Adeladius Makwega-TANGA

Katika siku kadhaa nimekuwa nikiona picha za vijana wanaokimbiza Mwenge wa Uhuru na nimekuwa nikifuatilia maoni juu ya mwenge huo kila unapopita. Huku nikijiuliza Je kweli Julius Nyerere na wenzake walipoanzisha dhana na Mwenge wa Uhuru nia yao ilikuwa mwenge huu ulalamikiwe kama unavyofanyiwa sasa?

Je huko ni kuwatendea haki ndugu hawa au wazo lao ililikuwa halina tija yoyote kwa taifa letu?Je mzigo huo wa lawama ni wa vijana wanaoukimbiza mwenge huo, wizara inayosimamia au CCM yenye serikali hiyo?

Lawama dhidi ya Mwenge wa Uhuru mara zote nilichobaini zimekuwa ikitwikwa kichwani CCM japokuwa makosa hayo huwa haifanyi yenyewe. Mara zote kwenye mwenge CCM huwa ni mwalikwa tu.

Nakumbuka, mwaka 2019 Mwenge wa Uhuru ulizinduliwa katika mkoa wa Songwe vizuri sana na Mgeni Rasmi alikuwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan. Baadaye vijana waliokuwa wanaukimbiza walianza kazi hiyo katika wilaya ya Mbozi. Wilaya hiyo ilikuwa na miradi zaidi ya mitano.

Katika siku hiyo ya kwanza kati ya miradi hiyo miradi mitatu ilikataliwa likiwamo Daraja Moja la TARURA, Darasa Moja la ELIMU SEKONDARI na Zahanati Moja ya AFYA. Msomaji wangu naomba mradi wa barabara na darasa iwekwe kando nikusimulie simulizi ya mradi mmoja tu uliokataliwa wa Zahanati ya Igunda,

Kijiji cha Igunda kilikuwa hakina zahanati kwa miaka mingi huku wanakijiji wake wakipata hisani ya kutibiwa katika vijiji vingine ndani ya kata ya Mlowo ambao ni mji mkubwa wa Kibiashara katika mkoa mpya wa Songwe uliopo kandokando ya barabara kubwa ya kwenda Tunduma mpakani mwa Tanzania na Zambia.

Wananchi walihamasishwa na wakaitika vizuri na kuweza kujenga zahanati hadi kiwango cha upauwaji, hapo serikali ya wilaya ikaongeza fedha za kumalizia hiyo zahanati huku mfanyabiashara mmoja anayejulikana kama MARMO GRANITES akajitolea malumalu nyingi kuukamilisha mradi huo kwa ubora zaidi.

Wakati huo tayari madirisha ya aluminiamu yalikuwa yamepachikwa vizuri na jengo kuwa limekamilika kwa kiwango cha juu kabisa. Binafsi sikuwahi kuona zahanati bora kama hiyo kwa mjini na hata kijijini.

Serikali ya wilaya ikapeleka watumishi, dawa na vifaa tiba ili Mwenge ukizindua huduma ziendelee.Wananchi wa eneo hilo ambao wengi walikuwa wanaunga mkono siasa za upinzani wakiongozwa na CHADEMA walishirikiana vizuri na CCM kukamilisha kazi hiyo. Eneo hilo lilikuwa na diwani na CHADEMA na mbunge wa CHADEMA.

Wananchi wa kata hii ambao wengi walikuwa Wanyia na Wanyakyusa wakiwa ndugu wa damu waliondoa tofauti zao za kisiasa za uchaguzi wa mwaka 2015 na kuwa kitu kimoja katika maendeleo.

Mara baada ya Makamu wa Rais kuondoka tu Mwenge ukaondoka uwanjani hadi Igunda wakimbiza mwenge walipofika hapo wakaukagua mradi, mwisho wa siku wakakataa kufungua mradi huo.


“Siufungui mradi huu, upo chini ya kiwango.”

Alisema kiongozi wa wakimbiza mwenge.

Wananchi waliguna mmmmmm! wakazima muziki ikawa kimya watu wakaanza kurudi majumbani mwao.

