Adeladius Makwega-TANGA

Mwishoni mwa wiki nilikuwa najiandaa na safari ya kwenda Tanga, nilipokuwa natafuta zawadi za kwenda nazo huko kwa ajili ya familia yangu, nilibaini kuwa japokuwa Tanga wana matunda mengi lakini ubuyu haupo. Kwa hiyo nilimuagiza kijana mmoja wa Chigogo aniletee gunia la ubuyu ili kuweza kwenda nao huko.

Kweli nililetewa gunia zima la ubuyu kwa shilingi 15,000/-huku likiwa limeja pomoni, nikaliangalia vizuri lile gunia nikasema ni mzigo mkubwa mno kusafiri nao hadi Tanga. Nikafikiriii nikaenda mashine jirani na kuwaeleza waupitishe katika mashine ya kukoboa ili nipate unga wake tu na mzigo uwe mwepesi.

Nilifanya hivyo na kupata madebe mawili ya unga wa ubuyu, alipomaliza kazi hiyo nikaona mbegu za ubuyu nyingi katika madebe zaidi ya manne. Nikauliza, sasa hizi mbegu zinatupwa?

Kijana wa mashine akajibu, ndiyo, zinatupwa mzee, lakini zamani tulikuwa tunazikamua mafuta au tunasaga katika jiwe/kinu na kuwa kiungo kizuri sana kwa mboga za Wagogo na wengine wakifanya baishara ya unga huo wa mbegu za ubuyu na mafuta yake.

“Kwa bahati mbaya Serikali ikapiga marufuku, wakisema mafuta ya ubuyu yana madhara kiafya.”

Nikamwambia kijana wa mashine nifungie mbegu zangu, nikawekewa katika kiroba na kwenda nazo kwangu. Kijana aliyebeba akauliza mzee hizi unakwenda nazo wapi? nikamwambia nyumbani kwangu kuna bonde kwa hiyo hizi mbegu naenda kuzimwaga hapo kupunguza mmomonyoko wa udongo katika bonde hilo.

“Mzee zitaota hizi, maana ardhi ya Dodoma ni udongo wa mibuyu.”

Nikajibu kuwa ikiwa inaota nitakuwa naipunguza kidogo kidogo.

Mzee, hizi mbegu zamani ilikuwa pesa ya maana sana, hata jirani yako alikuwa ni miongoni wa wafanyabiashara wa mafuta ya ubuyu, alisema kijana huyu.

“Mbegu za ubuyu kwa Dodoma, Singida na mikoa mingi jirani zinapatikana kwa wingi kama zingetumika sana zingeua kabisa soko la mafuta ya madukani na sisi Wagogo ni kiungo chetu cha miaka mingi hasa hasa zile mbegu zikitwangwa katika kinu na kuungia mboga zetu, mboga inanoga sana.”

Aliniambia kijana aliyenibebea mizigo, huku nikimtambua kwa jina moja la Josefu.

Nikashushiwa mizigo yangu na kwenda hadi kwa jirani, Nilipiga hodi na kukaribishwa vizuri, nikamuuliza eti jirani uliwahi kufanya biashara ya mafuta ya ubuyu?

Mama huyu anayefahamika kama Mdala Zipora alinjibu kuwa mwanangu biashara hiyo ilishamiri mno wakati wa Urais wa Jakaya Kikwete na lita moja ya mafuta ya ubuyu yalikuwa kati ya shilingi 20,000-30,000/-

Hivi sasa kuna shida ya mafuta, mimi wala nisingepata tabu, ningekusanya mbegu zangu na kukamua mafuta hayo, ningepata pesa na ningepata mafuta ya kupikia. Alisema jirani yangu huyu ambaye ni mama mwenye umri kati ya miaka 63-65.

Binafsi nikasema kama kwa mwaka 2013 lita moja iliuzwa shlingi 30,000/- miaka 10 sasa lita moja ingefika zaidi ya shilingi 50,000/- ambayo ni mara 16 ya lita ya petrol kwa bei ya sasa na pia ni mara tano ya bei ya lita moja ya asali ya nyuki wakubwa kwa sasa inayouzwa shilingi 10,000/-

Msomaji wangu hiyo nakisi ya bei ya lita moja ya mafuta ya ubuyu kwa lita moja asali au petrol inakupa picha ya thamani ya mafuta hayo.

Lakini Serikali Ikatangaza mafuta hayo yana madhara kiafya hivyo yasitumike kabisa.

“Hapa Dodoma palikuwa na Mkorea ambaye alikuwa akinunua unga wa ubuyu na mbegu zake ambazo alizikamua na kuyachukua mafuta hayo na mimi nilikuwa naenda kukamua na kuyauza kwa wateja wangu wengi yaani baba! Hata ukikamua robo ya lita unauza kwa shilingi kati ya 6,000-7,000/-.” Alisema Mdala Zipora.

Kwa kuwa Jakaya Kikwete alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya mwaka 2005-2015,binafsi nikaanza kutafuta taarifa za mafuta ya ubuyu katika kipindi hicho juu ya katazo hilo na athari zake kiafya.

