Na Mwandishi wetu, Dodoma
TANZANIA na dunia inapoelekea kuadhimisha siku ya wanawake duniani, tudurusu kidogo juhudi zinazofanyika hapa nchini katika kuwainua wanawake katika sekta ya madini hasa kwa kuangazia ujumbe muhimu uliojitokeza wakati wa Mkutano Mkuu wa 24 wa Chama cha Wanawake wachimba Madini Tanzania (TAWOMA) uliofanyika jijini Dodoma hivi karibuni.

Kilichosisitizwa zaidi ni umuhimu wa kuimarisha ajenda ya usawa na ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo nyeti kwa uchumi wa Tanzania. Mengi yalisemwa lakini kubwa ni nia iliyoonyeshwa na serikali na wadau toka sekta binafsi katika kutekeleza wa lengo hilo.

Lengo kuu la mkutano huo uliohudhuriwa na jumla ya wawakilishi 112 kutoka matawi yote ya TAWOMA nchini lilikuwa lilikuwa kuzungumzia namna ya kuboresha mazingira migodini na kuimarisha ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini ili kuchangia kipato chao na maendeleo ya taifa.

Akielezea umuhimu wa nafasi ya wanawake katika uchumi, mgeni rasmi, Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Doto Biteko alisema kutokana na idadi ya wanawake kuzidi wanaume kwa mujibu wa takwimu za sensa ya mwaka 2012, watendaji wa sekta ya madini watakuwa wanatenda kosa kubwa ikiwa mipango wanayopanga itawaweka kando wanawake. Alisema sifa za mwanamke zimeelezwa hata katika vitabu vya dini. Alisema wanawake ni waaminifu, sio wabinafsi, wenye kuweza kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, wenye kujali na wazazi.

“Katika mamia ya watu waliokamatwa wakitorosha madini kwa muda wote niliokaa Wizarani kama kiongozi, wanawake waliowahi kukutwa na kosa hilo ni wawili tu,” Waziri Biteko alitoa mfano akisisitiza kuwa haamaanishi kuwa kuwa wanaume sio waaminifu.

Alisema ili kupiga hatua katika sekta ya madini, ni muhimu sasa kuondokana na imani ya kihistoria kwamba kazi ya uchimbaji madini ni kazi ya wanaume pekee. Aliongeza kuwa imani ya kwamba kazi ya wanawake katika sekta hiyo ni ile ya kugongagonga mawe peke yake, au kusimamia tu na si kuwa wamiliki wa leseni, au kuwa wahasibu tu na si kuwa wanunuzi na kuwa watoa huduma ndogondogo tu kama vinywaji na chakula lazima sasa ibadilike.

“Kundi la wanawake likiingia katika sekta ya madini, jamii nzima itakuwa imefaidika,” alisema na kufafanua kuwa chochote watakachopata wanawake sio tu watalipa kodi, bali watawekeza katika familia zao.

Alisema wanawake wanapaswa kuwa vinara na kuwa dhambi kubwa ambayo wanatakiwa waichukie ni kujiona duni na badala yake wajione wanaweza kufanya mambo. Alisisitiza kuwa wanawake wa Tanzania wasikubali na wala wasiridhike kwamba wakati mpira unachezwa uwanjani, wao kazi yao iwe kukaa nje ya uwanja na kuokota mipira inayotoka nje na kuwarudishia wachezaji uwanjani.

Alisema yeye kama Waziri na watendaji wengine wizarani wanataka kuona wanawake wanakuwa mstari wa mbele na kufanya vizuri katika kazi zote kwenye mnyororo mzima wa biashara ya madini kuanzia utafiti, uchimbaji, uongezaji thamani na ukataji madini.

“Tuko tayari kuwasikiliza na tuko tayari kukosolewa,” alisema.

Katibu wa TAWOMA, Bi. Salma Ernest alieleza kuwa Chama kina mikakati ya kuhakikisha kinaunganisha Wanawake wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa madini ili kuwa na lugha moja katika kujiletea maendeleo, kufanya kazi kwa kufuata sheria za madini na kuhakikisha kila mmoja analipa kodi kwa misingi na taratibu zilizowekwa na Serikali.

Bi. Salma alipendekeza kuanzishwa kwa mfuko maalumu utakaowezesha wanawake walio kwenye mnyororo wa thamani wa madini na walio kwenye mazingira magumu ya uchimbaji na masoko hasa maeneo ya vijijini na pembezoni mwa nchi waweze kupata utaalamu, nyenzo na masoko ya uhakika pamoja na kuwatafutia wafadhili na wanunuzi wa uhakika wa madini yao.

Ili kudhihirisha ushirikiano wa serikali na sekta binafsi katika kuwainua wanawake katika sekta ya madini, matukio makubwa mawili yalishuhudiwa katika mkutano huo. Moja ilikuwa ni utiaji saini wa makubaliano kati ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na benki ya CRDB yenye lengo la kujenga uwezo kwa wachimbaji wadogo wanawake Tanzania hasa katika eneo la mikopo ili kukuza mitaji yao. Pili, ilikuwa ni uzinduzi wa mradi wa WORTH YETU.

