Na Said Mwishehe, Michuzi TV

KUNA mambo lazima tusema hadharani kuhusu hii Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Serikali ya Awamu ya Sita yenye kauli mbiu inayosema Kazi iendelee hakika inawatumikia Watanzania nikiwemo mimi kwa uadilifu,uzalendo na kubwa zaidi inatekeleza majukumu yake kwa kusimamia haki.

Kukaa kimya na kushindwa kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia hizo ni dalili za kuwa Mchawi...., Usijali ndugu yangu hilo neno Mchawi nimechomekea tu. Meza mate basi halafu endelea kunisoma, tabasamu hata kidogo.

Usisahahu Tanzania ni ya Watanzania na sasa chini ya Mama Samia ambaye ndio Rais wetu ameifanya nchi kuwa tulivu, imetulia na wenyewe, wala hatuna neno. Mama anaupiga mwingi sana, hongera Rais Samia, Hongera mama.

Sasa iko hivi sifa kubwa ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan naiweza kusema Awamu ya Sita ni zama za utu, ndio Rais Samia katika kauli zake amekuwa akisisitiza mambo kufanyika kwa kuzingatia utu, amini nakwambia.

Kitendo cha Serikali kusimama katika misingi ya utu kimeendelea kupongezwa na watu wa kada mbalimbali , wanaosifia wapo kutoka ndani na nje ya nchi yetu nzuri. Tanzania nzuri na ukitaka kuifaidi pata muda kisha angalia Filamu ya The Royal Tour, utaona uzuri halisi wa Tanzania yetu.

Ngoja nirudi kwenye hili la Rais Samia kujali utu lakini niongeza na lile nililosema mwanzo la upendo na kujali limesababisha Serikali muda wote kuwa karibu na watu, imekuwa sikivu,inasikiliza kisha inatafakari na baadae inaamua, katika hilo lazima tuseme ukweli.

Katika kujali ndio maana hata baada ya bei ya Mafuta kupanda na kusababisha malalamiko miongoni mwetu Rais Samia aliamua kukaa na kutafakari na kisha akaja na majibu. Wote tunakumbuka baada ya bei ya Mafuta kupanda kwenye soko la Dunia na huku kwetu nako ikapanda, ikapanda haswaa na hapo ndipo kilio kikaanza, Wafanyabishara nao wakatumia nafasi hiyo kupandisha bei ya bidhaa.

Mtaani malalamiko yakawa makubwa, kila mmoja akiwa anawaza itakuaje na bahati nzuri tunafamu Serikali ilipandisha bei ya Mafuta sio kwasababu haiwapendi watu wake bali soko la Dunia ndilo limesababisha hali hiyo Kuna sababu nyingi Mafuta kupanda kwenye soko la Dunia lakini sababu kubwa ni Vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine.

Wakati wananchi wa Tanzania tunajiuliza hali itakuaje na wakati huo huo nauli nazo zikipanda , Rais Samia Suluhu pamoja na wasaidizi wake wakaamua kuja na jibu moja tu ambalo wameona linaweza kusaidia kudhibiti bei ya ongezeko la mafuta.

Rais Samia akaamua kutoa ruzuku ya Sh Bilioni 100 ,lengo la ruzuku hiyo ni kujaribu kupunguza bei ya mafuta kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu na hasa kwa wauzaji Mafuta.
Na hiyo fedha iliyotolewa na Serikali ya Rais Samia ni katika kipindi cha mpito wakati hatua zaidi zikiendelea kuchukuliwa.

Hakika uamuzi wa Rais Samia na Serikali anayoiongoza kuamua kutoa fedha hizo imekwenda kuleta auheni kwa wananchi. Hakuna anayelalamika kama mwanzoni,unajua kwanini?..., wanaona jitihada ambazo Serikali inazichukua kudhibiti bei ya Mafuta.

Tuambiane ukweli fedha iliyotolewa na Serikali ni nyingi lakini Rais Samia kwa upendo wake kwa wananchi anawaongoza akaona isiwe tabu, anataka kuona watu wanaishi maisha ya furaha. Hili la kupanda bei ya mafuta lilikuwa linatia tumbo joto,dukani ukienda bidhaa bei juu,ukirudi kwenye usafiri nako vilio.

