Asikitishwa na Kauli yake
Na Mwandishi Wetu.
MBUNGE wa Muheza, Hamis Mwinjuma, almaarufu MwanaFA amesikitishwa na kauli ya kumshambulia binafsi, iliyotolewa na Msemaji wa Shirikisho la Baraza la Muziki nchini Steven Mengele.
Mbunge huyo alisema kitendo alichofanya jana Stev Nyerere kwenye mkutano wake na waandishi wa habari ni kumkejeli binafsi, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mamlaka zilizompitisha kuwa mbunge lakini pia amewadhalilisha wananchi wa Jimbo la Muheza.
Alisema amesikitishwa na kauli hiyo kwasababu Steve Nyerere, amesema uongo mbele ya jamii, amevikosea heshima vyombo vilivyompitisha ikiwemo vikao vya juu vya CCM, lakini pia amemshambulia binafsi wakati katika taarifa yao hawakumtaja bali walikosoa ukiukwaji wa taratibu za kikatiba uliofanywa na Shirikisho hilo.
"Sisi hatukumsema yeye, tuliwasema viongozi wa Shirikisho kwamba wamevunja katiba kwasababu nafasi ya usemaji haipo katika katiba, sasa mtu waliyempa cheo hicho wamekitoa wapi?" alisema MwanaFA na kuongeza,
"Yeye (Nyerere) hakujibu hoja yoyote kati ya hoja ambazo sisi tumezitoa, kwanza haikuwa kazi yake kujibu kubishana na sisi, yeye alienda pale asiseme hoja yoyote badala yake ananishambulia mimi binafsi,".
Alisema haikuwa sahihi kushambuliwa maana amevikejeli vikao halali vya chama vilivyokaa mwaka 2020 mbavyo viliteua wagombea mbalimbali akiwemo yeye (MwanaFA) na kwamba Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama, wakati huo.a
"Nafikiri alichofanya siyo sahihi kunishambulia mimi binafsi, pia amezikejeli mpaka vikao halali vya chama vinavyotumika kuteua wagombea ambavyo wakati huo mwaka 2020 hata mama Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano) yupo kama mjumbe wa Kamati Kuu kwahiyo amevikejeli vikao na amesema vitu vingi vya uongo kusema ukweli," alisema.
Hata hivyo, MwanaFA alisema wanasubiri malalamiko yao ya hoja za msingi walizozitoa zitakapopatiwa majibu na Shirikisho hasa watakapoiondoa nafasi ya usemaji ambayo kimsingi haipo katika katiba.
"Kisha tutauliza kwa Shirikisho maneno aliyosema Steve Nyerere, wamemtuma aseme hivyo," alisema MwanaFA bila kufafanua hatua atakazochukua mara baada ya majibu ya shirikisho.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...