Na Mwandishi Wetu


WAKAZI wa nyumba wa lililokuwa Shirika la Saruji Tanzania (Wazo Hill )kwenye kiwanda cha saruji kilichobinafishwa mwaka 1997, wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia ili Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) aweze kutekeleza uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa kuwauzia nyumba hizo kwa kuwa wengi ni wastaafu na ni wazee na Kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi kwenye nyumba hizo.

Akitoa ombi hilo kwa Rais Samia, Mmoja wa watumishi wa zamani wa Taasisi mafunzo ya Saruji (Saruji Training Institute) ambayo ilikuwa taasisi ndani ya shirika la saruji Tanzania, Mzee Wilfred Kaberege amedai kuna uamuzi wa Baraza la Mawaziri na waraka wa Serikali Na 60/2003 wa kuwauzia nyumba hizo wakazi wake.

Amedai kwamba TBA wameshindwa kusimamia uuzaji wa nyumba hizi kwa wakazi wake na kuamua kutoza kodi kubwa ya pango ambayo wengi wa wastaafu hawawezi kumudu.

Akifafanua zaidi kwa niaba ya wenzake amedai Shirika la Saruji Tanzani ilibinafsishwa mwaka 1997, kipindi cha mchakato wa ubinafsishaji mashirika nchini wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu lakini mwekezaji alinunua kiwanda na machimbo na alikataa kuuziwa sehemu ya makazi (nyumba)

Amedai kizuizi ni TBA ambaye alikabidhiwa kusimamia uuzaji wa nyumba hizo na baada ya kushindwa kutekeleza maagizo ya serikali, ameamua kupangisha na kupandisha kodi ambayo wengi wa wastaafu imekuwa mzigo mkubwa kwao.

“Sikia niwaandie ndugu zangu waandishi wa habari ,hatuna ugomvi na TBA na hatuoni sababu ya kulumbana nao ,bali tunacholalamikia ni namna ambavyo taratibu zinazotumika zinashindwa kutujali, tunaona hawa wenzetu wa TBA kama wamekuwa wasumbufu na tayari kuna watumishi wenzetu wa zamani watatu wameondolewa kwenye nyumba hizi na hatujui sababu za kuondolewa kwao, hivyo tunaomba Rais Mama Samia atusaidie kwa kuingilia kati maana tumeshatoa malalamiko yetu kwa viongozi wa ngazi za juu,"Kaberege.

Ameongeza taasisi hiyo nyumba zake za Mbeya, IMTU Hospital Mbezi Beach, Tanga, Morogoro, Sumbawanga, Arusha na Mwanza zote ziliuzwa, ila za Wazo Hill hapa Tegeta ni kizungumguti mpaka leo hii.

Akieleza zaidi kuhusu suala hilo, ambalo limechukua muda mrefu na kuwafanya wakazi hao kuandika barua mara mbili kwa Mhe Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, barua hizo, ambazo blogi hii imeziona, ziliandikwa moja Aprili 27, 2022 na nyingine Desemba 6, 2021 katika juhudi zao za kuhakikisha TBA inawauzia nyumba hizo.

Mmoja mwingine wa Shirika ambaye naye amestaafi( jina limehifadhiwa) na bado anaishi kwenye nyumba hizo, amesema kwa sasa kumekuwa na usumbufu mkubwa unaofanywa na baadhi ya watumishi wa TBA na lengo la usumbufu huo ni njama za kutaka watoke ili wazichukue wao.

"Pamoja na kwamba tunamuomba Rais wetu kuingilia kati bado tunayo imani na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa anaweza kuwa sehemu ya Daraja sahihi la kutuunganisha na Rais kupata ufumbuzi,sisi tuko tayari na barua zetu ambazo tumeandika mpaka kwa Waziri MKuu tunakumbushua kuuziwa nyumba hizi ambazo tumeishi kwa miaka yote,"amesema

Aidha amesema kwa sasa kodi zilizoletwa na TBA ni kubwa na malimbikizo ni makubwa na kuna baadhi ya wakazi wa nyumba hizo wamefutiwa kabisa na wengine wamepewa malimbikizo makubwa ya mamilioni ya shilingi.

