Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya SGA Security imedhihirisha umahiri wake na umakini katika masuala ya ulinzi kwa kukabidhiwa tena cheti cha ISO 18788 baada ya ukaguzi uliofanywa na kampuni ya United Kingdom Accreditation Services (UKAS) ya Uingereza na kuifanya iendelee kuwa kampuni pekee ya ulinzi yenye uthibitisho huu wa kimataifa.
Kampuni hiyo ya Uingereza ilitoa idhini kwa kampuni ya Intertek ya Ubelgiji kuendesha zoezi hilo lililosimamiwa na Dk. Nick Yordanov Jijini Dar es Salaam.
Alisema uthibitisho huu wa kimataifa unahitaji uzoefu wa hali ya juu katika kutoa huduma kwa wateja kwa kuzingatia haki za binadamu na sheria zote husika. “Masuala ya muhimu yanahusisha kuifahamu vizuri taasisi husika ili kuweka sawa mipango katika utekelezaji wa shughuli za ulinzi,” alisema.
Dr Yordanov aliupongeza uongozi wa SGA kwa kufuata taratibu zote za viwango vya ISO huku akiongeza kuwa walifanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali ambapo SGA inatoa huduma na kugundua kuwa wanazingatia sana haki za binadamu, elimu ya kutosha kwa wahusika na uwezo wa kutekeleza kwa vitendo mambo muhimu.
“Nimeainisha maeneo machache tu ambayo yatawasaidia kuboresha zaidi lakini kwa ujumla mumethibitisha kuwa viwango vya ISO vinazingatiwa vikamilifu, hongreni sana,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa SGA Tanzania, Bw. Eric Sambu, aliwapongeza wafanyakazi wake kwa kuonesha weledi wa hali ya juu katika utekelezaji wa huduma mbalimbali za kampuni hiyo ambazo zinahusisha ulinzi, usafirishaji wa fedha, alarm, ulinzi wa kielektronia na usafirishaji wa vifurushi.
“Tunajivunia katika uwezo wetu wa kuongeza thamani kwa wateja wetu katika utekelezaji wa viwango hivi vya ISO,” alisema na kusisitiza wataendelea kuwawezesha zaidi wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa njia ya mafunzo na elimu katika masuala mbalimbali kama haki za binadamu ili watoe huduma bora zaidi kwa wateja wao.
SGA Security ilipokea cheti cha ISO 18788 mwaka 2020 kwa muda wa miaka mitatu ambapo ukaguzi wa mara kwa mara hufanyika kuhakikisha viwango hivyo vinazingatiwa na uthibitisho wa ubora kuongezeka.
Kampuni hiyo ilianza kutoa huduma nchini mwaka 1984 kama kampuni ya kwanza ya binafsi ikijulikana kama Group Four Security na baadaye Security Group Africa (SGA).
SGA imetoa ajira kwa takriban watu 6000 Tanzania na 18,000 katika ukanda wa Afrika Mashariki. SGA pia ni mwanachama wa chama cha kimataifa kinachosimamia mwenendo wa makampuni ya binafsi ya ulinzi (ICoCA) cha Uswisi na kinasimamia utendaji bora wa nchi na makampuni katika utoaji wa huduma za ulinzi.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...