Na John Walter-Babati
Wananchi wenye ardhi katika mtaa wa Nangara Ziwani kata ya Nangara halmashauri ya mji wa Babati wametakiwa kujitokeza kuchangamkia fursa ya urasimishaji unaofanyika katika maeneo yao wakati wa utekelezaji wa mradi wa urasimishaji Ardhi katika eneo hilo, unaotekelezwa kupitia ofisi ya rais MKURABITA.
Mtaa wa Nangara Ziwani umekuwa wa kwanza katika mkoa wa Manyara kufikiwa na ofisi ya Rais, Mpango wa kurasimisha rasilimali na biashara za wanyonge Tanzania (MKURABITA) kurasimishiwa ardhi zao na kupatiwa hati Miliki.
Baadhi ya wananchi walionufaika na mradi huo wamesema fursa hiyo imekuja kwa wakati kwani walikuwa wakifuata hati zao umbali mrefu hivyo zoezi hilo kusogezwa karibu ni msaada kwao.
Zainabu Bakari amesema baada ya kukabidhiwa hati hiyo amesema licha ya kuepuka migogoro kupitia hati hiyo lakini pia ataweza kukopa fedha ili afanye biashara na kujikwamua kichumi.
Mratibu wa MKURABITA halmashauri ya mji wa Babati Japhary Shemashiu
Meneja Rasilimali ardhi mijini kutoka ofisi ya Mpango wa kurasimisha rasilimali na biashara za wanyonge Tanzania (MKURABITA) Mwesigwa Mwijage, amesema rasilimali ambayo mwananchi anayo ni ardhi pekee ambapo kwa asilimia kubwa haipo rasmi (haijapimwa) huku ikiwa haina msaada wowote pindi tatizo linapotokea.
Mwijage amewataka wananchi wote ambao tayari ardhi zao zimerasimishwa wafike katika ofisi za ardhi katika halmashauri zao kupata hati.
Hata hivyo amesema zoezi hilo katika mtaa wa Nangara Ziwani limekuwa na mwitikio mdogo ambapo kati ya viwanja 500 vilivyopimwa zaidi ya hati 300 na zaidi hazijalipiwa licha ya huduma kusogezwa katika ofisi za mtaa.
Aidha Mwesigwa ameelezea faida za urasimishaji ni pamoja na kuondoa migogoro ya ardhi, kumiliki ardhi kisheria ukiwa na kumbukumbu halali na hatimaye kupata hati, ardhi inapanda thamani ikiwa imepangwa na kupimwa, inainua maisha ya watu kwa kuweza kupata mikopo na pia kama dhamana kwa lolote.
Onesmo Munuo kutoka ofisi ya kamishna wa ardhi mkoa wa Manyara amesema umiliki wa ardhi ni kuwa na hati miliki bila hivyo ni kujidanganya."Nyie Nangara ndo kioo katika mkoa wetu,msituangushe,endeleeni kulipia ankara zenu ili muweze kupata hati,huwezi kusema una kiwanja na hauna hati, utakuwa nacho tu, anaweza kuja mtu mwingine akatengeneza hati na ukaonekana hauna haki"alisema Munuo
Aidha amesema gharama za hati ni kuanzia laki moja hadi laki na thelathini.
Mkuu wa idara ya ardhi na mipango miji halmashauri ya mji wa Babati Mathias Mkumbo ameishukuru serikali kwa kuipatia idara hiyo shilingi Milioni 230 kwa ajili ya kupima maeneo ya wananchi katika mtaa wa Nangara na Sawe huku mchakato wa kumpata mzabuni kwa ajili ya kuanza kazi hiyo unaendelea.
Amewataka wananchi wa Nangara kutumia vyema fursa waliyoipata kutoka ofisi ya Rais huku akiongeza kwamba ardhi ikitumika vizuri inaweza kupunguza au kumaliza kabisa umasikini.
Wananchi hao wamekiri kupata muamko mkubwa, kutokana na elimu waliyopewa na watalamu pamoja na gharama nafuu za urasimishaji, kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakimilki maeneo yao bila vibali maalumu vya serikali kwamba zoezi hilo litasaidia kuondoa migogoro ya ardhi iliyokuwa inajitokeza kutokana na udanganyifu uliokuwa unafanywa na watu wasio waaminifu na kwa kuchukulia kigezo cha uelewa mdogo wa watu wengi.
Halmashauri ya mji wa Babati inaendelea na zoezi la urasimishaji ardhi katika kijiji cha Nangara ambapo jumla ya viwanja 500 vimepimwa na kurasimishwa huku wamiliki hao wakiendelea kupatiwa hati miliki zao baada ya kulipia gharama zinazohitajika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...