Na Said Mwishehe, Michuzi TV
SERIKALI ya Tanzania kupitia Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo imesema ni vema mazoezi ya Yoga yakachukuliwa kwa umuhimu wake ili wananchi waweze kujenga Umoja,mshikamano na kuboresha afya ya mwili na akili.
Aidha imesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa kila aina pale inapohitajika ili wananchi wawe na furaha ya maisha kwa kuzingatia mchezo wa Yaga ambao asili yake ni nchini India umetokea kukubalika na mataifa mbalimbali duniani na watu zaidi ya Bilioni moja duniani wanafanya mazoezi ya Yoga
Hayo yamesemwa leo Juni 19,2022 na Naibu wa Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Pauline Gekul wakati wa mazoezi ya Yoga yaliyofanyika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam na kuwakutanisha watu 3000 wakiwemo raia wa India wanaoishi nchini wakiongozwa na Balozi wa India nchini Tanzania Binaya Srikanta Pradhan.
Akizungumza zaidi kabla ya mazoezi hayo Naibu Waziri Gekul amesema anamshukuru Balozi wa India nchini Tanzania Binaya Srikanta Pradhan pamoja na timu yake kwa juhudi za kuwaunganisha na kuwaongoza Watanzania wapenzi wa Yoga kukutana kila mwaka inapokuwa nafasi ya kufanya hivyo.
"Kupitia juhudi zako Balozi Srikanta leo hii tunaona Watanzania wanapata fursa ya kujumuika na kuadhimisha siku hii adhimu.Umekuwa kiunganishi muhimu kwa jamii za Kihindi zilizopo nchini na Watanzania kwa ujumla.Tunashukuru kwa juhudi za kuifanya Yoga ifahamike kwa Watanzania wa rika mbalimbali,"amesema.
Ametumia nafasi hiyo kueleza anawashukuru wote ambao wameshiriki mazoezi ya Yoga na amewaomba kilichofanyika leo kisiishie hapo bali iwe fursa ya kujifunza na kutumia mbinu hiyo inayosaidia kutibu mwili na akili kwa kiwango kikubwa.
"Natambua wazi huu ni mwaka wa nane wa kuadhimisha siku ya Yoga na jambo la kufurahisha Watanzania wameyakubali mazoezi ya Yoga.Ni vema tukafahamu Yoga ni mazoezi ya kimwili na kiroho yanayosaidia kurekebisha uhusiano wa roho,mwili na mawazo ya mwanadamu kwa Nia ya kuyafurahia Mazingira anayoishi kila siku.
" Hivyo mazoezi ya Yoga yameonekana kuwa na manufaa sana hasa yanapofanyika kwa utaratibu na utalaamu ambapo yanasaidia kutibu na kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza .Hivyo nisisitize watu wanaweza kujifunza wafanye hivyo kwa manufaa yao,"amesema.
Naibu Waziri huyo ametumia nafasi hiyo kuahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inajali kila kitu kinachomwezesha mtanzania kuishi kwa amani huku akishiriki michezo na burudani kwa kadri ya uwezo wake."Ni vema mazoezi ya Yoga yakachukuliwa kwa umuhimu wake. "
Awali Balozi wa India nchini Tanzania Biyana Srikanta Pradhan amesema kuwa mazoezi ya Yoga yamekuwa yakiadhimishwa kila ifikapo Juni 21 ya kila mwaka lakini kwa Tanzania wameadhimisha leo Juni 19 kwasababu ni siku ya mapumziko kwani Juni 21 itakuwa siku ya kazi.
Kuhusu mazoezi ya Yoga Balozi Pradhan amesema yameendelea kufanywa na watu wa mataifa mbalimbali duniani na idadi ya watu wanaofanya mazoezi hayo ni zaidi ya bilioni moja.Aidha maadhimisho hayo yako kwenye kalenda ya Umoja wa Mataifa ( UN).
Ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiutoa katika kufanikisha mazoezi ya Yoga na tangu yameanza kuadhimishwa wamekuwa wakipewa Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya kuadhimisha .Ameema kwa mwaka huu nchini Tanzania mazoezi ya Yoga yamefanyika katika mikoa mitano.
Naibu Waziri wa Utamaduni ,Sanaa na Michezo Pauline Gekul ( wa pili kushoto) akiwa na Balozi wa India nchini Tanzania Biyana Srikanta Pradhan ( wa kwanza kushoto) wakishiriki mazoezi ya Yoga yaliyofanyika leo Juni 19,2022 Uwanja wa Uhuru ,Dar es Salaam .Mbali ya viongozi hao watu zaidi ya 3000 wakiwemo raia wa India wanaoishi nchini wameshiriki.
Washiriki wa mazoezi ya Yoga wakiendelea kufanya mazoezi hayo
Balozi wa India nchini Tanzania Biyana Srikanta Pradhan (wa kwanza kushoto) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul ( wa pili kushoto) kabla ya kuanza kwa mazoezi ya Yoga yaliyofanyika leo Juni 19,2022 katika Uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul akizungumza kabla ya kuanza kwa maozi ya Yoga katika Uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam ambapo ametumia nafasi hiyo kuhamasisha Watanzania kushiriki mazoezi hayo.Balozi wa India nchini Tanzania Biyana Srikanta Pradhan akizungumza kuhusu maadhimisho ya mazoezi ya Yoga ambayo kwa nchini yameadhimishwa leo na ratiba ya Umoja wa Mataifa (UN) maadhimisho ya Yoga hufanyika kila ifikapo Juni 21 mwaka huu.
Sehemu ya washiriki wa mazoezi ya Yoga wakiendelea kufanya mazoezi hayo
Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Pauline Gekul (katikati) akiwa makini kufuatilia maelezo yaliyokuwa yakitolewa kabla ya kuanza kwa mazoezi ya Yoga yaliyofanyika Uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa mazoezi ya Yoga walipokuwa wakiendelea na mazoezi hayo yanayotumia mwili,akili na roho.Kwa mujibu wa takwimu zilizopo watu zaidi ya bilioni moja duniani wanafanya mazoezi ya Yoga
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...