Na WAF – Bungeni, Dodoma.
Licha ya matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza kuwa na gharama kubwa na yana hitaji tiba wakati wote, Serikali imekuwa ikitoa msamaha wa matibabu kwa wagonjwa wanaougua magonjwa yasiyoambukiza ambao wamethibitika kuwa hawana uwezo wa kugharamia matibabu yao kwa mujibu wa Sera ya Afya.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Jimbo la Chaani, Mheshimiwa Juma Usonge Hamad aliyehoji Serikali ina mpango gani wa kutoa matibabu bure kwa maradhi yasiyoambukiza kama Kisukari, Presha na Shinikizo la Damu.
Hata hivyo Dkt Mollel amesema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ambao utawezesha wananchi wote kupata huduma za afya katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini.
Akijibu Swali la nyongeza lilioulizwa na Mheshimiwa Usonge aliyehoji usumbufu wanaopata wazee pindi wanapoenda hospitalini kupata huduma za matibabu, Dkt. Mollel ameendelea kuwasisitiza wataalam kufuata maagizo yanayotolewa na viongozi ikiwemo kuhakikisha Wazee wanapata matibabu bure katika vituo vya kutolea huduma za afya.
“Nitumie fursa hii kutoa agizo kwa Waganga wote wa Mikoa na Wilaya, suala la matibabu kwa wazee ni bure na wanatakiwa kuwa na dirisha lao la kupata huduma, hatutegemei kusikia tena malalamiko ya wazee wanapitia mlolongo mrefu wa kupata huduma za matibabu” amesisitiza Dkt. Mollel.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...