Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kuwa jamii inahitaji kuyatumia mafunzo ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ili kujenga umoja, maridhiano na mshikamano miongoni mwa watu hapa nchini, licha ya changamoto mbali mbali za kimaisha zinazowakabili wananchi.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo jana, katika Kijiji cha Ndijani Mseweni, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, wakati wa Iftar Maalum, aliyoiandaa kwaajili ya wanakijiji hicho na wananchi mbali mbali wa maeneo ya karibu.

Amesema kuwa mikusanyiko yote inayofanyika, kuanzia iftari za pamoja, mashindano ya Qur-an Tukufu na kuwatembelea wenye mazingira magumu wakiwemo wazee wasiojiweza, wagonjwa na watu walioondokewa, licha ya kulenga katika malengo mengine, dhamira yake hasa ni kujenga umoja, ambao hapana-budi kuuendeleza, hata baada ya kwisha kwa Mfungo wa Ramadhani.

Mheshimiwa Othman ameeleza kuwa pamoja na hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi, umoja na mshikamano ni mambo yanayohitaji kuendelezwa, ambapo azma hiyo itawezekana kupitia juhudi za makusudi katika kusaidiana.

“Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, tunafunzwa kuwa pamoja na kutafuta fadhila bali ndani yake mna mambo matukufu na moja kati ya hayo ni hili la kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwa watu katika jamii hata katika maisha baada ya Ramadhani”, alisisitiza Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo–Zanzibar.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ndugu Rashid Hadid Rashid, amesema kuwa hafla hiyo ni yenye umuhimu wa kipekee, ni faraja kwa wananchi wake, na pia alama muhimu ya umoja, mshikamano na mwenendo wa maridhiano mema, katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Naye, Mzee Ame Rajab (76), akitoa salamu za shukrani kwa Mheshimiwa Othman na viongozi mbali mbali waliojumuika katika hafla hiyo, ametoa wito kwa wananchi kushukuru kwa namna ya kipekee kutokana na tukio hilo muhimu la kihistoria.

Alisema kuwa hiyo ni kutokana na ukweli kwamba, kwa kipindi chote cha uhai wake, haijawahi kutokea kwa Kiongozi ‘mwenye bendera’ na wa hadhi ya juu, kujitokeza kukaa pamoja nao, kula na kunywa na wananchi wa kijiji hicho au maeneo ya jirani, hali ambayo inamlazimu, yeye na wenzake, kuichukulia hafla hiyo kuwa ni maalum na heshima ya kipekee.

Katika iftar hiyo, Mheshimiwa Othman aliyeambatana na familia yake, alijumuika na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Jamii, Masheha wa baadhi ya Shehia, Vyama vya Siasa, na Vikosi vya Ulinzi na Usalama, ambao ni pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kusini Unguja, Bw. Salim Kassim Ali.


Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
17/04/2022










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...