Rais Samia Suluhu Hassan naomba kurudia tena ,nakupongeza kwa uamuzi huu wa kukubali kutoa hela ili kwenda kusaidia kwenye kudhibiti bei ya mafuta, Rais Samia umeamua kubeba mzigo kwa niaba yetu.
Ninaposema Rais wetu amejawa na utu, unaweza kuona kwenye hili la mafuta, ingekuwa wengine wala tusingesikilizwa lakini Mama amesikia kilio chetu, tunakushukuru Rais Samia na 2025 wewe ondoa shaka, tunakuachaje kwa mfano? Ni sisi na wewe ,wewe na sisi.

Kuna mtu mmoja tulikuwa tunajadiliana uamuzi huu wa Rais kutoa fedha Sh.bilioni 100 kwa ajili ya kwenda kuleta unafuu wa bei ya mafuta, wakati anazungumza alikuwa kama vile anachukulia poa lakini baadae alipopata maelezo ya kutosha nakumbuka alisema hivi; Watanzania hakika tunaye Rais anayejua shida za watu lakini na kuzipatia majibu kwa haraka , akamalizia kwa kumtakia afya njema na maisha marefu Rais wetu.

Lakini ngoja nieleze kitu hapa, Tanzania kwa nchi za Afrika Mashariki kwenye bei ya mafuta pamoja na kwamba imepanda lakini unapoamua kulinganisha na nchi nyingine majirani zetu bado tulikuwa chini na bado Rais akaona lazima aangalie njia ya kudhibiti bei.

Juzi juzi EWURA ilitoa bei elekezi kwenye mafuta ya Dizeli, Petroli na Mafuta ya taa, angalau bei inaleta auheni.
Ujue kwenye maisha pamoja na mambo yote unatakiwa kujifunza kushukuru pale unapoona limefanyika jambo jema.

Kwa niaba ya Watanzania wengine narudia tena kusema tena kwa msisitizo Rais Samia tunakushukuru kwa uamuzi huu wenye upendo mkubwa. Shilingi Bilioni 100 ambazo umezitoa kama zingetumika kufanya mambo mengine ya maendeleo hakika nchi ilikuwa inakwenda kupiga kasi kubwa ya kimaendeleo.

Ukitaka kujua wingi wa Sh.bilioni 100 chukua noti za shilingi 5000 au shilingi 10000 halafu zipange moja baada ya nyingine utaona zinakwenda kuishia wapi, lakini Rais wetu kwa upendo wake amezitoa kama ruzuku ya kudhibiti bei.

Hii ndio Awamu ya Sita ya Mama Samia Suluhu Hassan ,Mama anayejua watu wake wanataka nini na kwa wakati gani, hana sifa, hana majivuno halafu nikwambie tu hata mambo ya kusifiwa alikataa,nami wala simsifii bali namshukuru kwa hatua aliyoichukua .

Nakumbuka hata wakati anatangaza hatua ambazo Serikali itachukua wala hakuona haja ya kutangaza yeye ,aliamua kumuachia Waziri wa Nishati, January Makamba, ndio mwenye dhamana na Nishati zote, Makamba akaunguruma bungeni kuelezea hatua zilizochukuliwa na Serikali.

January kabla ya kutoa kauli ya Serikali bungeni alitumia nafasi hiyo kuelezea hali ilivyo kwenye soko la Dunia, naomba tumia dakika kupitia kile alichokieleza ,alisema hivi

"Napenda kuchukua hatua hii kuwajulisha kuwa Rais samia Samia Suluhu Hassan alituita na kutuketisha kitako sisi wasaidizi wake tukiongozwa na Waziri Mkuu. Mheshimiwa Rais alizungumza mengi, kwa uchungu mkubwa sana.

“Ameguswa sana na malalamiko na masononeko ya wananchi juu ya kupanda kwa gharama za mafuta na gharama za bidhaa na maisha kwa ujumla. Akasema, hata kama bei iko juu duniani, hata kama takwimu na namba zinaleta mantiki, lakini tutatungulize utu na huruma kwanza katika kulishughulikia suala hili.

“Bila shaka kwa wale waliomtizama katika televisheni akiongea na Taifa jana usiku mtakuwa mmeona huruma iliyojawa katika uso wake na imani katika sauti yake. Isingelikuwa uungwana wake wa kuheshimu mamlaka na mipaka ya Bunge, kauli hii ninayoitoa leo angeitoa yeye muda ule jana.