“Chakushangaza, baadhi ya wakazi wa nyumba hizo wameondolewa kabisa kodi na kuna baadhi yetu tumepewa malimbikizo makubwa, ambayo hatukutarajia kabisa na sasa ni vitisho kwenda mbele,” amedai.

Amesema kulikuwa na kesi ya msingi katika Mahakama Kuu ya Tanzania na kulikuwa na zuio la kuwataka TBA kutofanya chochote bila kuihusisha menejimenti ya kiwanda, yaani Tanzania Portland Cement Company Limited (TPCC), lakini inaonakana wamekiuka hukumu hiyo.

“Hili eneo lina wakazi wasiopungua 903 na nyumba hizi zipo takribani 132, lakini eneo lenye mgogoro ni ploti 1, 4 na 7. Kwa nini ploti zingine zote zimetulia? Ndiyo maana tunahisi hapa kuna jambo,” alisema mmoja wa wakazi wa nyumba hizo.

Uchunguzi wa Blog hii umebaini na kupata barua iliyowahi kuandikwa na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Marehemu Injinia John Kijazi ya tarehe 25 Novemba 2004 na yenye kumb . Na GB: 128/228/01/90 kwenda kwa Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) juu ya kuuza nyumba zilizokuwa Shirika la Saruji kwa utaratibu wa kiserikali.

Na sehemu ya barua hiyo inasema “ Tumepokea barua yenye Kumb NA .ac.121/510/01 ya tarehe 11/11/2004, kutoka kwa Mhe Waziri wa Viwanda na Biashara ihusuyo kurejeshwa serikalini (Wizara ya Ujenzi) nyumba zilizotajwa hapo juu kwa lengo la kuwauzia wanaoishi ndani ya nyumba hizo. Barua hiyo ni utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri (BLM) kupitia waraka NA: 60/2003.

Wakati barua nyingine ambayo Blog hii imeipata nakala zake ikitoka PSRC kwenda kwa wapangaji wa nyumba za wazo , yenye kumb PSRC/1/13/47 ya tarehe 26 Oktoba 2004 ya kuwataarifu uuzwaji wa nyumba hizo.

Akijibu madai hayo kwenye moja ya vyombo vya habari ( sio Blog hii) Kaimu Meneja wa Usimamizi na Umiliki Fredy Mangula, amenukuliwa akikanusha hizo ambapo amesema serikali imesitisha uuzaji wa nyumba za serikali kwa watumishi na kwa wasio watumishi wa umma.

“Serikali imesitisha zoezi la kuwauzia nyumba za serikali watumishi na wasio watumishi wa umma na hawa wa Wazo, ambao walikuwa watumishi wa Shirika la Saruji Tanzania tumewafanyia tathmini na ndiyo maana tumewapangia kodi stahimilivu,” alisema Bw Mangula.

Mangula amesema kwamba mwaka 2014 ndio walipewa rasmi usimamizi wa nyumba hizo na serikali baada ya ubinafishaji wa kiwanda uliosimamiwa na Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) na baada ya hapo wakaanza kuanza thamini na kuwahakiki wakazi wote wa hizo nyumna za wazo.

“Si kweli kuwa tumepandisha kodi kubwa kiasi ya kwamba hawawezi kulipa tatizo wengi walikuwa na malimbikizo makubwa maana walikuwa hawalipi kitu na kodi zinaanza Sh. 50,000, Sh. 70,000 hadi Sh.100,000 tu,” amesisitiza Mangula .

Kiwanda cha Saruji kilibinafishwa rasmi 1997 kutoka kwenye Shirika la Saruji Tanzania na kuchukuliwa na mwekezaji Tanzania Portland Cement Company Limited (TPCC) kipindi cha awamu ya tatu ambacho mashirika mengi ya umma yaliyoshindwa kujiendesha yalikuwa yanabinafishwa ili kuleta tija.

Pamoja na ufafanuzi huo, Blog hii inaendelea kutafuta wahusika wa TBA ili kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu nyumba hizo na madai ya wastaafu hao.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...