Mimi nilikuwa jirani na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Mbozi anaitwa Mzee Mboya. Huyu ni mtumishi wa umma mstaafu. Kwa bahati nzuri Mzee Mboya anazaliwa kata ya Mlangali, hii ni kata yenye Kimondo cha Mbozi, Mlowo na Mlangali ni kata jirani sana, hata kwa mguu unaenda na hawa wote ni ndugu kabisa wa damu.

Nikiwa jirani na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya, akaja mtu mmoja jirani yetu kabisa akamsalimia kwa Kinyia alafu akasema maneno haya,

“Si mnaona CCM mambo yenu yalivyo? Mwenyekiti!, Yaani sisi kujituma kote kule leo anakuja mtu anaukata mradi wetu?Eti Siufungui mradi huu, upo chini ya kiwango! Kweli mradi huu utafanya kazi ? ”

Hata mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Mbozi na yeye hakulidhishwa na mradi ule kukataliwa lakini alitumia hekima kukaa kimya, mimi nikamjibu ndugu yule kuwa mradi huu umeshaanza kufanya kazi leo hii na utaendelea kufanya kazi, kama kutakuwa na maagizo mengine yatapokelewa. Binafsi pale nilijibu kwa niaba ya Serikali nilikuwa mtu sahihi kulijibu swali hilo wakati huo.

Mwanakwetu Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya alibebeshwa mzigo mzito wa lawama kwa maamuzi ya mkimbiza Mwenge.Yule aliyeuliza alikuwa ni kiongozi wa CHADEMA wa kata huku alikuwa amevalia skafu ya chama hicho.

Mwenyekiti Mboya akaniambia kuwa jambo hili limeshaleta tabu hapa itabidi nirudi baada ya juma moja niongee na hawa ndugu zangu wote bila ya kujali vyama vyao.

Mzee Mboya alifanya hivyo na kuwaeleza kuwa watu wa Igunda kuwa nia ya CCM ya kuwa na Mwenge siyo kuleta mgawanyiko bali kuwa pamoja, aliomba ndugu zake na jambo hilo likaisha na hadi sasa Zahanati ya Igunda inafanya kazi vizuri,

Mwanakwetu Zahanati ya Igunda hata mtu akienda leo hii ni miongoni mwa zahanati bora za umma nchini.Kilichofanyika ni kuondoa jiwe lenye jina la mkimbiza mwenge na huduma kuendelea kama kawaida..

Swali la kujiuliza je Mkimbiza Mwenge anajua hali aliyoiacha baada ya kuukataa mradi huo na kazi kubwa iliyofanya na CCM baada ya tukio hilo?

Au Kazi ya CCM ni kubebeshwa lawama kwa makosa yanayofanywa na watu wengine?

Binafsi nilikwenda mbali zaidi, nilifuatilia hata alipotokea mkimbiza mwenge huyo, nilibaini kuwa hata kwao alipotokea wanatumia zahanati moja ya zamani ambayo hata ukarabati wake ulikuwa hafifu

Binafsi ninaona kuwa dhana ya kuikata miradi kwa wakimbiza mwenge haina tija inabomoa badala ya kujenga. Kwani hata kama mradi unakataliwa kwa faida ya nani?

Kama kweli mradi huo upo chini ya kiwango Rais kila eneo anawawakilishi kadhaa katika kila pahala watimize wajibu wao na mradi huo uondolewe kabla ya kiongozi wa mwenge hajafika na kinyume chake CCM itabebeshwa mzigo ambao si wake kila wakati.

Mwanakwetu japokuwa miradi hiyo mitatu ilikataliwa lakini wananchi wa wilaya hii jioni yake walijitokeza kwa wingi kufurahi pamoja na wenzao huku Christian Bella-Best of The Best akitumbuiza katika Viwanja vya Mlowo kwa nyimbo kama MSALIMITI, MAMA, NAKUHITAJI, NASHINDWA, USILIE, YAPO WAPI MAPENZI na zingine nyingi usiku kucha.

makwadeladius@gmail.com



0717649257





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...