
Njombe
WAKAZI wa kijiji cha Ivilikinge wilaya ya Makete mkoani Njombe,wameanza kuhamasishana kushika mimba na kuzaa kutokana na kujengwa Zahanati kubwa ukilinganisha na iliyokuwepo awali yenye miundombinu chakavu na huduma za matibabu zilizokuwa sio za uhakika.
Wameanza kubainisha hayo mbele ya mkuu wa wilaya ya Makete Juma Sweda wakati akipokea msaada wa mabati 200 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika kijiji hicho ambao umetolewa na benki ya NMB.
Abia Sanga, Amokile Mgaya na Yona Tweve ni baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamesema jengo la zahanati hiyo la awali ni dogo ambalo lilikuwa likipelekea kuwepo kwa mrundikano wa wagonjwa wengi hadi wengine kukosa sehemu ya kupumzishwa baada ya kupata matibabu na kusababisha wanawake kijijini hapo kusitisha kushika mimba na kuzaa watoto kutokana na hofu ya kupoteza maisha.
"Kuanzia sasa sisi wanawake tuhamasishane kuzaa kwa kuwa jengo hili la zahanati inayojengwa sasa itakidhi mahitaji na tutajifungua salama" alisema Abia Sanga
Mkuu wa wilaya hiyo Juma Sweda mara baada ya kupokea msaada huo wa mabati ambayo thamani yake ni 8.5 milioni alisema utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa zahanati utafanyika haraka iwezekanavyo ili wananchi wa kijiji hicho waweze kunufaika na huduma za afya.
"Kwakuwa zahanati hii itaisha niwaombe NMB mtuongezee vitanda na tukishafanya hivyo wakina mama wapo wanataka kujifungua na wapo tayari kushika mimba na serikali ya mama Samia inasema kushika mimba na kijifungua ni bure" alisema Sweda.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...