Kulingana na taarifa iliyoandikwa na mwanahabari Theopista Nsanzungwako ya Julai 8, 2013 katika gazeti la serikali Habari Leo ilisema kuwa,

“Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la Wajasiriamali wanaouza mafuta ya ubuyu kama dawa, na kuwaelekeza wananchi kunywa, napenda kuwataarifu kuwa mafuta hayo ni hatari kwani yana tindikali ya mafuta.”

Gazeti hilo lilimnukuu msemaji wa TFDA Gaudensia Simwanza aliyekuwepo katika maonesho ya 37 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam huku msako ulifanyika katika maonesho hayo kwa wale waliodiriki kufanya biashara hiyo hapo kiwanjani.

Jambo hilo halikuishia hapo nalo Gazeti la Mwananchi la Julai 31, 2013, siku 23 baada ya TFDA kusema hayo, lilimnukuu Mkemia Mkuu wa Serikali wakati huo, Profesa Samwel Manyele akiwataka Watanzania kuacha kutumia mafuta ya ubuyu kwa maelezo kuwa yana kemikali yenye madhara kwa afya ya binadamu.

Profesa Manyele alipinga kauli iliyotolewa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road mwanzoni mwa wiki hiyo wakati huo kwamba mafuta hayo hayana madhara katika mwili wa binadamu yakitumiwa vizuri.

Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii wakati huo, Dk Seif Rashid, alitangaza kuwa mafuta hayo si salama na kusisitiza kuwa huo ndiyo msimamo wa serikali kuhusu mafuta hayo, hivyo wananchi waamue wenyewe kuyatumia au kutokuyatumia.

Akizungumza na gazeti mwananchi, Profesa Manyele alisema,

“Ofisi yangu inaiunga mkono kauli ya Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) kuzuia matumizi ya mafuta hayo, Watanzania wanatakiwa kuwa wasikivu na onyo hilo.”

Alisema sheria inayoruhusu mtu yoyote kufanya biashara ya chakula na dawa ipo chini ya TFDA, wao ndio wanaotoa kibali cha kufanya biashara na kutengeneza bidhaa, kwamba wakisema bidhaa fulani haifai wanatakiwa kusikilizwa.

“Wao ndio wanaotoa kibali cha kutengeneza bidhaa, pia wana uwezo wa kuzuia uzalishaji kwa mujibu wa sheria. Ofisi ya Mkemia Mkuu haiwezi kuzuia uzalishaji.”

Aliongeza kuwa tayari TFDA imeshaeleza athari ya kemikali iliyopo katika mafuta ya ubuyu inayoweza kuathiri afya za Watanzania, kuwataka wananchi kuwa makini na kama wanahitaji taarifa za msingi wanatakiwa kwenda katika ofisi za mamlaka hiyo.

“Mimi kama Mkemia Mkuu wa Serikali nitaingilia kati kama mambo yote yatashindikana na serikali itataka kutoa tamko rasmi kuhusu matumizi ya mafuta haya.”

Binafsi naona kuwa swali ambalo bado limebaki kwa kipindi cha miaka inayokaribia 10 kwa sasa je kwanini  Ocean Road kwa upande wake na TFDA ya wakati huo kwa pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali kwa nini kila mmoja alipita njia yake katika hilo?

Kama hoja ni madhara mbona sigara, tumbaku, pombe zina madhara kwa binadamu lakini hazijapigwa marufuku bali tu imekwa sentensi katika bidhaa hizo kuwa zina athari kwa afya ya mtumiaji?

Kwa hakika hata kama kuna kemikali ndani ya mafuta hayo, kwa maendeleo ya sayansi ya sasa inaweza kuondolewa kwa kutumia vifaa bora ili kuisaidia jamii kuendelea kuyatumia mafuta hayo na hilo litasaidia kukuza hata uchumi wa maeneo ambayo mibuyu inastawi kwa wingi.

Kwa maana ya mazungumzo ya ndugu hawa, wao walikuwa wakitumia unga wa ubuyu na mafuta yake kama kiungo kwa miaka mingi wamezaliwa wakiona mababu na mabibi wanautumia unga na mafuta hayo iweje ulipigwa marufuku?

Mwanakwetu ushauri wangu hasa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Ocean Road na TFDA mpya ya sasa watoe wataalamu ambao ni wazaliwa wa asili ya mikoa ya Dodoma, Singida na hata Iringa wakae pamoja walitazame jambo hilo alafu watoke kuielezea jamii ya watumiaji wa kiungo hicho  na hatua kadhaa za maboresho ya kiungo hicho ili kuondoa utata kwani nimebaini kuwa kiungo hicho bado kinatumika kwa siri.

Mwanakwetunalisema hilo kwa kuwa itambulike waziwazi kunaga ubaga kuwa namna ya kupika na kula vyakula ni sehemu ya utamaduni wa makabila yetu. Kupiga marufuku haitoshi, elimu ya kina inahitajika zaidi isitoshe hata huko kupishana kwa wataalamu kunajenga hoja nyengine.

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...