Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari wa zamani Marehemu Kanyama Chiume (kushoto) na Marehemu Robert Makange(kulia) katika viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam mwaka 1985 siku chache kabla ya Baba wa Taifa kustaafu Urais.
Mzee Robert Makange (1928-1999)
Huyu kwa Watanzania wengi anafahamika zaidi kama muasisi wa mlo wa kuku wa kukaanga katika Bar yake ya Tropicana Club aliyokuwa akimiliki mtaa wa Nkrumah, jirani na Bustani ya Mnazi Mmoja upande wa kusini, ambapo zamani palikuwa ni makao makuu ya chama cha Umoja wa madereva teksi cha Co-Cabs. Umaarufu wa "Kuku wa Makange" ulijulikana ndani na nje ya nchi kiasi kwamba hadi hii leo jina hilo limekuwa likitumika ama kujulikana na karibu kila mtu nchini kama aina fulani ya mlo mtamu wa kuku wa kukaanga.
Lakini ni wachache wanaojua kwamba Mzee Makange alikuwa mmoja wa wanaharakati wafanyabiashara wakubwa waliopigania Uhuru. Yeye alikuwa mwandishi na mhariri wa gazeti la "Mwafrika" kati ya mwaka 1957 hadi 1961. Gazeti lao walikuwa wakilichapa kwenye kiwanda chao cha uchapaji cha Pan African Publishing House waliyokuwa wakiendesha yeye, Mzee Chiume na Mzee Kheri Rashidi Baghelleh hapo hapo Tropicana Club kwa nyuma.
Gazeti hilo lilifanya kazi kubwa ya kueneza siasa ya TANU ya kudai Uhuru. Mwaka 1958, Marehemu Mzee Makange pamoja na mmiliki mwenzake, Kheri Rashidi Baghelleh, walifungwa miezi 6 na Serikali ya mkoloni kwa tuhuma za uchochezi.
Maandiko ambayo yaliwapeleka jela ni haya hapa:
"Sisi wote tunajua kuwa Mwingereza yupo hapa kwetu kwa sababu ya kutunyonya damu na kujipatia manufaa yake mwenyewe, na wala asitudanganye kwamba yupo hapa kwakuwa anatuonea huruma na kutaka kutufundisha ustaarabu au kuleta maendeleo ya nchi.
Maneno haya ni kigeugeu cha kutaka kutufunika macho; na kwa kadri atakavyozidi kuwa hapa ndivyo madini na fedha zitakavyozidi kutolewa katika nchi hii kupelekwa kwao, ambako bila ya sisi hawawezi kuishi sawasawa.“
(Mwafrika [weekly edition], No. 19, June 1st 1958, p. 5)
Mzee Makange pia alikuwa ni mtunzi wa vitabu mbali mbali kupitia kampuni ya uandishi na uchapaji ya Pan-African Publishing Company aliyoiongoza kwa miaka mingi pamoja na rafiki yake wa karibu, Mzee Kanyama Chiume.
Mzee Kanyama Chiume
Huyu alipata kuandikia magazeti ya Serikali ya "Nationalist" (ambalo baadaye likawa "Daily News/Sunday News") pamoja na magazeti ya Chama ya "Uhuru na Mzalendo" kuanzia miaka ya 1960 hadi ya 1980. Vile vile Mzee Chinyama alikuwa columnist (mwandishi wa makala) katika magazeti mbali mbali nchini katika miaka ya 80 hadi 90.
Kabla ya hapo Mzee huyu alipigania Uhuru wa Malawi na kupata kushikilia nafasi mbali mbali za uongozi nchini humo, kama vile kuwa Waziri wa kwanza wa Elimu na Waziri wa kwanza wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, kabla ya kukimbilia uhamishoni Tanzania ambako aliishi kati ya mwaka 1964 na 1994. Hiyo ikiwa ni baada ya kukiudhi chama tawala cha Malawi Congress Party chini ya "Rais wa Maisha" Hastings Kamuzu Banda.
Mzee Chinyama alirejea tena Malawi mwaka 1994 kufuatia shinikizo la ndani na la kimataifa alilopewa Rais Banda. Hapo alifanya kazi kwa muda kama Mwenyekiti wa Huduma za Maktaba za Taifa na Malawi Book service kabla ya kustaafu na kuhamia New York, Marekani akiwa na familia yake. Alifariki dunia Novemba 21, 2007. BOFYA HAPA https://issamichuzi.blogspot.com/2007/11/mzee-kanyama-chiume-katutoka.html
Mabaki ya mwili wake yalirejeshwa Malawi Novemba 29, 2007 ambako alizikwa kwa heshima zote za kitaifa. Aliyekuwa Rais wa Malawi wakati huo, Bingu wa Mutharika, aliongoza maziko hayo
Vile vile, alikuwa Msuluhishi wa kwanza wa mgogoro wa kisiasa huko Zanzibar kati ya ASP na ZNP chini ya usimamizi wa PAFMECA.
Mzee Chinyama Alikuwa muumini mkubwa wa falsafa ya "Pan-Africanism" na mtunzi wa vitabu mbali mbali na mwanaharakati wa demokrasia nchini Malawi dhidi ya utawala wa kidikteta wa Rais wa Maisha wa wakati huo, Kamuzu Banda.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...