Mjiolojia Fortunatus Kidayi akitoa maelezo kuhusu mradi wa LNG kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab R. Telack aliyetembelea banda la PURA katika Maonesho ya Tano ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yanayoendelea mkoani Morogoro.


Na Ebeneza Mollel

Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeeleza kuwa imejipanga kikamilifu kusimamia mradi wa kubadili gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) ili kuhakikisha mradi huo unaleta tija na kuchangia maendeleo ya uchumi nchini.

Hayo yamesemwa na Mjiolojia Fortunatus Kidayi alipokuwa akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab R. Telack aliyetembelea banda la PURA katika Maonesho ya Tano ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yanayoendelea mkoani Morogoro.

Alifananua kuwa miongoni mwa majukumu ya PURA kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 ni kusimamia mradi wa LNG. Mradi huu unalenga kuvuna gesi asilia iliyogunduliwa kina kirefu cha bahari nchini kwa ajili ya matumizi ya ndani na kiasi kingine kuuzwa nje ya nchi.

“Mradi huu ni wa thamani ya Dola za Marekani bilioni 30 na unatarajiwa kutekelezwa eneo la Likong'o mkoani Lindi na PURA imeendelea kujiimarisha kiutendaji ikiwemo kuendelea kuwajengea watumishi wake uwezo katika eneo la LNG'' alieleza Bw. Kidayi.

Aliongeza kuwa PURA imejipanga kuhakikisha Watanzania wanapata fursa ya kushiriki katika mradi wa LNG kupitia ajira na utoaji wa huduma na bidhaa katika kipindi chote cha utekelezaji wake.

“Katika kufanikisha hilo, PURA kwa kushirikiana na EWURA imeandaa kanzi data ya kuwasajili watoa huduma wa Kitanzania na wazawa wenye taaluma mbalimbali ikiwemo masuala ya mafuta na gesi. Kanzi data hiyo inajulikana kwa jina la Common Qualification System (CQS) na iko tayari kutumika,” alibainisha.

Aliongeza kuwa “mradi wa LNG unatarajiwa kuleta fursa nyingi nchini ikiwa ni pamoja na ajira zaidi 6,000 na ikiwa ni pamoja na fursa za kuuza bidhaa na huduma wakati wa utekelezaji wa mradi huo. Serikali ilishatoa Shilingi bilioni 5.7 kulipa fidia kwa wananchi zaidi ya 640 waliopisha utekelezaji wa mradi. Aidha, majadiliano baina ya Serikali na kampuni zitakazotekeleza mradi wa LNG yanaendelea na yanatarajiwa kukamilika hivi karibuni''

Kwa upande wake, Mhe. Telack ameipongeza PURA kwa kusimamia suala ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za mkondo wa juu wa petroli, na kusema kuwa wananchi wa mkoani humo wanasubiri kwa hamu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo na kwamba ana imani watapewa kipaumbele wakati wa utekelezaji wake.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...