Na Shamimu Nyaki- WUSM, Dodoma

Serikali kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bodi ya Filamu na Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) imefanikiwa kuzindua mifumo ya kidijitali ya Usajili na utoaji wa vibali kwa wasanii na wadau wengine wa sanaa unaojulikana kama Artist Management Information System (AMIS) ambao unarahisisha kukamilisha hatua zote za kujisajili, kulipia vibali na kupokea vyeti vya kutambuliwa wakiwa popote walipo nchini au nje ya nchi.

Hayo yalielezwa Machi 16, 2022 Mtumba jijini Dodoma na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akiwasilisha taarifa ya Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, ambapo amesema kuwa lengo ni kuboresha na kurahisisha ufanyaji kazi wa wadau wa sekta hiyo.

“Kupitia Taasisi ya Haki Miliki Tanzania (COSOTA), ikiwa ni baada ya takribani miaka minne, imelifanyia kazi suala la mirabaha ya wasanii na kuongeza mapato ya mirahaba kutokana na makusanyo ya maonesho kwa umma na utangazaji yaliyofanyika kati ya zaJulai 1 hadi Disemba 31, 2021, ambapo jumla ya Shilingi milioni 312.29 zilikusanywa na kugawanywa. Hiki ni kiasi kikubwa kuwahi kugawiwa ambapo kazi za Sanaa 5,924 zilizofuzu vigezo vya kupata mirabaha ambapo jumla ya wasanii 1,123 walinufaika” alisema Mhe. Mchengerwa.

Mhe. Mchengerwa aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja, Bodi ya Filamu imefanikiwa kutoa Tuzo za filamu zilizofanyika mwezi Desemba jijini Mbeya, huku Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) tayari limepokea jumla ya kazi 1,360 za wasanii mbalimbali wapatao 536 nchini kwa ajili ya Tuzo za Muziki ambazo mchakato wake unaendelea na utajumuisha kusanyiko la tuzo za manguli mbalimbali wa tasnia ya muziki yaani “Award Academy” ambayo haijawahi kutokea katika historia ya tuzo zozote za muziki.

Fauka na hayo, Mhe. Mchengerwa ameeleza kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi Tanzania (KISUVITA) imefanikiwa kuratibu na kukamilisha mashindano ya urembo na mitindo kwa Viziwi yaliyofanyika mwezi Agosti 2021, ambapo Watanzania sita kati ya washiriki 74 kutoka zaidi ya nchi 15 za Afrika walifikia vigezo vya kushiriki mashindano ya dunia yaliyokuwa yamepangwa kufanyika nchini Brazil, hata hivyo baada ya Tanzania kuonesha ufanisi katika mashindano hayo ngazi ya Bara la Afrika, imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Mashindano hayo ya dunia yenye washiriki zaidi ya 300 yanatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2022 .


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...