Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Sweden nchini Sandra Diesel na Mkurugenzi Mtendaji wa KTO Maggid Mjengwa wakisaini makubaliano ya kuendeleza ushirikiano wa kuendeleza sekta ya elimu kupitia FDCs wanaoshuhudia ni Makamu mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya KTO Vivian Temi (kushoto,) na Mkuu wa Programu anayeshughulikia elimu kutoka ubalozi wa Sweden Paula Engwall, Leo jijini Dar es Salaam.



* Wanawake vijana washauriwa kutumia fursa hiyo kwa kupata elimu ya maarifa na ujasiriamali bure

·         * KTO yapongezwa kwa kutwaa tuzo ya heshima iliyotolewa na Rais Samia

TAASISI ya Karibu Tanzania Organisation imepokea shilingi Bilioni 2.5 kutoka Serikali ya Sweden kupitia shirika lake la SIDA fedha zilizoelekezwa kuboresha sekta ya elimu katika vyuo vya maendeleo ya wananchi (FDCs) kwa miaka miwili 2022/2024 pamoja na programu za kuwasaidia wanawake vijana waliokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mimba za mapema na hali duni ya maisha.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba wa kuendeleza ushirikiano baina ya SIDA na KTO Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Karibu Tanzania Organisation Maggid Mjengwa amesema kuwa Serikali ya Sweden kupitia SIDA wameendelea kushirikiana na Serikali kupitia KTO katika sekta ya elimu kwa kusaidia vyuo vya maendeleo ya wananchi 54 vilivyopo kote nchini.

‘’Awali wafadhili wengi hawakuelewa azma ya hiki tunachokifanya , Tulipowaeleza SIDA juu ya mpango huu walituelewa na kutusaidia…Tusingekuwepo hadi leo wametufanya tuendelee kufanya kazi kwa bidii na kuwafikia walengwa wengi zaidi na wafadhili wengine wameanza kuelewa tunachokifanya na wanajitokeza kushirikiana nasi katika kazi hii.’’ Amesema.

Mjengwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuhimiza suala la elimu kwa wanawake vijana waliokatisha masomo yao kupitia mfumo usio rasmi ambao KTO wanafanya kazi na wataendelea kuhakikisha vijana watanzania wakike na wakiume wanapata elimu.

Amesema SIDA wamekuwa na imani na taasisi hiyo katika kuhakikisha wanawake vijana wanapata elimu ya maarifa na ujasiriamali na kuwataka wazazi na walezi kuhamasika na kuhamasisha vijana kutumia fursa hizo kwa kupata elimu ya maarifa na ujasiriamali bila malipo kupitia vyuo hivyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Sweden nchini  Sandra Diesel amesema kuwa Sweden inaamini katika vyuo vya maendeleo ya wananchi na wameona ni vyema wakaendeleza mahusiano yao na taasisi hiyo kutokana na utendaji kazi na ushirikiano mzuri kutoka kwa Serikali katika kuboresha sekta ya elimu kwa wanawake vijana.

‘’Ushirikiano huu ni matokeo ya kazi inayofanywa na KTO na mfumo imara wa elimu ambao Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo KTO katika kuboresha sekta muhimu na matunda yanaonekana….. niwapongeze KTO kwa kupokea tuzo ya heshima kutoka kwa Rais wa Jamhuri wa Tanzania Samia Suluhu Hassan hivi karibuni hii inadhihirisha jitihada mnazozifanya zina tija kwa jamii.’’ Amesema.

Pia amesema kuwa katika sekta ya elimu kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi KTO inafanya jitihada kubwa na kueleza kuwa maeneo mengine ambayo SIDA wanafanya kazi nchini Tanzania ni pamoja na haki za binadamu na demokrasia, mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na masuala ya uchumi.

Awali Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi (KTO,) Vivian Temi ameeleza kuwa bodi itahakikisha fedha zilizotolewa na SIDA zinawafikia walengwa ambao ni wanawake vijana waliokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali hasa mimba za mapema na hali duni ya maisha kwa kuhakikisha wanapata elimu na fursa nyingine kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi ikiwa ni pamoja na ujasiriamali mpira fursa.

Vivian amesema, wataendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuhakikisha vijana walengwa wanarudi shuleni na kutimiza ndoto zao zilizokatishwa awali.

Vilevile Mkuu wa kitengo cha mawasiliano KTO Symphrose Makungu amesema, katika mkataba mpya wameongeza mambo mapya ambayo watayasimamia katika kuwaimarisha walengwa wa vyuo vya maendeleo ya wananchi.

Amebainisha mambo hayo ni pamoja na kupiga vita rushwa ya ngono kwa kujenga uelewa kwa mabinti na jamii na tayari programu hiyo imeanza katika FDC’s kwa kampeni ya ‘’Kuwa Jasiri, Kataa Rushwa ya Ngono.’’ Na kila chuo kitakuwa na klabu ya kupiga vita rushwa ya ngono.

Programu nyingine mpya zitakazosimamiwa na KTO ni pamoja na Elimu kwa watu wazima, teknolojia, utunzaji wa mazingira sambamba na uhamasishaji wa matumizi ya gesi asilia.

Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Sweden nchini  Sandra Diesel akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo na kueleza kuwa Sweden wanaamini katika vyuo vya maendeleo ya wananchi na wataendelea kushirikiana na ili kuleta matokeo chanya zaidi, Leo jijini Dar es Salaam.




Matukio katika picha wakati wa hafla hiyo.



·         

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...