*GEL yasema maandalizi yamekamilika
Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolph Mkenda, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya tatu ya wanafunzi waliosoma vyuo vikuu nje ya nchi yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya wakala wa vyuo vikuu nje ya nchi, Global Education Link (GEL), Abdlulmalik Mollel, wakati akizungumzia mahafali hayo.

Alisema hayo ni mahafali ya wanafunzi waliobahatika kusoma nje ya nchi na kuhitimu yatakayofanyika siku ya Jumapili katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam kuanzia asubuhi.

Alisema mabalozi wanchi mbalimbali ambazo vijana hao wamesoma wamethibitisha kushiriki katika mahafali hayo.

Alisema kwenye mahafali hayo wamealika Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu Zanzibar na Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU).

Alisema wengine waliothibitisha kushiriki ni Bodi ya Tiba Tanganyika (MCT), Bodi ya Uhasibu (NBAA), Sekretarieti ya Ajira ambayo ilikuwa ikitoa mafunzo kwa wahitimu kuhusu namna ya kujiajiri wanapomaliza masomo badala ya kusubiri kuajiriwa.

“Ili mahafali haya yafane mlengwa mkubwa ni mzazi na mtoto wake kwasababu mwanafunzi aliyesoma nje anakuja kusherehekea na wazazi na walezi waliojinyima kumlipia ada hivyo wanafunzi wametibitisha kushiriki,” alisema

Mollel alisema wanafunzi wanaotarajia kwenda nje ya nchi kusoma wataalikwa ili waweze kujifunza kutimiza malengo yao kama wenzao walioenda kusoma wakahitimu na wakarudi nyumbani kuleta ujuzi kusaidia maendeleo ya nchi yao.

Alisema wanafunzi wa Kitanzania watakaokwenda nje ya nchi watabebeshwa malengo ya kuitangaza nchi ili kusaidia jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akiitangaza nchi kwenye maeneo mbalimbali duniani.

“Tunamwona mama yetu anavyokwenda nje ya nchi yetu kuisemea katika rasilimali tulizonazo, fursa na uzuri wanchi yetu sasa peke yake hataweza tunataka watanzania watakaokwenda nje sasa hivi kuitangaza nchi liwe ajenda ya kipaumbele,” alisema Mollel

Alisema anataka kuona mwanafunzi anayekwenda nje ya nchi anaporudi anarudi na wawekezaji kwenye nyanja mbalimbali kama elimu na utalii badala ya kuhitimu na kurejea nchini wakiwa na vyeti vitupu.

“Tunataka kuona kupitia wao tunapata watalii na wawekezaji wa elimu kwasababu hatuhitimu na vyeti tu tunapaswa kuhitimu na maarifa ili nchi iweze kupiga hatua,” alisema

Alisema mahafali hayo ni kwa wanafunzi wote waliosoma nje ya nchi na siyo tu kwa waliopitia Global Education Link hivyo aliwataka ambao hawakupitia GEL waingie kwenye tovuti ya GEL watakuta sehemu ya mahafali ili wajaze maelezo yao.

Alisema mwanafunzi anayeruhusiwa kushiriki kwenye mahafali hayo ni yule aliyehitimu na anauthibitisho wa kuhitimu na uthibitisho ni cheti.

Alisema kuhitimu au kushindwa kuhitimu nje ya nchi kunategemea uwajibikaji wa mwanafunzi anapokuwa nje ya nchi hana usimamizi wa wazazi na walezi au taarifa potofu walizopata kuhusu vyuo wanavyoenda kusoma.

Mollel alisema kuna wanafunzi wanaenda kusoma nje ya nchi kwa kuchagua vyuo kwenye mitandao na wanapogundua kwamba havitambuliki wanaamua kuahirisha masomo.

“Kuna changamoto ya ada, mwanafunzi anasoma chuo ambacho kinalazimisha ada ilipwe yote kwa wakati mmoja na mzazi anakwama kulipa na anazuiwa kuendelea lakini kupitia GEL lazima ahitimu kwanza mambo mengine yafanyike baadae,” alisema

Alisema kuna mambo mengi yanayosababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kuhitimu nje ya nchi ikiwemo kujiingiza kweye mambo yasiyohusiana na masomo kutokana na kukosa usimamizi sahihi anapokuwa anaendelea na masomo.

Alisema mahafali hayo ni kama daraja kwa wanafunzi hao kukutana na wawekezaji mbalimbali ili kama kuna fursa za ajira waweze kuchukua vijana hao ambao alisema wamehitimu kwa ufaulu mzuri.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya wakala wa vyuo vikuu nje ya nchi, Global Education Link (GEL), Abdlulmalik Mollel, Akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya Mahafali ya nne ya wanafunzi wanaosoma nje.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya wakala wa vyuo vikuu nje ya nchi, Global Education Link (GEL), Abdlulmalik Mollel, Akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya Mahafali ya nne ya wanafunzi wanaosoma nje.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...