Bw. Prosper Nambaya, Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa na Serikali katika benki ya CRDB, alieleza kuwa wao kama wadau kutoka taasisi za kifedha wanauona ushirikiano unaojengeka na serikali kupitia STAMICO katika kutatua changamoto za wachimbaji wadogo kama kitu muhimu sana.

“Pawe na vyama vya majaribio kama ilivyo kwenye vyama vya kilimo. Vyama vya wachimbaji wadogo viwe na uongozi, katiba na mahesabu rasmi, akaunti za benki na mfumo unaoeleweka,” alisisitiza.

Akitoa maelezo mafupi kuhusu mradi wa WORTH YETU, Mkurugenzi wa Shirika la PACT Tanzania, Bi. Marianna Balampama alisema mradi huo ni muendelezo wa ushirikiano kati ya shirika hilo na TAWOMA ulioanza 2017 katika kuongeza uwezo wa kina mama wachimbaji hasa katika kujiendeleza kiuchumi na ujuzi. PACT Tanzania na TAWOMA waliandika andiko na kuliwasilisha Benki ya Dunia na kupata ruzuku iliyozinduliwa katika tukio hilo.

Ruzuku hiyo ina malengo makuu matatu: kwanza, kuongeza uwezo wa kina mama wachimbaji kiuchumi kwa kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa ambapo watapata elimu ya fedha. Pili, kupanua zaidi masoko ambayo yamekuwa yakiendeshwa na shirika hilo kwa kushirikiana na TAWOMA katika mkoa wa Tanga na mikoa mingine.

Tatu, kujenga uwezo wa TAWOMA kuwa taasisi imara na endelevu. Alisema kwa mara ya kwanza, TAWOMA wamepatiwa ruzuku hiyo ambapo watatumia fedha hiyo na kuripoti kwa PACT Tanzania tofauti na zamani ambapo fedha ilikuwa ikitunzwa na PACT Tanzania.

“Tunatamani kuiona TAWOMA ikikua. Sisi kama wadau tutaendelea kusimama na serikali katika kusukuma mbele sekta hii,” alisema Bi. Marianna.

Bw. Tuna Bandoma, Meneja, Wachimbaji Wadogo, STAMICO alieleza kuwa utoaji mafunzo kwa wachimbaji wadogo wakiwemo wanawake ni kipaumbele cha serikali ili kuwawezesha na kuwajengea uwezo kufanya kazi zao za uchimbaji, uongezaji thamani pamoja na biashara ya madini kwa ufanisi na weledi zaidi. Alisema katika hilo, STAMICO imeshaandaa mwongozo wa mafunzo kwa wakufunzi wote wanaohusika na utoaji mafunzo kwa wachimbaji wadogo nchini.

Bi. Sophia Mwanauta, mchimbaji mdogo wa dhahabu Chunya, Mbeya alitoa wito kwa STAMICO kusaidia wanawake kupata taarifa za kijilojia kwa urahisi kwani wengi wao huingiza mitaji mikubwa katika shughuli za uchimbaji bila kuwa na taarifa hizo muhimu na kupelekea shughuli hizo kutokuwa endelevu. Alitoa wito kwa serikali kutoa kipaumbele kwa wanawake pindi maeneo ya wachimbaji wadogo yanapotengwa.

Mkurugenzi wa STAMICO, Dkt. Mwasse alisema STAMICO iko tayari kufanya kazi na wadau wengine kama PACT Tanzania ili kuifanya TAWOMA kuwa kubwa, endelevu na chombo chenye manufaa kwa wengi. “Katika dhana nzima ya uchumi jumuishi, ukiigusa TAWOMA unakuwa umetekeleza jukumu hilo kwa vitendo,” alisisitiza Dkt. Mwasse.
Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Doto Biteko akisikiliza maelezo alipotembelea mabanda ya maonyesho wakati wa Mkutano Mkuu wa 24 wa Chama cha Wanawake Wachimba Madini (TAWOMA) mjini Dodoma hivi karibuni.
Mkurugenzi Mkuu wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse (wa pili kushoto) na Bw. Prosper Nambaya, Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa na Serikali CRDB Bank wakibadilishana nyaraka baada ya makubaliano ya pande hizo mbili ya kuwainua wachimbaji wadogo wakati wa Mkutano Mkuu wa 24 wa Chama cha Wanawake Wachimba Madini (TAWOMA) mjini Dodoma hivi karibuni.
Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiteta jambo na akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa TAWOMA, Bi. Rajah Gilly (kulia kwa Waziri) na Mkurugenzi wa PACT Tanzania, Bi. Marianna Balampama (kushoto kwa Waziri) baada ya uzinduzi wa WORTH YETU wakati wa Mkutano Mkuu wa 24 wa Chama cha Wanawake Wachimba Madini (TAWOMA) mjini Dodoma hivi karibuni.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...