dodoma kulikuwa na ndugu wawili kaka na mdogo wake.K aka alikimbilia kuishi milimani ambaye alikuwa akifahamika kama Nanunda na mdogo mtu akifahamika kama Waluhanji aliyeishi jirani na vyanzo vya maji.
Kama ilivyo desturi ya eneo hili wanaloishi Wakaguru kila mara mafuriko yanawakumba hali hii ipo tangu enzi, huyu mdogo mtu aliyekimbilia kuishi jirani na vyanzo vya maji mafuriko yalimkuta na nyumba zake kusombwa na mafuriko hayo. Kaka mtu kwa huruma alimchukua na kumsaidia kumrudisha milima nduguye. Wakiwa milimani ilibidi waishi tena pamoja, udugu huo ulikuwa wa kuheshimina huku wakitaniana kuwa bila kaka mafuriko yangemmaliza mdogo mtu. Mafuriko hayo yakaleta utani baina ya Waitumba na Wameji tangu wakati huo hadi sasa.
Jambo la kustajabisha wakati wa ujio wa Wamsionari Wameji walikuwa wakwanza kuwapokea na kukaa vizuri na ndugu hao, jambo hilo liliwasaidia wao kuweza kupata huduma mbalimbali kama elimu na afya mapema lakini wale wa milimani Waitumba hali ilikuwa tofauti kabisa.
Hili liliwafanya Waimeji wajione wao ni bora ya Waitumba huku Waitumba wao wakijiona ndiyo Wakaguru halisi kwa kuwa hawakuingiliwa na utamaduni wa kigeni. Ugeni huu wa wamisionari uliongeza utani zaidi baina yao. Japokuwa hali hiyo sasa imepungua mno wengine wakiamini kutoweka kabisa kutokana na suala la maeandeleo kwa wote.
Pia utani wa Wakaguru unaonekana na makabila mengine, huu umejengwa katika mambo makubwa matatu makabila yaliyokuwa yakiwavamia na kuwachukua watumwa, ushirikina na yale makabila yaliyokuwa yanawaibia mifugo Wakaguru.
Miongoni mwa makabila hayo ni Wanyamwezi wa Tabora, Wanyamwezi walikuwa ni marafiki wakubwa wa Waarabu kwa hiyo walishirikiana nao katika kuwatafuta watumwa na hata kuwakamata wapagazi wa kubeba mizigo kutoka bara hadi pwani.
Inaaminika kuwa Mamboya ilikuwa ni sehemu ambayo Waarabu na Wanyamwezi walipita mno, inawezekana kuwa mpagazi anapofariki njiani ilibifdi kumtafuta mtu wa kuziba pengo la kubeba pembe za ndovu au hata mtumwa akifariki njiani, akipungua jambo hilo liliwafanya Waarabu na Wanyamwezi kuwakamata Wakaguru kuziba pengo hilo.
Wakaguru kutokana na biashara hii ya watumwa kuwa hivyo kwao ilikuwa ni biashara haramu na ya kihuni ambayo iliwakwaza mno na hili liliwafanya Wakaguru kuwachukia mno Wanyamwezi kwa kushirikiana na Waarabu.
Chuki hiyo ikahamishiwa kwa Wanyamwezi kwani lilikuwa ni kabila lisilofanya tohara ya wanaume, jambo hilo liliwafanya Wakaguru kuwadharau zaidi Wanyamwezi nakulitazama kama ni kabila duni wakati Wakaguru walikuwa wakifanya tohara hiyo ya wanaume.
Mambo haya mawili biashara ya utumwa na tohara ya wanaume ndiyo yakawa ufunguo wa utani baina ya Wakaguru na Wanyamwezi. Wakaguru wakiwaambia Wanyamwezi kuwa nyinyi mlikuwa hamuendi jandoni wakati Wakaguru wakiambiwa kuwa nyinyi tulikuwa tunawakamata na kuwapeleka watumnwa. Utani ukaibuka na hapo wakaishi kama ndugu hadi sasa.
Kabila lengine lenye utani na Wakaguru ni Wangulu, Wangulu (Nguu ) walishiriki pia katika biashara ya utumwa kwa kuwavamia Wakaguru, ndugu hawa kwa asili walikuwa wakikaa eneo lenye miti mingi ya miyombo na jambo hilo likawafanya Wakaguru kuwatambua Wangulu kama Wayombo.
Kwa faida ya msomaji wa matihi haya, yapo baadhi ya maeneo katika Tanzania yetu yanaitwa Yombo (Miyombo) Kongowe (Mkongowele) na kadhalika haya ni majina kutokana na miti iliyokuwa inapatikana maeneo hayo kama alama.Hii nakupa kama zawadi msomaji wangu.
Wakaguru waliwatazama Wangulu kama kabila llinalojihusisha mno na ushirikina na kwa hiyo Wakaguru waliwaogopa mno Wangulu, moja kwa kuwavamia na kuwakamata utumwa huku wakitumia silaha kama bunduki walizopata kwa Waarabu, pili Wangulu kama washirikina, mambo hayo yaliwanyima raha kabisa Wakaguru.
Kabila la tatu na mwisho ambalo wanataniana na mno na Wakaguru ni Wamasai hawa jamaa walikuwa na desturi ya kuwavamia Wakaguru si kwa nia ya kuwapeleka utumwa la hasha bali kuwaibia ng’ombe zao na kutoweka nazo kabisa. Jambo hilo lilikuwa ni mchezo mchafu kwa Wakaguru na kuwachukia Wamasai kama ilivyokuwa wa Wanyamwezi na Wangulu, haya yanathibitishwa na ndugu D.Z Mwaga katika maandishi yake ya Mahusiano ya Utani kwa Wakaguru.
“Wamasai ni kabila ambalo linalofanya tohara tangu enzi huku namna wanavyotahiri huwa wanaondoa ngozi ya mbele ya uume lakini sehemu ya ngozi hiyo huiacha ikining’nginia kwa chini. Wakaguru wao pia hufanya tohara kwa wanaume kwa kuiondoa ngozi yote ya mbele ya uume na kuitupilia mbali. Hizo ni namna mbili tofauti za kutahiri kwa Wamasai na Wakaguru.” Anasema D.Z Mwaga.
Wakaguru walienda mbali kwa kuwatania Wamasai kuwa kuwa namna tohara inavyofanyika siyo tohara kamili bali ile yao Wakaguru ndiyo tohara timilifu. Jambo hilo mwanzoni lilikuwa ni utani ulioleta ugomvi mkubwa lakini baadaye likajenga udugu baina ya makabila haya mawili, maana waswahili wanasema wale wagombanao, ndiyo wapatanao.
Hoja kuwa nyie tunawaibia ng’ombe na hoja kuwa nyie tohara yenu si tohara kamilifu yalikuwa ya kawaida na jambo hilo likaibua utani baina ya Wakagurtu na Wamasai hadi sasa.
Kwa hoja hiyo ya utafiti wa D.Z Mwaga juu ya ipi tohara bora baina ya Wakaguru na Wamasai ambayo ilileta utani baina yao,ndivyo na mimi mwanakwetu nafika tamati ya matini haya kwa leo.
Nakutakia siku njema
makwadeladius@gmail.com
0717649257
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...