“Lakini akaniambia, maadam Bunge lilikuelekeza wewe uwasilishe taarifa, basi busara ya kiuongozi inataka Bunge lisikie taarifa hii kutoka kwako. Hivyo amenituma kuja kwenu leo kuwaletea habari njema.Kabla sijaufikisha ujumbe huo na kueleza hatua ambazo Serikali inachukua kwenye suala hili, ili kuongeza uelewa na kujenga muktadha.

“Ni vyema nikaeleza mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia na kutoa mnyambulisho wa gharama zinazojumuishwa katika kukokotoa bei za mafuta.Nchi yetu haina visima vya mafuta wala mitambo ya kuchakata mafuta ghafi. Kama zilivyo nchi nyingi, sisi ni wapokeaji wa bei. Kwa maana hiyo."

Makamba akatoa mfano kwa mafuta ya dizeli, mchango wa bei katika soko la dunia kwenye bei ya mwisho ya mlaji ulikuwa ni asilimia 64 mwezi huu. Na bei za mafuta katika soko la dunia zinatokana na uzalishaji au upatikanaji wa mafuta ghafi (crude oil), upatikanaji wa mafuta yaliyochakatwa na mahitaji ya mafuta.

Pamoja na ufafanuzi wa kina ambao Waziri Makamba alielezea kuhusu hali ya upatikanaji mafuta katika soko la Dunia ambayo, amesema kutokana na mahitaji ya wananchi, maoni na ushauri wa Wabunge, maelekezo ya CCM na ujasiri wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais alitoa maelekezo kwamba mwaka ujao wa fedha ni mbali.

Akataka ahueni itafutwe mapema zaidi. Hivyo basi, kama hatua ya dharura Rais ametoa maelekezo kwamba, katika kipindi hiki kabla hatujafikia mwaka mpya wa fedha, Serikali ijibane na ijinyime na zitolewe Sh.bilioni mia moja kwa ajili ya kupunguza bei za mafuta hapa nchini. Ruzuku hiyo inatolewa kwa kupunguza matumizi ya Serikali katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2021/22.

Ameongeza kutolewa kwa ruzuku hiyo hakutagusa miradi ya maendeleo ambayo inaendelea. Nafuu nyingine inayotokana na mikopo aliyoeleza awali itakuja katika mwaka ujao wa fedha itaelezwa kwa kina zaidi na Waziri wa Fedha kwenye Bajeti ya Serikali mwezi ujao.

“Ruzuku hii ya Sh,bilioni bilioni 100 itatolewa kwa ajili ya kupunguza bei kuanzia Juni 1, 2022. Hii ni kutokana na kuwa, wafanyabiashara wa jumla wamekwisha lipia gharama ya mafuta ambayo imejumuishwa katika bei hizi za Mei 2022 na wafanyabiashara wa mafuta katika vituo wamekwishanunua mafuta kwa bei hii inayotumika sasa.

“Hatua nyingine zisizo za kifedha zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuruhusu watu wenye uwezo wa kuleta mafuta kwa bei nafuu kufanya hivyo. Wizara imekamilisha kufanya tathmini ya kampuni zote zilizoonesha nia ya kuweza kuleta mafuta kwa bei nafuu kwa lengo la kujiridhisha na uwezo wao wa kuleta mafuta hayo ili kuhakikisha uwepo wa mafuta nchini,”amesema.

Amesema mipango hiyo ikileta matokeo yanayotarajiwa, bei za mafuta zitapungua zaidi kuanzia mwezi Agosti 2022.Pia kuanzisha Mfuko wa Kuhimili Ukali wa Bei za mafuta (Fuel Price Stabilization Fund). Serikali imeandaa utaratibu wa kuanzisha mfuko maalumu utakaotumika kupunguza makali ya bei ya mafuta.

Baada ya kuelezea yote nitumie nafasi hii kushukuru msomaji wangu kuhusu nilichoandika lakini kubwa zaidi kila mmoja kwa nafasi yake atambue anaowajibu wa kumuunga mkono Rais Samia kwa kazi kubwa na nzuri ambayo ameendelea kuifanya kwa ajili ya nchi yetu, binafsi kwenye ruzuku ya Mafuta nitaendelea kumshukuru siku hadi siku.Ahsante Rais Samia kwa upendo wako kwetu.



0713833833




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...