Asila Twaha, TABORA

Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo  kwa  kuendelea kutoa fedha kujenga na kuboresha viwanja katika  shule za Msingi na Sekondari ikiwa ni kutambua umuhimu wa  somo la michezo  na kuendelea kuibua vipaji kwa wanafunzi.

Hayo ameyasema Julai 21, 2022  Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Batilda Burian wakati akikagua viwanja vinavyoendelea kujengwa na vinavyoendelea  kufanyiwa ukarabati katika Shule ya Sekondari  ya wavulana Tabora  na  Shule ya Wasichana Tabora  ikiwa ni maandalizi  ya michezo ya  Umoja wa Michezo na Taaluma Shule ya Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na  Mashindano ya  Umoja wa Michezo Sekondari Tanzania (UMISETA).

Dkt. Batilda amesema, pamoja na maendeleo mazuri yanayoendelea katika  ujenzi  huo amewataka wasimamizi  na mafundi kuzingatia muda, ubora na thamani ya fedha iliyotolewa  na Serikali katika uwekezaji  wa ujenzi wa viwanja hivyo na kusema si tu vitatumika kwa michezo hiyo bali ni viwanja endelevu vitakavyoendelea kutumika kizazi hadi kizazi.

“Ninamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya michezo,  sisi viongozi tutaendelea kusimamia miradi yote ya maendeleo inayoletwa na Serikali  ili kuhakikisha inajengwa kwa ubora na kukamilika kwa wakati" amesema Dkt. Batilda 

Kuhusu  Maandalizi ya mashindano ya Michezo ya UMISETA na UMISHUMTA  yatakayofanyika  Kitaifa Mkoani Tabora amesema,  Mkoa umejipanga  kupokea wageni wote  na  kuwahakikishia  uwepo wa mahitaji muhimu yatakayohitajika  na kuahidi kutoa ushirikiano na wapo tayari  kupokea  mashindano hayo.

“Nitoe wito kwa wenyeji wenzangu tufanye kazi kwa kujituma na kwa amani ugeni huu utatusaidia kuongeza  kipato endapo tu tutajituma kwa kufanya biashara zetu za kihalali na amani tuboreshe biashara kama mnavyofahamu  Tabora hatuna jambo dogo” amesisitiza Dkt. Batilda

Kwa upande wa Afisa Elimu Mkoa Mwl. Juma Kaponda ameishukuru Serikali kwa kupendekeza  mashindano  hayo  kufanyika Mkoa huo  na kuwataka  washiriki wenyeji kuwa  tayari kushiriki na tayari wanajinoa kwa kuendelea kufanya mazoezi.

Naye Mratibu wa Michezo Ofisi ya Rais - TAMISEMI Bw. George Mbijima amesema,  maandalizi yapo vizuri na yamekamilika na washiriki 3900  watashiriki michezo ya UMITASHUMTA  na   washiriki 4200 UMISETA ambapo itahusisha na viongozi wa michezo hiyo. 

Aidha, ametoa wito kwa washiriki wa michezo kuonesha vipaji vyao kwa kuzingatia sheria na taratibu za michezo kutoka kwa walimu kwani michezo ina sheria zake kama ilivyo katika masomo mengine.

Mashindano ya michezo ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule ya Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na  Mashindano ya  Umoja wa Michezo Sekondari Tanzania (UMISETA) inashirikisha Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...