Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo

WAKAZI wanaosubiri fidia kupisha Mradi wa barabara ya Bagamoyo - Mlandizi - Mzenga wameipigia goti kuiomba, Serikali kuharakisha ulipaji wa fidia zao, ili waendelee na shughuli za kimaendeleo.

Kilio hicho kimetolewa na wawakilishi wa wananchi hao ,kupitia Kamati waliyoiunda kutokea Matimbwa (Bagamoyo), Mbwawa (Kibaha Mji) na Mlandizi Kibaha (Vijijini) wakati Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Michael Mwakamo, alipozungumza nao.

Taimury Sematore alisema ,tangu walipopewa tangazo la kusimamisha shughuli za maendeleo , ujenzi wa nyumba ni kipindi kirefu pasipokuwa na matarajio ya kulipwa huku nyumba zao zikizidi kubomoka hali inayokwamisha maendeleo yao.

"Tumefanyiwa tathimini mara mbili lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea ,nyumba zetu zikiendelea kubomoka, tunawaona wewe Mwakamo na Muharami Mkenge mnavyoipambania lakini hatujajua hatma yetu" alisema Sematore.

Kipenzi Kondo alisema,wanaona maeneo mengine miradi kama hiyo inavyotekelezwa kwa kasi, lakini barabara hiyo utekelezaji unasuasua.

"Tunatamani tulipwe fidia zetu mapema tukafanye shughuli za maendeleo, kwani tulipo hatuwezi kufanya lolote la maendeleo, Mbunge katuitie Waziri mwenye dhamana aje atuambie ni lini tutalipwa fidia na ujenzi utaanza lini," alisema Kipenzi.

Bawazir Alwatan alisema kuwa barabara hiyo inayounganisha majimbo manne ina umuhimu mkubwa lakini inakigugumizi cha kuitengeneza.

Nae Mbunge Michael Mwakamo wa Kibaha Vijijini aliwaeleza, Serikali bado ina mpango wa kujenga barabara hiyo, na mara kadhaa wamekuwa akiiuliza Serikali ina mpango gani wa kuijenga kwa kiwango cha lami kuhusiana na ujenzi huo lakini majibu ni kwamba wanasubiri mafungu.

Mwakamo aliwataka,wananchi hao kuwa na subiri wakati serikali ikiendelea kujipanga kulipa fidia ili mradi huo ufanyike.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage alieleza,hawezi kuzungumzia suala hilo kwani linashughulikiwa na ngazi za juu.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...